Sunday, February 3, 2013

                           WATAHADHARISHWA NCHI KUIGAWA VIPANDE.

Na Daniel Limbe,Geita

MAKAMU mwenyekiti wa jukwaa la katiba Tanzania Israel Ilunde
amewatahadharisha wananchi juu ya utoaji maoni ya uandikwaji wa katiba mpya ya Tanzania kutokana na baadhi yao kuonyesha nia ya kuigawa nchi vipande vipande.

Ametoa rai hiyo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wadau wa asasi zisizo za kiserikali juzi kwenye mdahalo wa katiba kwenye kata za Busanda,Katoro na Kalangalala wilayani geita mkoani hapa.

Mdahalo huo umeandaliwa na mtandao wa mashirika yasiyokuwa ya kiserikali mkoani geita (GENGOP) kwa ufadhili wa shirika la kutoa ruzuku kwa asasi za kiraia la The Foundation for Civil Society.

Ilunde alisema haitawezekana kupatikana katiba mpya yenye mawazo mazuri iwapo watanzania hawatakuwa tayari kutoa mawazo mazuri yenye kuzingatia amani,upendo na mashikamano kwa taifa.

Alisema hivi sasa Tume ya mabadiliko ya Katiba nchini imeanza kupokea maoni kutoka makundi maalumu ikiwemo asasi zisizo za kiserikali, hivyo ninafasi nyingine muhimu kwa wananchi na asasi za kiraia kutoa michango yao ya mawazo ili wao kama mtandao waweze kuwasilisha mawazo hayo kwenye tume hiyo.

Alidai kuwa kinachofanywa na mtandao wa mashirika yasiyo ya kiserikali mkoani hapa ni kusikiliza mapendekezo ya wananchi kisha wao kuyawasilisha kwenye Tume ya mabadiliko ya katiba kwa niaba ya asasi na wala siyo kukusanya maoni kwa kuwa wajibu huo ni kazi ya tume pekee.

Kwa upande wake Mratibu wa mtandao wa mashirika hayo mkoani geita Isaka Kubini amefafanua kuwa mdahalo huo ni moja kati ya mingine inayotarajiwa kufanyika kwenye majimbo ya Geita Busanda na Nyang’hwale.

Hiyo itafanyika kwa lengo la kuimalisha uhusiano wa wananchi na
wabunge majimboni kwa kushirikisha asasi zisizo za kiserikali, wafanyakazi,vijana, walemavu,wanawake,wanafunzi,

wazee,wakulima na wafanyabiashara.

Baadhi ya wananchi walieleza mapendekezo yao katika uundwaji wa katiba mpya ya Tanzania,kuwe na kipengele maalum kitakacho ruhusu wananchi kuwakataa wabunge kwenye majimbo yao iwapo wataonekana kushindwa kuwasaidia badala ya kusubiri kukamilika kwa kipindi chao cha miaka mitano.

Kipengele hicho kionyeshe kisheria iwapo wananchi watajiorodhesha na kufikia aslimia 30 ya watu waliomchagua mbunge husika,wawe na uwezo wa kumkataa kisha kuondolewa nafasi yake katika kuwawakilisha wananchi Bungeni,kabla ya kufanyika uchaguzi mwingine.

Joseph Mangilima mkazi wa kalangalala alisema ili wabunge waweze kuwajibika kikamilifu kwa wananchi kunahaja kubwa kwa katiba ijayo kuruhusu wananchi kuwakataa kabla ya kumalizika kwa vipindi vyao.

Hatua hiyo inatokana na baadhi ya wawakilishi hao Bungeni kubweteka na kushindwa kuwasaidia wananchi waliowachagua katika majimbo yao huku wengine wakidai wamepata ubunge kutokana na fedha zao,hivyo huonekana wanakusanya fedha walizotumia.

Kutokana na hali hiyo wananchi wamekuwa wakiteseka kwa zaidi ya miaka 5 tangu uchaguzi unapomalizika huku wakishindwa kuwawajibisha wabunge hao kutokana na kukosekana sheria inayotambulika kikatiba inayowaruhusu wananchi kuwakataa iwapo watashindwa kuwawakilisha vyema.

Kadhalika Mangilima ambaye pia ni mwakilishi kutoka mgodi wa dhahabu wa GGM,amesema katiba ijayo itamke wazi kuwa mapato yatokanayo na uwekezaji katika migodi hapa nchini aslimia 30 ya mapato hayo ilejeshwe kwa wananchi wa eneo husika ili iwe rahisi kwao kunufaika na raslimali waliyojaliwa na mwenyezi mungu.

Mapendekezo hayo yamekuja huku kukiwa na mvutano mkali dhidi ya serikali na wananchi kufuatia sakata la ujenzi wa bomba la
kusafirishaji wa gesi asili kutoka Mtwara hadi Dar es salaam,hatua
inayodaiwa kuwa na usiri mkubwa katika mradi huo kiasi cha wananchi kutaka kupata ufafanuzi wa kina.

Mwenyekiti wa chama cha wazee wa wilaya ya Geita Laurent Galani amesema ili kupata katiba bora kwa manufaa ya watanzania kuna kila sababu ya kuingizwa kipengele cha kutambua haki za wazee na pindi wanapofikisha umri wa kuanzia miaka 60 wapewe Ruzuku na serikali kila mwaka hadi mauti yatakapo wakuta.

Kwa upande wake Asteria Chozaile mkazi wa kijiji cha shilabela,ameomba katika uandikwaji wa katiba mpya kiwekwe kipengele cha shule za wasichana za kidato cha tano na sita katika kila kata nchini ili kuinua kiwango cha elimu kwa watoto wa kike badala ya ilivyo katika katiba ya sasa ambayo haikutofautisha na kutoa fursa kuwa kwa wasichana.

Shaban Malesa ambaye ni mlemavu wa viungo na mkazi wa kijiji cha katoro,geita amesema katiba ijayo itoe elimu na matibabu bure kwam walemavu wa aina zote sanjari na kuwapatia ajira pasipo vikwazo kutokana na taaluma zao.

                                            Mwisho.