Sunday, July 8, 2012

                   SERIKALI YAWATAKA WAUZAJI MADAWA KUZINGATIA SHERIA


Baadhi ya wauzaji wa madawa muhimu ya binadamu wakiwa katika maandamano wakati wa   kuhitimu mafunzo ya siku 35 wilayani Chato.
Na Daniel Limbe,Chato
SERIKALI ya wilaya ya Chato mkoani geita imewataka wauzaji wa maduka ya dawa muhimu za binadamu kuzingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa maduka hayo ili kunusuru vifo ambavyo vimekuwa vikitokea kutokana na wauzaji wengi kutokuwa na taaluma hiyo na kwamba serikali ya wilaya hiyo haitawavumilia watu wote watakaoendela kutoa dawa pasipo kuzingatia misingi ya sheria.
Akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya utoaji wa dawa muhimu za binadamu jana (leo) Katibu tawala wa wilaya ya chato Cosmas Lugora alisema kwa muda mrefu wamiliki wa maduka ya dawa baridi ya binadamu wamekuwa wakiendesha shughuli zao pasipo kuzingatia baadhi ya taratibu na kanuni za utoaji wa dawa hali ambayo imekuwa ikihatarisha maisha ya wananchi kutokana na kupewa dawa pasipo maelekezo sahihi.
Alisema dawa ni tiba iwapo ikitolewa kwa kuzingatia taratibu lakini pia ni sumu iwapo itatumiwa kinyume hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya wananchi na kusababisha kupoteza nguvu kazi ya taifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya mkurugenzi mkuu wa Mamalaka ya Chakula na dawa nchini,iliyotolewa na Meneja wa TFDA kanda ya ziwa Seth Kisenge uchunguzi uliofanywa na wizara ya afya  kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Management Sciences for Health (MSH) mwezi aprili hadi mei 2001 walibaini ukiukwaji mkubwa wa utoaji huduma kwenye maduka ya madawa nchini,hali ambayo ilikuwa ikihatarisha maisha ya wananchi kutokana na tamaa za fedha kwa wamiliki wa maduka hayo.
Baadhi ya mambo waliobaini katika uchunguzi huo ni pamoja na wauzaji kutokuwa na elimu ya utoaji tiba,kuuza dawa moto na zisizosajiriwa kisheria badala ya dawa baridi za binadamu,kutoa mimba,kudunga sindano,kufunga vidonda na kulaza wagonjwa.
“Baada ya serikali kupitia mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la MSH tulibaini ikiukwaji mkubwa wa uendeshwaji wa maduka ya dawa baridi kutokana na kuuza dawa wasizoruhusiwa kisheria na kutoa huduma za kitabibu kinyume na maadili,hatua aliyopelekea seriakali kubuni mpango mkakati wa kuwaelimisha wamiliki na wauzaji wa maduka hayo”alisema
Kisenge alisema lengo la Mamlaka ya Chakula na dawa ni kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma sahihi kupitia kwa wauzaji dawa wenye ujuzi uliothibitishwa na serikali ikilinganishwa hali ilivyokuwa awali ambapo wauzaji wengi walikuwa wakitoa huduma hiyo kutokana na mazoea hali ambayo haitakiwi kisheria.
Alisema katika mafunzo maalumu ya wauzaji wa maduka ya madawa baridi ya binadamu ambayo yanatarajiwa kupandishwa hadhi na kuwa maduka muhimu ya dawa yameonyesha mafanikio makubwa zaidi hasa katika mkoa wa Ruvuma ambako utekelezaji wake ulianza tangu februali 2002.
Aidha alisema mpango huo umetekelezwa katika mikoa 15 ya Tanzania na kuonyesha mafanikio makubwa baada ya wauzaji hao kutambua sheria na kanuni za utoaji wa sahihi wa dawa,kuelewa mbinu za magonjwa yatokeayo mara kwa mara katika jamii,huduma kwa magonjwa ya watoto,stadi za mawasiliano na elimu ya ukimwi na ushauri nasaha.
Alizitaja mikoa zilizoinufaika mafunzo hayo kuwa ni Ruvuma,kigoma,Manyara Lindi,Mbeya,Shinyanga,Pwani ,Dododma,Mara,Iringa,Singida,Tanga,Mtwara,Morogoro na rukwa huku mikoa mingine sita ikiwemo Kagera ikiendelea kupatiwa mafunzo hayo kwa kuzingatia uwezo wa seriakali.
Mganga mkuu wa wilaya ya chato Dk Athanas Ngambakubi alisema mafunzo hayo ya siku 35 yatakuwa yamewasaidia kuongeza uelewa na mbinu sahihi za utoaji huduma kwa wagonjwa wao ukilinganisha na awali.
Vilevile Ngambakubi alisema iwapo dawa zikitumiwa kwa usahihi huleta matunda yaliyokusudiwa na dakatari  pamoja na  jamii,lakini kinyume chake zikitumika isivyofaa hugeuka na kuwa sumu hivyo husababisha madhara makubwa ambayo hayakukusudiwa.
Aidha katika risala ya wahitimu wa mafunzo hayo iliyosomwa kwa niaba yao na Rachel Kassawa walidai kabla ya mafunzo hayo walikuwa wakiuza dawa kiholela pasipo kuzingatia sheria namba moja ya mwaka 2003 na kanuni ya sheria hiyo namba 122 (H) na kwa,mba mafunzo hayo yamewafanya kutambua Sheria,Kanuni na Miongozo ya uendeshaji wa maduka ya dawa muhimu.
Hata hivyo katika mahafari hayo wahitimu 81 walioshiriki kwenye mafunzo hayo walitunukiwa vyeti vinavyotambuliwa na serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii,hatua itakayowasaidia kuongeza soko la ajira yao sanjari na kukua kwa mishahara yao ukilinganisha ha ilivyo hivi sasa.

                                                                                                     Mwisho.

No comments:

Post a Comment