Saturday, July 14, 2012

                                        JIMBO LA MAGUFULI VIPANDE VIPANDE
                                        MHADHIRI WA CHUO KIKUU MZUMBE ATIMKIA CHADEMA
                                        MAKADA WENGINE SABA WASALIMISHA KADI ZAO

 Kushoto Mkurugenzi wa ulinzi na usalama Chadema taifa Bw, Wilfred Lwakatare akipokea kadi ya CCM na Kumkabidhi Kadi ya Chadema Dk Benedicto Lukanima (jana) muda mchache baada ya kujiunga na Chama hicho.

Na.Daniel Limbe,Chato.
MKURUGENZI wa ulinzi na usalama wa Chadema taifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho mkoani Kagera Wilfred Lwakatare amezidi kuzibomoa ngome za Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli,baada ya wanachama 72 wa Chama cha Mapinduzi wakiwemo makada 8 wa chama hicho katika jimbo la Chato mkoa mpya wa geita kukihama na kujiunga na Chadema.
 
Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Chato kwenye mkutano wa hadhara jana Lwakatare alidai kushangazwa na uwezo wa Dk Magufuli kutunza takwimu za mambo mbalimbali ikiwemo wingi wa samaki ndani ya maziwa,mito,bahari sanjari na barabara zilizopo nchini lakini takwimu hizo zimeshindwa kuwasaidia wananchi wa jimbo lake katika kutatua tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama licha kuwepo ziwa victoria katika umbali wa nusu kilometa.
 
Alisema kuwa Dk Magufuli hana uwezo wa kuwatumikia wananchi wake kutokana na kuwa kwenye chama cha watu mafisadi wasio na aibu ya mwenyezi mungu kutokana na baadhi ya viongozi wa serikali ya chama hicho kuhujumu raslimali za taifa na kuzificha nje ya nchi kwa lengo la kuongopa kufahamika kwa wananchi.
 
“Kama mnafuatilia vizuri vyombo vya habari,juzi bungeni kuna mbunge aliyeeleza wazi kuwa kunakiasi cha zaidi ya shilingi 300 bilioni zimeibwa na baadhi ya viongozi wa serikali na kuzificha kwenye benk ya uswis ili wananchi tusijue…kiasi hiki cha fedha ni kikubwa sana kiasi kwamba kwa bajeti nzima ya halmashauri ya chato ya mwaka 2012/13 kiasi cha bilioni 12…fedha hizi zilizoibwa iwapo zingetolewa kwenye halmashuri yenu zingetumika kwa miaka 24 pasipo serikali kutoa fedha.
 
Kauli hizo zilipelekea baadhi ya wanachama 72 wakiwemo makada wanane wa Chama cha Mapinduzi kukihama na kujiunga na Chadema hatua iliyotofasiriwa kuwa ni kuvunjwa kwa ngome za mbunge wa Chato,baada ya wanachama wengine 27 wakiwemo makada 7 wa chama hicho kukihama na kujiunga na Chadema mwezi mei 2012.
     
Baadhi ya makada wa CCM waliokihama chama hicho ni pamoja na aliyewahi kupambana na Dk Magufuli katika kinyang’anyiro cha kusaka nafasi ya kuwania ubunge wa jimbo hilo kupitia chama cha mapinduzi kwenye kura za maoni za mwaka 2010 Dk.Benedicto Lukanima ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Mzumbe Morogoro ambaye alishika nafasi ya pili kati ya wagombea wanne wa chama hicho.
 
Wengine waliokihama cha hicho ni Cosmas Kabitelanya mwenyekiti wa kitongoji cha Nyisanzi,Mashaka Sululu kitongoji cha Dodoma,Charles Ngoloma kitongoji cha Nyasenga,kada aliyewahi kuwa mwenyekiti wa ccm tawi la Busaka mwaka 2006/08 Josephat Manyenye na aliyekuwa mjumbe wa mkutano mkuu  Uvccm mkoa Makonzere Phinias.
 
Wanachama hao walikihama cha hicho jana kwenye mkutano wa hadhara wa chadema uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Chato na kuhudhuria na mamia ya wakazi wa wilaya hiyo,ambapo walisema wamelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kuona CCM kinpoteza mwelekeo wa kisiasa kutokana na kukumbatia mafisadi waliohujumu rasilimali za Taifa huku wananchi wakibaki kuwa masikini wa kutupwa.
 
Mara baada ya kukabidhi kadi ya CCM kwa mgeni rasmi Dk.Lukanima alisema kuendelea kuwa kwenye chama cha mapinduzi ni sawa na kukubali kuendelea kuwa mtumwa hivyo hayupo tayari kuendelea kukaa kwenye chama ambacho tayari kimewakatisha tamaa wananchi kwa kuwasababishia umaskini wa kutupwa.
 
“Kukubali kuendelea kuwa ndani ya CCM ni sawa na kuwa mtumwa kwa kuwa wengi wao hujinufaisha matumbo yao kinyume na dhamira ya mwasisi wa chama hicho hayati Mwalimu Julias Nyerere ambaye alihitaji kuwa Chama cha wakulima na wafanyakazi..cha kutetea maslahi ya wanyonge…lakini kimekuwa cha kuwanyonya wananchi’’alisema Dk.Lukanima na kuongeza.
 
“Mimi na elimu yangu siwezi kuendelea kuwa ndani CCM kana kwamba nimelogwa..dunia imeniamini kuwa daktari elimu ambayo inategemewa na jamii kuisaidia katika kutenda mema..hivyo siwezi kukubali kula sahani moja na mafisadi huku wananchi wakiendelea kutaabika kwa kukosa huduma mbalimbali za elimu,afya na maji’’
 
Alisema moja ya malengo yake baada ya kukihama CCM na kujiunga na Chadema ni kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kweli katika kuwakomboa wananchi wa Tanzania wakiwemo wa jimbo la Chato ambao wameshindwa kutengenezewa vichocheo vya kiuchumi ili kukabiliana na lindi la Umasikini unao wakabili.
 
Hatua hiyo imekuja huku kukiwa na taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa tayari kuna diwani mmoja maalufu katika halmashauri ya chato ambaye jina leke limehifadhiwa na kata anayotoka kuwa anajiandaa kulejesha kadi ya CCM na kujiunga na Chadema wakati wowote.
 

No comments:

Post a Comment