Monday, August 13, 2012


             ASKARI WA KISIWA CHA RUBONDO WATUHUMIWA KWA MAUAJI YA WATU 9

                                                      Hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo.

Na Daniel Limbe,Geita.
CHAMA cha wananchi CUF wilayani geita mkoani hapa kimelaani vikali mauaji ya watu 9 yanayosadikiwa kufanywa na askari wa hifadhi ya kisiwa cha Rubondo katika ziwa Victoria baada ya kuwafyatulia risasi za moto na wengine kuwatosa majini kutokana na kuwatuhumu kujihusisha na uvuvi haramu,huku serikali ya wilaya hiyo ikidaiwa kufumbia macho vitendo hivyo.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya maandishi iliyotolewa kwa waandishi wa habari leo na Katibu wa chama cha CUF wilayani geita Seveline Malugu,Matukio hayo yalitokea kwa nyakati tofauti mwishoni mwa mwaka 2011 hadi 2012 ndani ya ziwa Victoria baada ya askari hao kuwakamata baadhi ya wananchi kwenye maeneo jirani na mpaka wa hifadhi ya kisiwa hicho kisha kuwaua na wengine kuwabambikizia kesi mahakamani kinyume cha sheria.
 
Baadhi ya watu waliodaiwa kufa kwa risasi na wengine kutoswa ndani ya maji ya kina kirefu ni Paschal Mabwete,Selemani Tembo,Jeremiah Mussa,Abel Zacharia,na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Kulwa.
 
Wengine ni Idd Mussa,Shija Shigondo,Baluhya Buzinza na Marco Masanyiwa ambapo katika tukio hilo wawili waliokoka na kifo baada ya kufanikiwa kuogelea hadi nchi kavu  wote walikuwa wavuvi wa mtu aliyefahamika kwa jina la Burhan mkazi wa kisiwa cha Ikuza wilaya ya Muleba mkoani kagera.
 
Katika taarifa ya Chama hicho imekituhumu kitengo cha doria kinachoongozwa na Ofisa doria mkuu Chuwa J. kwa madai kimekuwa kikiboresha mwahusiano mazuri na baadhi ya wawindaji haramu kisha kuingia ndani ya hifadhi hiyo na kuuwa wanyama kinyume cha sheria kwa lengo la kujinufaisha kwa maslahi binafsi.
 
Imeelezwa kuwa hali hiyo ilipekelekea tembo mmoja kuuawa na wawindaji haramu ambapo idara hiyo ililazimika kutumia gharama kubwa kununua mafuta ya kutosha na kuiteketeza kwa lengo la kupoteza ushahidi kwa viongozi wa ngazi za juu.
 
Akizungumza na gazeti hili mjini geita mmoja wa wananchi waliofanyiwa ukatili wa kutisha na askari wa kisiwa hicho Yusuf Nasibu (46) amesema April 26 mwaka huu alipokea taarifa kwa njia ya simu kuwa rafiki zake wamekamatwa na askari wa kisiwa hicho na kwamba ili kuwaachilia walitakiwa kutoa kiasi cha shilingi 100,000 kama faini ya kuvua samaki eneo la hifadhi.
 
Baada ya kuwasiliana na mwajiri wa wavuvi hao waliamua kuchukua boti na kiasi cha fedha zilizohitajika ili kuwalipia faini wavuvi hao,lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida baada ya mwajiri huyo(Jina limehifadhiwa) kutoa kiasi cha pesa zote alizokuwa nazo 600,000 mfukoni ili kulipa shilingi 100,000 il;iyohitajika,askari hao walimwamuru kutoa fedha zote pasipo kurudisha mfukoni kiasi kilichosalia.
 
Nasibu amesema baada ya kupokonywa fedha hizo yeye alihoji sababu ya kuchukua fedha kinyume cha makubaliano,hali iliyosababisha kupelekwa kwenye kambi moja yapo ya ndani ya hifadhi hiyo na kuanza kushambuliwa kwa vipigo vikali kisha kubambikizwa kesi ya kuingia ndani ya hifadhi pasipo kibari cha serikali,kukutwa na nyavu haramu na kutuhumiwa kutoa rushwa ili askari hao wasifanye kazi.
 
Kufuatia hali hiyo Chama hicho kimemwandikia walaka Mkuu wa wilaya ya Geita Omary Manzie kuelezea Ukatili wa kinyama unaofanywa na askari wa kisiwa cha Rubondo na kumtaka kutoa ufafanuzi juu ya mauaji hayo badala ya serikali kukaa kimya na kuyafumbia macho huku wahusiano ya wananchi na askari hao yakizidi kutoweka kila kunapo kucha.
 
Aidha mbali na chama hicho kumwandikia barua mkuu wa wilaya pia,kimemtaka kuunda tume huru kuchunguza vitendo hivyo badala ya kusubiri kupewa taarifa na viongozi wa hifadhi hiyo ambao wanadaiwa wamekuwa wakipotosha maelezo kwa kuhofia kuwajibishwa iwapo itafahamika wazi unyama wanaoutenda.
 
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia tuhuma dhidi yake Ofisa doria wa kisiwa hicho Chuwa alidai yupo safarini na kwamba hawezi kulitolea maelezo swala hilo na kumtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na mhifadhi mkuu wa kisiwa cha Rubondo kwa namba 0782643402 ambaye hata hivyo baada ya kutafutwa kwa simu hakuweza kupatikana.
 
Kadhalika baada ya jitihada za mwandishi wa habari hizi kugonga mwamba alilazimika kumtafuta kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya geita Omary Manzie ambaye pia simu yake ya mkononi haikupatikana mbali na kumtafuta mara kwa mara.
 

                                                            CUF CHAMLIPUA DC GEITA
                                                            ADAIWA KUONGOZA KIBABE
                                                            AWATIMUA WANANCHI OFISINI KWAKE

                                                      Mkuu wa mkoa wa Geita Said Magalula
Na Daniel Limbe,Geita
CHAMA cha wananchi CUF wilayani geita mkoani hapa kimemshitaki mkuu wa wilaya hiyo Omary Manzie kwa mkuu wa mkoa wa huo Said Magalula kwa madai ya kutawala kibabe,kushindwa kutatua kero za wananchi na kuwabagua wananchi wake kwa itkadi za vyama vyao kinyume cha sheria.
 
Hatua hiyo imetokana na malalamiko mbalimbali ya wananchi ambayo yamekuwa yakiwasilishwa kwake kwa ajili ya kuyapatia ufumbuzi lakini baadhi yao huwatimua ofisini mwake kwa madai hana nafasi ya kusikiliza majungu.
 
Katibu wa Chama cha wananchi CUF wilayani geita Sevelin Malugu ameliambia NIPASHE kuwa Mkuu wa wilaya hiyo aliteuliwa na rais Jakaya Kikwete hivi karibuni kwaajili ya kuwatumika wananchi wa wilaya ya geita lakini hali hiyo imekuwa kinyume na matarajio ya wengi kwa kuwa amekuwa limbukeni wa madaraka,hali inayosababisha watu kuhoji sifa za kuteuliwa kwake.
 
“Mimi namuona DC wangu huyo ni limbukeni wa madaraka… kama nafasi aliyonayo anakuwa hivyo,je angepewa ukuu wa mkoa ingelikuwaje..ama angelikuwa kwenye cheo cha mheshimiwa Kikwete si angeliweza kutemea mate watu”alihoji Malugu.
 
Kutokana na hali hiyo Katibu huyo amemwandikia walaka wa maandishi mkuu wa mkoa huo (Magalula ) kuingilia kati mgogoro wa ardhi dhidi ya wananchi wa kijiji cha Nyantorontoro “A” na baadhi ya viongozi Idara ya madini wilayani humo ambao wanadaiwa kumilikisha ardhi ya wananchi kinyume cha sheria.
 
Katika taarifa ya Chama hicho mwekezaji aliyemilikishwa ardhi hiyo kinyume cha sheria ni Majaliwa Maziku, ambaye anadaiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa idara hiyo kisha kumpatia eneo hilo licha ya wananchi wa maeneo hayo kudai hawajaripwa fidia ya ardhi yao .
 
Awali eneo hilo lilikuwa likimilikiwa na wananchi na baadaye mwaka 2004 ardhi hiyo ilichukuliwa na kampuni ya kichina ya  Sino Hidro Company Limited, iliyokuwa ikitengeneza barabara kwa kiwango cha lami kutoka wilayani Geita hadi Buzirayombo wilayani Chato kwa makubaliano ya kuitumia ardhi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu ya mradi huo kisha ingelejea mikononi mwa wananchi hao.
 
Katika mradi huo wananchi hao walitakiwa kuhama maeneo hayo ili kuepuka kupata madhara yatokanayo na shughuli za ulipuaji baruti na vumbi kubwa linalotokana na usagaji wa kokoto kwenye “Crasher” ambapo wananchi hao walilipwa fedha kidogo kwa makubaliano ya miaka mitatu huku wengine wakikosa hata kiasi hicho cha fedha.
 
Hata hivyo baada ya mradi huo kuanza kutekelezwa baadhi ya wananchi walijitokeza na kupeleka malalamiko yao kwa mtendaji wa kjiji cha Nyankumbu kudai kulipwa fidia ya mazao na nyumba zao zilizoharibiwa baada ya milipuko iliyotokea septemba 8 mwaka 2006 kutokana na maeneo yao kutokuwa kwenye orodha ya watu waliolipwa awali.
 
Hatua hiyo ilipelekea mtendaji wa kijiji hicho kumwandikia barua mkuu wa wilaya hiyo Septemba 11 mwaka 2006 ikimuarifu Malalamiko ya kuharibiwa mazao kutokana na milipuko inayotokana na wachina wanaotengeneza barabara ya Geita hadi Buzirayombo,na baadaye Ofisi ya mkuu wa wilaya kuandika barua yenye Kumb. Namba.R. 40/1/VOL.V/147 ya novemba 8 mwaka 2006 kwenda kwa Meneja wa Tanroads Mkoa wa mwanza juu ya uwepo wa malalamiko hayo.
 
Aidha baada ya mradi huo kukamilika mwaka 2007 wananchi walilejea kwenye maeneo yao ya awali na kuendesha maisha yao ya kila siku lakini katika hali ya kushangaza hivi karibuni walipewa taarifa kupitia ofisi ya madini wilayani humo kuwa maeneo hayo yamemilikishwa kwa mwekezaji na kutakiwa kuondoka kwa kuwa tayari walishalipwa fidia ya ardhi zao na kampuni ya Kichina iliyokuwa ikitengeneza barabara.
 
Alipotakiwa kuzungumzia malalamiko hayo Ofisa madini wa kanda ya ziwa Juma Kharuna alikiri eneo hilo kugawiwa kwa mwekezaji na kudai kuwa taratibu zote za kisheria zimezingatiwa kwa kuwa eneo hilo lilikaa wazi kwa muda mrefu mpaka hapo alipojitokeza mwekezaji huyo.
 
Kadhalika Kharuna alimtaka mwandishi wa habari hizi kufanya mawasiliano na Mtendaji wa kata ya Kalangalala Hamad Juma ili kuzungumzia suala hilo kwa kina kutokana na kuufahamu vizuri mgogoro huo wa wananchi dhidi ya serikali.
 
Hata hivyo baada ya mwandishi wa habari hizi kumtafuta kwa njia ya simu mtendaji huyo alikanusha kuwa taarifa sahihi na badala yake kumuomba mwandishi wa habari kumtafuta mkuu wa wilaya kwa kuwa mgogoro huo ulishafika ofisini kwake.

 

Wednesday, August 1, 2012

MADIWANI CHATO WAGEUKA MBOGO KUDAI GARI LA MKURUGENZI

Na Daniel Limbe,Chato
MADIWANI wa halmashauri ya Chato Mkoani Geita wamemtuhumu mwenyekiti na aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo Hamida Kwikwega kuficha gari la serikali kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa huku baadhi yao wakidai gari hilo limeuzwa kwa mtu binafsi kinyume cha sheria.
Wakizungumza kwenye kikao cha baraza jana madiwani hao waligeuka Mbogo,baada ya kumtaka Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Charles Maisha kueleza mahali lilipouzwa gari jipya la halmashauri hiyo STK 5211 aina ya Toyota Land Cruser V8 lililonunuliwa na serikali kwa thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 200.
Hatua hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Diwani wa kata ya Muganza Marco Maduka (CHADEMA)kuomba mwongozo wa Kanuni,na kisha kutaka baraza hilo kupewa taarifa juu ya mahali lilipo gari hilo ambalo ni mali ya halmashauri ya wilaya hiyo.
Awali gari hilo lilikuwa likitumiwa kwa ajili ya matumizi ya Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo,lilifanya kazi kwa muda wa miezi mitatu kisha ikadaiwa kwamba limeharibika Injini na kupelekwa katika moja ya gereji za kutengeneza magari jijini mwanza.
Hata hivyo baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo waligundua kupitia kwa raia wema kwamba gari hilo lilihujumiwa na baadhi ya watumishi wa serikali wakiongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kwa kunyofoa Injini yake na kuiuza kwa mtu binafsi kisha kuweka injini nyingine isiyofaa.
Kufuatia hali hiyo madiwani walikuja juu na kumtaka aliyekuwa mkurugenzi wa halmashauri hiyo (Hamida Kwikwega) kabla ya kuvuliwa madaraka na kuhamishiwa katika sehemu nyingine kikazi,kulirejesha gari hilo na hasa baada ya kubaini kuwa gari hilo lilikuwa limepelekwa kwenye Gereji ya Mumewe waliyoitaja kwa jina la M City.
Vile vile madiwani hao walilazimika kumweleza Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI)Agrey Mwanry wakati alipotembelea halmashauri hiyo mwishoni mwa mwaka jana katika ziara yake,na kudai kuwa gari hilo limefanyiwa njama za kuuzwa injini yake kwa lengo la kuwanufaisha watu wachache.
Katika sakata hilo Naibu Waziri alimsimamisha Mkurugenzi huyo na kumtaka kutoa maelezo juu ya tuhuma hizo ambapo alikiri kwamba gari hilo liliharibika Injini na hivyo kupelekwa Jijini mwanza kwa ajili ya matengenezo ingawa baadhi ya watendaji na hata madiwani hawakupatiwa taarifa.
Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri alimuagiza mkurugenzi kuambatana naye hadi jijini mwanza lilipo gari hilo kwa ajili ya kulishuhudia na baada ya kuliona alimuagiza kulitoa kwenye gereji hiyo iliyokuwa ikidaiwa kuwa ni ya mumewe na kulipeleka TEMESA,hata hivyo lilipofikishwa huko ilibainika kuwa gari hilo halikua na injini yake halali.
Akizungumia sakata hilo katika baraza hilo Diwani wa kata ya Buseresere Chrispine Kagoma (Chadema) alisema taarifa za uhakika ambazo madiwani wamezipata ni kwamba TEMESA wamekataa kulitengeneza gari hilo kwa vile vifaa vingi vya gari hilo ikiwemo injini yake vimenyofolewa na kuuzwa.
“Taarifa sahihi tulizo nazo ni kwamba baada ya sisi kuibua ufisadi huo mbele ya Naibu Waziri,watendaji wanaodaiwa kuliuza gari hilo kwa harakaharaka waliamua kulirejesha gari hilo kwenye gereji ya mume wa aliyekuwa mkurugenzi ili lionekane linatengenezwa,lakini kumbe ilikuwa ni kiini macho,na kibaya zaidi pamoja na Waziri kuagiza lirejeshwe mpaka leo hii bado halijarejeshwa…’’ Alisema Diwani huyo kwa msisitizo.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Ilemela Ismael Luge alisema hawako tayari kuona ufisadi mkubwa kama huo unaendelea kufanyika katika halmashauri hiyo huku wao kama wawakilishi wa wananchi wapo,ambapo alimtaka Mwenyekiti huyo kulirejesha gari hilo hata kama ni bovu ili liwekwe katika eneo la halmashauri hiyo.
“Mwenyekiti hatuko tayari kuendelea kuona vitendo vya kifisadi vikiendelea kufanyika kwenye halmashauri yetu,tunachotaka ni kuona hilo gari linarejeshwa hapa kwenye halmashauri yetu,ni bora lije hapa ili tuwe tunaliona tu inatosha vinginevyo kama haliji basi sisi tufanye maamuzi mazito,lakini kubwa tunahitaji kuliona gari hilo kwa sababu lina thamani kubwa na haliwezi kupotea kienyeji hivyo……’’ alisema Luge.
Akijibu hoja hizo za madiwani ambazo zilijadiliwa na zaidi ya madiwani zaidi ya watamo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo alionekana kutumia ubabe kuiondoa hoja hiyo ya madiwani kwa kueleza kuwa suala hilo linashughulikiwa na taarifa zake tayari zipo na kuamua kuufunga mjadala huo pamoja na kwamba baadhi ya madiwani waliendelea kunung’unika na kisha kuendelea na kikao kwa kujadili ajenda zingine.
Ni miezi minane sasa imepita tangu Naibu Waziri wa TAMISEMI Mwanry kuuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kulirejesha gari hilo,ingawa hadi jana Jumatano lilikuwa halijarejeshwa na hakukuwa na majibu sahihi juu ya Gari hilo.
Halmashauri ya wilaya ya Chato ni miongoni mwa halmashauri zilizokumbwa na kashfa mbalimbali ikiwemo kuhujumu fedha za pembejeo za wakulima zaidi ya shilingi Bilioni 1.3,hali iliyopelekea serikali kuamua kuwawajibisha Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa kumvua madaraka,pamoja na kuwafikisha mahakamani maofisa waandamizi wa Idara ya kilimo wilayani humo kwa tuhuma hizo.