Saturday, September 1, 2012




                                              NGELEJA AUMBULIWA NA MADIWANI SENGEREMA
                                                Mbunge wa Jimbo la Sengerema William Ngeleja.

Na Daniel Limbe,Sengerema
 
BAADHI ya madiwani wa sengerema mkoani mwanza wamemuumbua aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja baada ya kubainika kutojua taratibu na kanuni za uendeshwaji wa mabaraza ya halmashauri hiyo kutokana na kutohudhuria vikao tangu alipochanguliwa kuwa mbunge wa jimbo la sengerema.
 
Hatua hiyo ilikuja baada ya Ngeleja kuchangia hoja kwenye kikao cha baraza la madiwani akiwa amekaa chini, kitendo kilichopelekea diwani wa kata ya Nyehunge Benjamini Msheleja[Chadema]kutoa taarifa kwa mwenyekiti wa halmashauri hiyo Methew Lubongeja kusimamia sheria,taratibu na kanuni zinazoelekeza kila mjumbe anapochangia hoja lazima asimame isipo kuwa mwenyekiti pekee.
 
“Mheshimiwa mwenyekiti taarifa yangu inalenga kutaka meza yako iheshimiwe…aliyemaliza kuchangia hoja hivi sasa (Ngeleja) lazima atambue kuwa nayeye ni diwani mwenzetu,hivyo anapohitaji kuzungumza kwenye kikao hiki ni mhimu asimame badala ya kukaa…tunatambua mwenye mamlaka hayo ni wewe peke yako”alisema Msheleja huku akishangiliwa na madiwani wenzake.
 
Diwani huyo alitoa hoja hiyo muda mfupi baada ya mbunge huyo kumaliza kuchangia taarifa ya diwani wa kata ya Busisi (CCM) Joseph Njiwapori kuhusu uhaba wa chakula unaoikabili kata hiyo ambapo alisema kutokana na mazao yaliyolimwa katika msimu uliopita kukauka wakazi wa kata hiyo wanahitaji tani 1877 za mahindi ili kujikwamua balaa la njaa.
 
Ngeleja wakati akichangia taarifa hiyo huku akiwa amekaa alionyesha kusikitishwa na kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo Juma Mwanjombe kutokuwa na takwimu sahihi za kaya zinazokabiliwa na uhaba wa chakula kwa wilaya nzima,ambapo mwenyekiti alizitaja baadhi ya kata zinazokabiliwa na tatizo kuwa ni Kalebezo,Busisi,Nyakasungwa,Buyagu na Igalula.
 
Wakizungumza na gazeti hili nje ya ukumbi wa baraza hilo,baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo walidai hatua ya Ngeleja kutojua taratibu na kanuni za uendeshwaji wa vikao, zinatokana na kutohudhuria vikao hivyo tangu alipochaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la sengerema mwaka 2005na kwamba amekuwa akielewa zaidi kanuni za Bunge la Jamhuri ya muungano badala ya zile za vikao vya halmashauri.
 
Mbali na kupongeza matumizi mazuri ya fedha za mfuko wa jimbo katika kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wa sengerema madiwani hao wamesema wilaya hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na malipo ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji ambao wameanza kususia kuhamasisha shughuli za maendeleo kutokana na kutolipwa stahiki zao kwa kipindi kirefu.
 
Vilevile wamedaiwa kuonyesha mgomo baridi kushiriki katika kuwa zoezi la sensa ya watu na makazi linalotarajiwa kuanza kufanyika agosti 26 nchini kote kutokana na kile walichosema ni vugumu kuwapa ushirikiano wa dhati makarani wa sensa ambao wamelipwa kwa kazi hiyo huku wenyeviti hao wakiwa hawana malipo ya aina yoyote katika zoezi hilo .

No comments:

Post a Comment