Wednesday, June 6, 2012


                           TAKUKURU YAISHUKIA MAHAKAMA YA ARDHI CHATO


                                       Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Dk Edward Hossea
Na Daniel Limbe,Chato
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wilayani chato mkoani kagera imeishukia mahakama ya ardhi na nyumba wilayani humo kwa madai ya kugeuza ofisi hiyo duka la kuuza haki kwa wananchi kinyume cha sheria,hatua ambayo imepelekea baadhi ya wananchi kupoteza imani na huduma zinazotolewa na mahakama hiyo.
 
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya taasisi hiyo kupitia dawati la utafiti,udhibiti na takwimu kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na utendaji kazi wa mahakama ya ardhi na nyumba wilayani humo,ambapo ilibaini ukiukwaji mkubwa wa uwajibikaji wa watendaji wa sekta hiyo muhimu kwa wananchi.
 
Akizungumza na NIPASHE Kamanda wa Takukuru wilayani chato Ellimius Millanzi alisema kuwa taasisi yake ililazimika kufanya utafiti huo kutokana na malalamiko ya wananchi wengi waliofika katika mahakama hiyo kwa lengo la kupata ufumbuzi wa migogoro ya ardhi zao,na baadaye kutoridhishwa na utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa mahakama hiyo kutokana na kuendekeza vitendo vya kuomba rushwa.
 
Millanzi alisema utafiti huo ulifanyika mwezi machi hadi mei 2012 kwa njia ya mahojiano na wananchi,viongozi na watendaji mbalimbali waliopo kwenye maeneo ya wilaya hiyo ambapo Takukuru ilibaini kesi nyingi zinazofunguliwa dhidi ya serikali zimekuwa zikiisha kwa serikali kushindwa, kutokana na kutotoa rushwa hali ambayo imekuwa ikiisababishia hasara kubwa.
 
Akitoa mfano wa soko la Iparamasa alisema “Kuna mwananchi mmoja aliishtaki serikali ya kijiji cha Iparamasa baada ya kujenga soko kwenye eneo alilodai lilikuwa la kwake na mahakama ya ardhi na nyumba wilayani hapa iliamuru soko hilo kuvunjwa,licha ya kuwa tayari ilikuwa imeshawekeza gharama kubwa kutokana na kodi mbalimbali za wananchi”alisema
 
“ Kama haitoshi mahakama hiyo imekuwa ikilalamikiwa kwa kitendo chake cha kupokea upya kesi ambazo tayari zimekwisha tolewa hukumu na mahakama zingine za juu…kuendesha mashauri na kutoa hukumu bila kwenda kwenye eneo la migogoro…na baadhi ya kesi zimekuwa zikisikilizwa kwa kipindi kirefu baada ya kuahirishwa mara kwa mara pasipo kuwa na sababu za msingi”alisema Millanzi.
 
Mambo mengine ni pamoja na kuishi jijini mwanza badala ya chato ambapo ndiyo kituo chake cha kazi,hivyo kupelekea kushindwa kupata muda wa kutosha kusikiliza kesi za wananchi,kuzitoa mahakamani baadhi ya kesi ambazo walalamikaji wanatoa taarifa za kutofika mahakamani kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa,licha ya kuwepo kwa kesi zingine ambazo walalamikaji walitoa udhuru kwa zaidi ya mara tatu na zinaendelea kuwepo mahakamani hapo kutokana na mazingira ya rushwa.
 
Millanzi aliongeza kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakiilalamikia mahakama hiyo kuwa imekuwa duka la kuuzia haki kwa sababu ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa katika utoaji haki na kwamba mtu anayetoa pesa ndiye amekuwa akishinda kesi,hali  ambayo imepelekea wananchi wengi kutolidhishwa na utendaji kazi wa mahakama hiyo.
 
Kufuatia hali hiyo TAKUKURU imelazimika kupeleka utafiti huo kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya chato Hadija Nyembo kwa lengo la kutaka wadau wa maendeleo ikiwemo Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya,mashirika yasiyo ya kiserikali,Ofisa ardhi maliasili na mazingira,diwani na ofisa tarafa ya chato kujadili na kutoa mapendekezo namna ya kutatua kero zilizopo kwenye mahakama hiyo.
 
Akijibu tuhuma hizo Hakimu wa baraza la ardhi na nyumba wilayani hapa Elias Mogasa alikiri kupokea malalamiko hayo, huku akikanusha vikali ofisi yake kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kwa madai uwajibikaji wa mahakama hiyo imeboreka ukilinganisha na idadi ya kesi zilizokuwepo awali na hivi sasa.
 
Alisema tangu kuanzishwa kwa mahakama hiyo mwaka 2007 kwa lengo la kuhudumia wakazi wa wilaya tatu za Chato,Biharamulo na Ngara zaidi ya kesi 580 zilifunguliwa na kati ya hizo kesi 425 zimeshatolewa maamuzi huku kesi 157 zikiendelea kusikilizwa mahakamani hapo,nakwamba takwimu zinaonyesha kuwa wilaya ya ngara inaongoza kwa kesi nyingi ikifuatiwa na Biharamulo na mwisho ni Chato.
 
Aidha Mogasa alisema kuwa anachokiamini yeye ni kuwa wananchi wana imani na utendaji kazi wa mahakama hiyo kutokana na kulidhishwa na maamuzi yanayotolewa pindi pande mbili zinapo kuwa na mvutano wa migogoro ya ardhi ambayo baadhi yake imekuwa ikitishia uvunjifu wa amani kwa wananchi.
 
Hata hivyo alidai taarifa iliyotolewa na TAKUKURU ni changamoto katika kuongeza uwajibikaji wa mahakama hiyo katika kutenda haki dhidi ya kesi zinazofikishwa hapo.
 
Kwa upande wao baadhi ya wananchi na viongozi wa vyama vya siasa wilayani hapa wameupongeza uamuzi wa taasisi hiyo kufanya utafiti kwenye mahakama hiyo ambayo wamedai kumekuwa na urasimu mkubwa katika upatikanaji wa haki kwa kesi zinazopelekwa hapo kutokana na viongozi wake kupenda rushwa kuliko kutenda haki.
 
Salum Selemani mkazi wa kijiji cha Kalema na Frola Mashauri mkazi wa mkuyuni wamesema TAKUKURU wamefungua ukurasa mpya katika kuhakikisha haki kwa jamii inatendeka kwa kuzuia mianya yote ya rushwa huku wakiishauri kwenda mbele zaidi hasa katika idara ya afya kutokana na baadhi ya wauguzi wilayani humo kuendekeza vitendo vya kuomba rushwa kwa wagonjwa na mama wajawazito ambao hufika kwenye hospital,vituo vya afya na zahanati ili kupata huduma za kiafya.
 
Wamedai kuwa baadhi ya wanawake wajawazito wamekuwa wakiombwa fedha na wauguzi pindi wananpo kwenda kujifungua kwenye hospitali ya wilaya hiyo kinyume cha sheria na kwamba wanapo kaidi hupata matibabu yaliyochini ya kiwango kwa lengo la kuwakomoa.
 
                                                                                                Mwisho.
 

No comments:

Post a Comment