Saturday, July 28, 2012

KUKU WA AJABU AIBUKA SENGEREMA AKIWA NA HIRIZI,SHANGA NA CHALE.



WAKAZI wa mtaa wa barabara ya Nyanchenche mjini Sengerema juzi walifurika kushuhudia tukio la ajabu lisilokuwa la kawaida baada ya kuonekana kuku dume wa ajabu akiwa hana manyoya na akitembea huku akiwa amefungwa shanga na hilizi mbili shingoni na mabawa yake yakiwa yamechanjwa chale na kupakwa dawa nyeusi za kienyeji.

Tukio hilo lililovuta umati mkubwa wa watu lilitokea juzi majira ya saa 7:00 mchana kwenye moja ya familia ya mtaa huo[jina limehifadhiwa]ambaye alidai kwamba kuku huyo alijitokeza nyumbani kwake bila kufahamu alikotokea.

Kuku huyo wa ajabu alikutwa na wananchi katika mji huo ambao uko kando kando ya barabara,jambo ambalo limeshituwa mamia ya wananchi wa mji wa Sengerema ambao walifika katika eneo hilo ili kushuhudia tukio hilo ambalo wamelihusisha na imani za kishirikina.

Katika tukio hilo la kuonekana kuku wa ajabu hakuna hata mwananchi aliyejitokeza kumshika kuku huyo huku wenyeji wa mji husika wakiendelea na shughuli zao licha ya kuonyesha mshituko wa tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa kitongoji hicho Leah James alionyesha kushangazwa na tukio hilo na kusema kuwa ni la ajabu haijawahi kutokea jambo kama hilo katika kitongoji hicho ambalo limeibuwa hisia tofauti miongoni mwa wanajamii.

“Nimepata taarifa za tukio hili ilikuwa mchana muda wa saa saba na tumefika mpaka eneo la tukio ….kwa kweli inashangaza na kusikitisha huyo kuku wa ajabu hana nyoya hata moja wala alama ya kidonda na amechanjwa chale kwenye mbawa zake,kavishwa hilizi mbili shingoni na amefungwa shanga kwenye mbawa zake”alisema mwenyekiti.

Baada ya tukio hilo uongozi wa eneo hilo na jeshi la jadi sungusungu uliamuwa kuitisha mkutano siku iliyofuata leo(jana) ambapo walifuatilia na kumbaini mmiliki wa kuku huyo kuwa ni  Leticia Makoye ambaye alidai kuku huyo ni wake na  humtumia katika shughuli za uganga wa kienyeji .

Kikao hicho kiliamua kumrudishia kuku huyo ingawa alikuwa amekufa kutokana na kupigwa baridi usiku kucha,maamuzi yaliyopingwa na wananchi na hivyo kulazimika kumshambulia kwa mawe hadi nyumbani kwake huku viongozi wa mtaa huo wakimpatia ulinzi hadi alipoingia ndani ya nyumba.

Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili eneo la tukio wamekuwa na hisia tofauti huku baadhi yao wakilihusisha na imani za kishirikina kutokana na vitu alivyokutwa navyo kuku huyo ikiwa ni pamoja na shanga,hilizi,na chale alizochanjwa kwenye mbawa zake.

Baadhi ya wananchi hao Grece Michael (32) Fadhili Alfani (45) na Daniel Marco walisema kuanza kutokea kwa matukio ya ajabu kama hilo ni dalili za mwisho wa dunia kutokana na vitendo vya kishirikina kuongezeka na kwamba njia pekee ya kuepukana navyo ni kudumu katika sara na imani ndiyo njia pekee.
                                 Mwisho.

1 comment: