Saturday, September 1, 2012




                                MBIO ZA MWENGE WA UHURU ZAENDELA KUINGIA DOSARI GEITA
                                BENDERA YA TAIFA YAZUA TAFRANI CHATO.
Na Daniel Limbe,Geita
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mbio za Mwenge wa uhuru juzi ziliendelea kuingia dosari katika Mkoa mpya wa geita baada ya Waandishi wa habari pamoja na Madereva waliokuwa kwenye msafara wa mbio za Mwenge katika Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita, kujikuta katika wakati Mgumu baada ya kuzuiwa kula chakula na Ofisa usalama wa Taifa wa Wilaya hiyo Sunday Steven.
Tukio hilo liliwakera madereva waliokuwa wakiendesha magari kwenye msafara huo na kulazimika kuingia kwenye mgomo,kabla ya mgomo huo kunusuriwa na kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka huu Kapteni Honest Mwanossa.
Baada ya kumaliza kula chakula katika chumba maalum katika shule ya msingi Lugunga kiongozi wa mbio za mwenge alitoka nje na kuwafuata madereva hao waliokuwa wamejikusanya katika kundi moja wakijadili kugoma kuendesha magari hayo na kuwaomba kwenda kula chakula katika chumba hicho.
Haikufahamika mara moja mtu aliyempa taarifa kiongozi huyo wa mbio za mwenge kwamba madereva hao walikuwa wamenyimwa chakula na kwamba walikuwa katika harakati za kugomea safari,ambapo katika hali isiyokuwa ya kawaida alipomaliza kunawa alikwenda moja kwa moja na kuwafuata madereva hao mahali walipokuwa na kuwaelekeza mahali pa kula chakula.
Vilevile Mwanossa aliendelea na zoezi la kuwasaka madereva wengine ambao walionekana hawako katika mazingira hayo ambapo alikuwa akimsaka mmoja baada ya mwingine na kumpeleka kwenye chumba cha chakula,na baada ya hapo safari ikaanza,hata hivyo alionekana kukerwa na hali hiyo.
Madereva hao zaidi ya 11 walikumbana na mkasa huo kwa kile kilichoelezwa  na ofisa ulasama huyo wa wilaya kwamba chakula hicho kilikuwa kimeandaliwa kwa ajili ya viongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa,Mkoa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 8:26 mchana katika kijiji na kata ya Lugunga  wakati madereva hao  wakiwa kwenye foleni ili kupata chakula na baadaye kuendelea na msafara hadi katika shule ya sekondari Masumbwe kuzindua klabu ya kupambana na rushwa.
Walipokumbana na mkasa huo kutoka kwa ofisa usalama wa taifa walienda kujadili kuhusu suala hilo umbali wa mita 100 kutoka kwenye moja vyumba vya madarasa lililokuwa likitumika kama chumba cha kupatia chakula cha mchana katika shule ya msingi Lugunga.
Katika majadiliano hayo madereva walikubaliana kususia kuendelea na msafara wa mbio za mwenge wa uhuru kwa kuwa hawakuwa katika orodha ya wageni waliotakiwa kupata chakula hicho,kitendo ambacho kiliwafanya baadhi yao kukaa mbali na magari yao.
Pia mkasa kama huo uliwakumba waandishi wa habari sita waliokuwa wameambatana na msafara huo kutoka mkoani na wilayani humo baada ya ofisa usalama huyo kuwazuia kupata chakula cha asubuhi kilichokuwa kimeandaliwa katika ya sekondari Isangijo kata ya ushirika ambapo kiongozi wa mbio hizo aliweka jiwe la msingi kwenye chumba cha maabara.
Ofisa huyo alitumia kauli ya kwamba wanaotakiwa kupata chakula walikuwa wageni wa kitaifa na kimkoa licha ya miongoni mwa wanahabari hao kutoka mkoani ambao walikuwa wameambata na mbio za mwenge tangu ulipoingia katika mkoa wa Geita agosti 26,mwaka huu.
Mkuu wa wilaya hiyo Husna Mwilima ambaye naye alionekana kukerwa na kitendo cha Ofisa usalama huyo,alizungumza baadaye na waandishi wa habari na kuwaomba radhi kwa yote yaliyojitokeza,na kuwataka kuendela na zeozi hilo la kukimbiza mwenge katika wilaya hiyo.
"Jamani Ndugu kila binadamu ana mapungufu yake,naomba mumsamehe alikua hajui alitendalo,namuombea msamaha wa dhati kabisa,jamani wilaya yangu ni Mpya,na naweza kuwathibitishia kwamba wilaya mama (Bukombe) imenitenga sana katika zoezi hili nimhangaika sana na huyu ofisa usalama yanwekena amechanganyikiwa....'' alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.
Hatua hiyo ilikuja siku moja baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti habari za mkuu wa wilaya ya Geita Omary Mangochie  kupoteza mbio za mwenge wa uhuru baada ya kupitiliza mradi  mmoja uliotarajiwa kukaguliwa na kiongozi wa mbio hizo Kapten Mwanosa katika kijiji cha Nyamalimbe.
Tukio hili lilitokea baada ya kiongozi huyo kupitiliza umati mkubwa wa watu waliokuwa wamepanga foleni barabarani kusubiri kuupokea mwenge huo ili kukagua na kutoa mkopo  kwenye kikundi cha mikopo na akiba cha kijiji hicho.
Baada ya mbio hizo kukimbia umabli wa kilomita 3,kiongozi huyo alipoipitia ratiba ya mkoa aligundua kupitilizwa mradi huo huku mkuu wa wilaya akiwa amekaa kimya kitendo kilichoonekana kumkera na la kulazimika kuusimamisha msafara na kuhoji kabla ya kuamua kuendelea na msafara huo.
Mbali na hilo Mwanossa alionekana kukerwa na mapokezi ya mwenge huo katika wilaya ya chato baada ya kuufikisha mwenge wa uhuru kwenye uwanja wa mkesha na kukuta hakuna maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kutokuwepo Bendera ya taifa.
“Huu ni mwenge wa uhuru ambao tunaukimbiza kitaifa…nasikitika kufika hapa kwenye mkesha wa mwenge huu lakini sijaona bendera ya taifa ikipepea mahari hapa”alisema
Kutokana na kauli hiyo baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo ambao hawakujulikana majina yao haraka walilazimika kuwaagiza baadhi ya vijana ambao wapo kwenye mafunzo mgambo wilayani humo kwenda kung’oa bendera iliyokuwa imesimikwa kwenye ofisi za kata ya chato na kuikimbiza haraka kwenye uwanja wa mkesha wa mwenge huo.
Awali akikagua baadhi ya miradi ya maendeleo kwenye wilaya hiyo Mwanossa alidai miradi mingi aliyojionea aslimia kubwa imejengwa chini ya kiwango licha ya kuwa pesa nyingi za serikali zikionekana kutumika katika miradi hiyo.
                                                                                 Mwisho.


                  MSUKUMA AOMBA KUNUSURU JAHAZI LA CCM GEITA.
                                Katibu wa itkadi na uenezi wa CCM Nape Mnauye.

Na Daniel Limbe,geita
ALIYEKUWA mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita,Joseph Musukuma amesema Chama cha mapinduzi mkoani humo kitafanikiwa kuzirejesha nafasi mbalimbali zilizotwaliwa na vyama vya upinzani iwapo atachaguliwa kushika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho.
 
Msukuma aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya kuchukua fomu ya kugombea nafasi ya uenyekiti wa CCM mkoa mpya wa geita ambapo alidai anakusudia kurejesha imani ya chama hicho kwa wananchi kutokana na baadhi yao kukisusia baada ya viongozi waliokuwepo awali kutokuwa na mvuto kwa wananchi.
 
Alisema CCM ni chama chenye maono mazuri kwa ajili ya kuwasaidia wananchi lakini baadhi ya viongozi wachache wamekuwa wakikivuruga chama hicho kutokana na kutaka kujipatia maslahi binafsi kinyume cha sheria huku wananchi waliowengi wakizidi kutaabika na ugumu wa maisha. 
 
Msukuma ambaye pia ni diwani wa Kata ya Nzera(CCM),alisema ameamua kuchukuwa fomu kuwania nafasi hiyo baada ya kuona wagombea wenzake wanaowania nafasi hiyo hawana sifa za kuongoza nafasi hiyo nyeti ndani ya chama cha mapinduzi.

Kufuatia hali hiyo alidai kushawishika kuomba nafasi hiyo mhimu ili kurejesha mshikamano na kukijenga chama hicho kwa kile alichodai kimepoteza sifa kutokana na baadhi ya viongozi kufanya kazi kwa mazoea na si kuwaletea maendeleo wananchi wa kipato cha chini hali ambayo imesababisha watu kukichukia na kukihama kila kukicha kwa kukimbilia kwenye vyama vingine vya upinzani.

“Nimelazimika kuchukua fomu ya uenyekiti Mkoa wa Geita baada ya kugundua wote walioomba nafasi hiyo wameshindwa kukiongoza maana wengi wao ni wale waliokuwa viongozi wa chama chetu ndani ya Wilaya na badala ya kukipeleka kwenye msitari kwa sasa kinaenda mlama hiyo ndiyo sababu kubwa ya mimi kuamua kuomba nafasi hiyo ili nikirudishe chama chetu kwenye msitari”
 
 
Kwa mjibu wa Katibu wa CCM mkoa wa geita Francis Elias tayari vigogo watatu ndani ya chama hicho akiwemo Musukuma wamechukuwa fomu za kuwania nafasi hiyo ambapo wengine  ni pamoja na Daud Ntinonu aliyewahi kuwa mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Geita,na nafasi yake kuchukuliwa na mwenyekiti wa sasa John Chenge Luhemeja ambaye naye anawania kiti hicho.
 
 
Musukuma aliondolewa kwenye nafasi ya uenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Geita na madiwani wenzake mapema mwaka jana baada ya kutuhumiwa kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutangaza hadharani majina ya mafisadi wa halmashauri ya geita na kuahidi kuwaburuza mahakamani pasipo kibari cha madiwani wenzake.



                                              NGELEJA AUMBULIWA NA MADIWANI SENGEREMA
                                                Mbunge wa Jimbo la Sengerema William Ngeleja.

Na Daniel Limbe,Sengerema
 
BAADHI ya madiwani wa sengerema mkoani mwanza wamemuumbua aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja baada ya kubainika kutojua taratibu na kanuni za uendeshwaji wa mabaraza ya halmashauri hiyo kutokana na kutohudhuria vikao tangu alipochanguliwa kuwa mbunge wa jimbo la sengerema.
 
Hatua hiyo ilikuja baada ya Ngeleja kuchangia hoja kwenye kikao cha baraza la madiwani akiwa amekaa chini, kitendo kilichopelekea diwani wa kata ya Nyehunge Benjamini Msheleja[Chadema]kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo Methew Lubongeja kusimamia sheria,taratibu na kanuni zinazoelekeza kila mjumbe anapochangia hoja lazima asimame isipo kuwa mwenyekiti pekee.
 
“Mheshimiwa mwenyekiti taarifa yangu inalenga kutaka meza yako iheshimiwe…aliyemaliza kuchangia hoja hivi sasa (Ngeleja) lazima atambue kuwa nayeye ni diwani mwenzetu,hivyo anapohitaji kuzungumza kwenye kikao hiki ni mhimu asimame badala ya kukaa…tunatambua mwenye mamlaka hayo ni wewe peke yako”alisema Msheleja huku akishangiliwa na madiwani wenzake.
 
Diwani huyo alitoa hoja hiyo muda mfupi baada ya mbunge huyo kumaliza kuchangia taarifa ya diwani wa kata ya Busisi (CCM) Joseph Njiwapori kuhusu uhaba wa chakula unaoikabili kata hiyo ambapo alisema kutokana na mazao yaliyolimwa katika msimu uliopita kukauka wakazi wa kata hiyo wanahitaji tani 1877 za mahindi ili kujikwamua balaa la njaa.
 
Ngeleja wakati akichangia taarifa hiyo huku akiwa amekaa alionyesha kusikitishwa na kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Juma Mwanjombe kutokuwa na takwimu sahihi za kaya zinazokabiliwa na uhaba wa chakula kwa wilaya nzima,ambapo mwenyekiti alizitaja baadhi ya kata zinazokabiliwa na tatizo kuwa ni Kalebezo,Busisi,Nyakasungwa,Buyagu na Igalula.
 
Wakizungumza na gazeti hili nje ya ukumbi wa baraza hilo,baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo walidai hatua ya Ngeleja kutojua taratibu na kanuni za uendeshwaji wa vikao, zinatokana na kutohudhuria vikao hivyo tangu alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la sengerema mwaka 2005na kwamba amekuwa akielewa zaidi kanuni za Bunge la Jamhuri ya muungano badala ya zile za vikao vya halmashauri.
 
Mbali na kupongeza matumizi mazuri ya fedha za mfuko wa jimbo katika kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wa sengerema madiwani hao wamesema wilaya hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na malipo ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji ambao wameanza kususia kuhamasisha shughuli za maendeleo kutokana na kutolipwa stahiki zao kwa kipindi kirefu.
 
Vilevile wamedaiwa kuonyesha mgomo baridi kushiriki katika kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kuanza kufanyika agosti 26 nchini kote kutokana na kile walichosema ni vugumu kuwapa ushirikiano wa dhati makarani wa sensa ambao wamelipwa kwa kazi hiyo huku wenyeviti hao wakiwa hawana malipo ya aina yoyote katika zoezi hilo .



                         Baadhi ya wananchi wakiwa pamoja na wakimbiza mwenge kitaifa  mkoani geita

Na Daniel Limbe,Geita
MBIO za mwenge wa uhuru wilayani geita mkoani hapa zimeingia dosari mara mbili baada ya mkuu wa wilaya hiyo Manzie Mangochie kukabidhi risala ya utii ya wilaya ya nyang'hwale badala ya geita sanjari na kuupoteza msafara wa mwenge na kusababisha baadhi ya miradi iliyotarajiwa kukaguliwa na kiongozi wa mbio hizo kitaifa Kapten Honest Mwanossa kupitilizwa.

Dosari ya kwanza ilijitokeza jana majira ya saa 10:21 jioni hatua iliyosababisha msafara huo kusimama kwa muda wa dakika 10 katika kijiji cha Ngula kata ya Nyakagwe hatua iliyomkera kiongozi wa mbio hizo kitaifa na kutoa kalipio kali kwa mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.

Msafara huo ulipitiliza mradi wa kikundi cha kuweka na kukopa cha Nyamalimbe ambacho kilitarajia kukaguliwa na kiongozi wa mbio hizo kabla ya kuondoka saa 11:00 mchana kwenda kukagua shamba la mihogo katika kijiji cha Ngula.

Mbio hizo zilisimama baada ya kukimbizwa umbali wa kilometa tatu kutoka kwenye eneo husika la mradi huo kitendo  ambacho kilimuweka kwenye wakati mgumu mkuu huyo wa wilaya baada ya kuhojiwa na kiongozi wa mbio za mwenge kuhusiana na tukio hilo la kushidwa kuongoza vyema msafara huo.

Kapteni Mwanossa aliamua kuusimamisha msafara huo baada ya kupitiliza kundi kubwa la wananchi waliokuwa wamejiandaa kuupokea mwenge wa uhuru wakiwa wamejipanga barabarani huku wakiimba nyimbo mbalimbali za mapokezi.

Kitendo hicho kilionekana kumsikitisha baada ya kuona anapitiliza mamia ya wananchi hao waliokuwa wakionekana kuhamasika zaidi,hali iliyomfanya kushindwa kutoa hotuba kwenye uzinduzi wa shamba bora la mbegu za mhogo na kumwelekeza msaidizi wake Kadia Godfrey kutoa hotuba katika mradi huo.

“Kilichoniumiza zaidi mimi ni ule wingi wa wananchi waliokuwa wamefurika pale wakitusubiri,nilidhani kuna sehemu tunakwenda kisha tunarudi kwa wale wananchi kumbe tumewaacha?!,unajua huu ndio mwanzo wa wananchi kuichukia serikali….’’ Alisikika akilalamika Kiongozi huyo wa mbio za mwenge.

Katika dosari ya pili mkuu huyo wa wilaya  alijikuta akimkabidhi katibu tawala wa Geita Moses Minga risala ya utii ya wilaya kwa rais  wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete risala ya wilaya ya Nyag’hwale badala ya risala ya wilaya ya Geita.

Wakati akisoma risala hiyo, Minga alijikuta akisimama kwa muda kusoma risala hiyo baada ya kubaini kuwa aliyokuwa akiisoma ilikuwa taarifa ya wilaya jirani na sio ya Geita ambapo alilazimika kueleza bayana kwamba taarifa hiyo ilikuwa ya Nyang’hwale wakati huo mwenge wa uhuru ukiwa tayari umeanza kupewa heshima.

‘’Mkuu wa wilaya hii taarifa ni ya Nyag’hwale sio ya Geita,iko wapi yenyewe ?’’alihoji Minga,hatua ilipelekea mkuu wa wilaya kupaza sauti mbele ya umati wa wananchi waliofurika kushuhudia tukio hilo kumwita dereva wake kupeleka taarifa hiyo kwa katibu tawala ili isomwe kwa mgeni rasmi kwa niaba ya rais Jakaya Kikwete.

‘’Peter yuko wapi?!....Peter lete risala imo kwenye gari’’alisikika Mangochie akipaza sauti,kitendo ambacho kilidumu kwa muda wa dakika 15 kupatikana kwa risala hiyo baada ya ofisa mmoja wa usalama wa Taifa kuokoa sakata hilo ambalo lilionekana kumkera pia kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11:45 jioni muda mfupi baada ya mbio za mwenge wa uhuru kufika katika kijiji cha Nyakagwe kwenye eneo la mkesha ambapo pamoja na mambo mengine kiongozi  huyo alifungua miradi ya sekta ya Afya,kituo cha polisi kilichojengwa kwa nguvu za wananchi na halmashauri kutokana na mradi wa uchimbaji madini wa serikali ya kijiji hicho.

Aidha akihutubia wananchi wa wilaya ya Geita wakati wa mbio hizo za mwenge  kapteni Mwanosya aliwataka watendaji wa serikali kusimamia matumizi ya fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Kauli hiyo aliitoa wakati alipozindua ujenzi wa ofisi ya kata ya Nyanguku unaotarajia kukamilika kwa gharama ya sh.75 miilion zinazotokana na michango ya wananchi na halmashauri ya wilaya ya Geita,ambapo alisema baadhi ya watendaji wamekuwa wakihujumu fedha za miradi na kusababisha miradi kukamilika chini ya kiwango.