Baadhi ya wananchi wakiwa pamoja na wakimbiza mwenge kitaifa mkoani geita
Na Daniel Limbe,Geita
MBIO za mwenge wa uhuru wilayani geita mkoani hapa zimeingia dosari mara mbili baada ya mkuu wa wilaya hiyo Manzie Mangochie kukabidhi risala ya utii ya wilaya ya nyang'hwale badala ya geita sanjari na kuupoteza msafara wa mwenge na kusababisha baadhi ya miradi iliyotarajiwa kukaguliwa na kiongozi wa mbio hizo kitaifa Kapten Honest Mwanossa kupitilizwa.
Dosari ya kwanza ilijitokeza jana majira ya saa 10:21 jioni hatua iliyosababisha msafara huo kusimama kwa muda wa dakika 10 katika kijiji cha Ngula kata ya Nyakagwe hatua iliyomkera kiongozi wa mbio hizo kitaifa na kutoa kalipio kali kwa mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
Msafara huo ulipitiliza mradi wa kikundi cha kuweka na kukopa cha Nyamalimbe ambacho kilitarajia kukaguliwa na kiongozi wa mbio hizo kabla ya kuondoka saa 11:00 mchana kwenda kukagua shamba la mihogo katika kijiji cha Ngula.
Mbio hizo zilisimama baada ya kukimbizwa umbali wa kilometa tatu kutoka kwenye eneo husika la mradi huo kitendo ambacho kilimuweka kwenye wakati mgumu mkuu huyo wa wilaya baada ya kuhojiwa na kiongozi wa mbio za mwenge kuhusiana na tukio hilo la kushidwa kuongoza vyema msafara huo.
Kapteni Mwanossa aliamua kuusimamisha msafara huo baada ya kupitiliza kundi kubwa la wananchi waliokuwa wamejiandaa kuupokea mwenge wa uhuru wakiwa wamejipanga barabarani huku wakiimba nyimbo mbalimbali za mapokezi.
Kitendo hicho kilionekana kumsikitisha baada ya kuona anapitiliza mamia ya wananchi hao waliokuwa wakionekana kuhamasika zaidi,hali iliyomfanya kushindwa kutoa hotuba kwenye uzinduzi wa shamba bora la mbegu za mhogo na kumwelekeza msaidizi wake Kadia Godfrey kutoa hotuba katika mradi huo.
“Kilichoniumiza zaidi mimi ni ule wingi wa wananchi waliokuwa wamefurika pale wakitusubiri,nilidhani kuna sehemu tunakwenda kisha tunarudi kwa wale wananchi kumbe tumewaacha?!,unajua huu ndio mwanzo wa wananchi kuichukia serikali….’’ Alisikika akilalamika Kiongozi huyo wa mbio za mwenge.
Katika dosari ya pili mkuu huyo wa wilaya alijikuta akimkabidhi katibu tawala wa Geita Moses Minga risala ya utii ya wilaya kwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete risala ya wilaya ya Nyag’hwale badala ya risala ya wilaya ya Geita.
Wakati akisoma risala hiyo, Minga alijikuta akisimama kwa muda kusoma risala hiyo baada ya kubaini kuwa aliyokuwa akiisoma ilikuwa taarifa ya wilaya jirani na sio ya Geita ambapo alilazimika kueleza bayana kwamba taarifa hiyo ilikuwa ya Nyang’hwale wakati huo mwenge wa uhuru ukiwa tayari umeanza kupewa heshima.
‘’Mkuu wa wilaya hii taarifa ni ya Nyag’hwale sio ya Geita,iko wapi yenyewe ?’’alihoji Minga,hatua ilipelekea mkuu wa wilaya kupaza sauti mbele ya umati wa wananchi waliofurika kushuhudia tukio hilo kumwita dereva wake kupeleka taarifa hiyo kwa katibu tawala ili isomwe kwa mgeni rasmi kwa niaba ya rais Jakaya Kikwete.
‘’Peter yuko wapi?!....Peter lete risala imo kwenye gari’’alisikika Mangochie akipaza sauti,kitendo ambacho kilidumu kwa muda wa dakika 15 kupatikana kwa risala hiyo baada ya ofisa mmoja wa usalama wa Taifa kuokoa sakata hilo ambalo lilionekana kumkera pia kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru.
Tukio hilo lilitokea majira ya saa 11:45 jioni muda mfupi baada ya mbio za mwenge wa uhuru kufika katika kijiji cha Nyakagwe kwenye eneo la mkesha ambapo pamoja na mambo mengine kiongozi huyo alifungua miradi ya sekta ya Afya,kituo cha polisi kilichojengwa kwa nguvu za wananchi na halmashauri kutokana na mradi wa uchimbaji madini wa serikali ya kijiji hicho.
Aidha akihutubia wananchi wa wilaya ya Geita wakati wa mbio hizo za mwenge kapteni Mwanosya aliwataka watendaji wa serikali kusimamia matumizi ya fedha za serikali zinazotolewa kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kauli hiyo aliitoa wakati alipozindua ujenzi wa ofisi ya kata ya Nyanguku unaotarajia kukamilika kwa gharama ya sh.75 miilion zinazotokana na michango ya wananchi na halmashauri ya wilaya ya Geita,ambapo alisema baadhi ya watendaji wamekuwa wakihujumu fedha za miradi na kusababisha miradi kukamilika chini ya kiwango.
No comments:
Post a Comment