Na Daniel Limbe,Chato
MADIWANI wa
halmashauri ya Chato Mkoani Geita wamemtuhumu mwenyekiti na aliyekuwa
mkurugenzi wa halmashauri hiyo Hamida Kwikwega kuficha gari la serikali
kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa huku baadhi yao wakidai gari hilo
limeuzwa kwa mtu binafsi kinyume cha sheria.
Wakizungumza
kwenye kikao cha baraza jana madiwani hao waligeuka Mbogo,baada ya
kumtaka Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo Charles Maisha kueleza
mahali lilipouzwa gari jipya la halmashauri hiyo STK 5211 aina ya
Toyota Land Cruser V8 lililonunuliwa na serikali kwa thamani ya zaidi
ya Shilingi Milioni 200.
Hatua
hiyo ilikuja muda mfupi baada ya Diwani wa kata ya Muganza Marco Maduka
(CHADEMA)kuomba mwongozo wa Kanuni,na kisha kutaka baraza hilo kupewa
taarifa juu ya mahali lilipo gari hilo ambalo ni mali ya halmashauri ya
wilaya hiyo.
Awali
gari hilo lilikuwa likitumiwa kwa ajili ya matumizi ya Mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya hiyo,lilifanya kazi kwa muda wa miezi mitatu
kisha ikadaiwa kwamba limeharibika Injini na kupelekwa katika moja ya
gereji za kutengeneza magari jijini mwanza.
Hata
hivyo baadhi ya madiwani wa halmashauri ya wilaya hiyo waligundua
kupitia kwa raia wema kwamba gari hilo lilihujumiwa na baadhi ya
watumishi wa serikali wakiongozwa na aliyekuwa Mkurugenzi wa
halmashauri hiyo kwa kunyofoa Injini yake na kuiuza kwa mtu binafsi
kisha kuweka injini nyingine isiyofaa.
Kufuatia
hali hiyo madiwani walikuja juu na kumtaka aliyekuwa mkurugenzi wa
halmashauri hiyo (Hamida Kwikwega) kabla ya kuvuliwa madaraka na
kuhamishiwa katika sehemu nyingine kikazi,kulirejesha gari hilo na hasa
baada ya kubaini kuwa gari hilo lilikuwa limepelekwa kwenye Gereji ya
Mumewe waliyoitaja kwa jina la M City.
Vile
vile madiwani hao walilazimika kumweleza Naibu Waziri wa Tawala za
Mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI)Agrey Mwanry wakati alipotembelea
halmashauri hiyo mwishoni mwa mwaka jana katika ziara yake,na kudai
kuwa gari hilo limefanyiwa njama za kuuzwa injini yake kwa lengo la
kuwanufaisha watu wachache.
Katika
sakata hilo Naibu Waziri alimsimamisha Mkurugenzi huyo na kumtaka kutoa
maelezo juu ya tuhuma hizo ambapo alikiri kwamba gari hilo liliharibika
Injini na hivyo kupelekwa Jijini mwanza kwa ajili ya matengenezo ingawa
baadhi ya watendaji na hata madiwani hawakupatiwa taarifa.
Kufuatia
hali hiyo Naibu Waziri alimuagiza mkurugenzi kuambatana naye hadi
jijini mwanza lilipo gari hilo kwa ajili ya kulishuhudia na baada ya
kuliona alimuagiza kulitoa kwenye gereji hiyo iliyokuwa ikidaiwa kuwa
ni ya mumewe na kulipeleka TEMESA,hata hivyo lilipofikishwa huko
ilibainika kuwa gari hilo halikua na injini yake halali.
Akizungumia
sakata hilo katika baraza hilo Diwani wa kata ya Buseresere Chrispine
Kagoma (Chadema) alisema taarifa za uhakika ambazo madiwani wamezipata
ni kwamba TEMESA wamekataa kulitengeneza gari hilo kwa vile vifaa vingi
vya gari hilo ikiwemo injini yake vimenyofolewa na kuuzwa.
“Taarifa
sahihi tulizo nazo ni kwamba baada ya sisi kuibua ufisadi huo mbele ya
Naibu Waziri,watendaji wanaodaiwa kuliuza gari hilo kwa harakaharaka
waliamua kulirejesha gari hilo kwenye gereji ya mume wa aliyekuwa
mkurugenzi ili lionekane linatengenezwa,lakini kumbe ilikuwa ni kiini
macho,na kibaya zaidi pamoja na Waziri kuagiza lirejeshwe mpaka leo hii
bado halijarejeshwa…’’ Alisema Diwani huyo kwa msisitizo.
Kwa
upande wake Diwani wa kata ya Ilemela Ismael Luge alisema hawako tayari
kuona ufisadi mkubwa kama huo unaendelea kufanyika katika halmashauri
hiyo huku wao kama wawakilishi wa wananchi wapo,ambapo alimtaka
Mwenyekiti huyo kulirejesha gari hilo hata kama ni bovu ili liwekwe
katika eneo la halmashauri hiyo.
“Mwenyekiti
hatuko tayari kuendelea kuona vitendo vya kifisadi vikiendelea
kufanyika kwenye halmashauri yetu,tunachotaka ni kuona hilo gari
linarejeshwa hapa kwenye halmashauri yetu,ni bora lije hapa ili tuwe
tunaliona tu inatosha vinginevyo kama haliji basi sisi tufanye maamuzi
mazito,lakini kubwa tunahitaji kuliona gari hilo kwa sababu lina
thamani kubwa na haliwezi kupotea kienyeji hivyo……’’ alisema Luge.
Akijibu
hoja hizo za madiwani ambazo zilijadiliwa na zaidi ya madiwani zaidi ya
watamo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo alionekana kutumia ubabe
kuiondoa hoja hiyo ya madiwani kwa kueleza kuwa suala hilo
linashughulikiwa na taarifa zake tayari zipo na kuamua kuufunga mjadala
huo pamoja na kwamba baadhi ya madiwani waliendelea kunung’unika na
kisha kuendelea na kikao kwa kujadili ajenda zingine.
Ni
miezi minane sasa imepita tangu Naibu Waziri wa TAMISEMI Mwanry
kuuagiza uongozi wa halmashauri ya wilaya hiyo kulirejesha gari
hilo,ingawa hadi jana Jumatano lilikuwa halijarejeshwa na hakukuwa na
majibu sahihi juu ya Gari hilo.
Halmashauri
ya wilaya ya Chato ni miongoni mwa halmashauri zilizokumbwa na kashfa
mbalimbali ikiwemo kuhujumu fedha za pembejeo za wakulima zaidi ya
shilingi Bilioni 1.3,hali iliyopelekea serikali kuamua kuwawajibisha
Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa kumvua madaraka,pamoja na
kuwafikisha mahakamani maofisa waandamizi wa Idara ya kilimo wilayani
humo kwa tuhuma hizo.
No comments:
Post a Comment