Monday, August 13, 2012


             ASKARI WA KISIWA CHA RUBONDO WATUHUMIWA KWA MAUAJI YA WATU 9

                                                      Hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo.

Na Daniel Limbe,Geita.
CHAMA cha wananchi CUF wilayani geita mkoani hapa kimelaani vikali mauaji ya watu 9 yanayosadikiwa kufanywa na askari wa hifadhi ya kisiwa cha Rubondo katika ziwa Victoria baada ya kuwafyatulia risasi za moto na wengine kuwatosa majini kutokana na kuwatuhumu kujihusisha na uvuvi haramu,huku serikali ya wilaya hiyo ikidaiwa kufumbia macho vitendo hivyo.
 
Kwa mujibu wa taarifa ya maandishi iliyotolewa kwa waandishi wa habari leo na Katibu wa chama cha CUF wilayani geita Seveline Malugu,Matukio hayo yalitokea kwa nyakati tofauti mwishoni mwa mwaka 2011 hadi 2012 ndani ya ziwa Victoria baada ya askari hao kuwakamata baadhi ya wananchi kwenye maeneo jirani na mpaka wa hifadhi ya kisiwa hicho kisha kuwaua na wengine kuwabambikizia kesi mahakamani kinyume cha sheria.
 
Baadhi ya watu waliodaiwa kufa kwa risasi na wengine kutoswa ndani ya maji ya kina kirefu ni Paschal Mabwete,Selemani Tembo,Jeremiah Mussa,Abel Zacharia,na mtu mmoja aliyejulikana kwa jina moja la Kulwa.
 
Wengine ni Idd Mussa,Shija Shigondo,Baluhya Buzinza na Marco Masanyiwa ambapo katika tukio hilo wawili waliokoka na kifo baada ya kufanikiwa kuogelea hadi nchi kavu  wote walikuwa wavuvi wa mtu aliyefahamika kwa jina la Burhan mkazi wa kisiwa cha Ikuza wilaya ya Muleba mkoani kagera.
 
Katika taarifa ya Chama hicho imekituhumu kitengo cha doria kinachoongozwa na Ofisa doria mkuu Chuwa J. kwa madai kimekuwa kikiboresha mwahusiano mazuri na baadhi ya wawindaji haramu kisha kuingia ndani ya hifadhi hiyo na kuuwa wanyama kinyume cha sheria kwa lengo la kujinufaisha kwa maslahi binafsi.
 
Imeelezwa kuwa hali hiyo ilipekelekea tembo mmoja kuuawa na wawindaji haramu ambapo idara hiyo ililazimika kutumia gharama kubwa kununua mafuta ya kutosha na kuiteketeza kwa lengo la kupoteza ushahidi kwa viongozi wa ngazi za juu.
 
Akizungumza na gazeti hili mjini geita mmoja wa wananchi waliofanyiwa ukatili wa kutisha na askari wa kisiwa hicho Yusuf Nasibu (46) amesema April 26 mwaka huu alipokea taarifa kwa njia ya simu kuwa rafiki zake wamekamatwa na askari wa kisiwa hicho na kwamba ili kuwaachilia walitakiwa kutoa kiasi cha shilingi 100,000 kama faini ya kuvua samaki eneo la hifadhi.
 
Baada ya kuwasiliana na mwajiri wa wavuvi hao waliamua kuchukua boti na kiasi cha fedha zilizohitajika ili kuwalipia faini wavuvi hao,lakini katika hali isiyokuwa ya kawaida baada ya mwajiri huyo(Jina limehifadhiwa) kutoa kiasi cha pesa zote alizokuwa nazo 600,000 mfukoni ili kulipa shilingi 100,000 il;iyohitajika,askari hao walimwamuru kutoa fedha zote pasipo kurudisha mfukoni kiasi kilichosalia.
 
Nasibu amesema baada ya kupokonywa fedha hizo yeye alihoji sababu ya kuchukua fedha kinyume cha makubaliano,hali iliyosababisha kupelekwa kwenye kambi moja yapo ya ndani ya hifadhi hiyo na kuanza kushambuliwa kwa vipigo vikali kisha kubambikizwa kesi ya kuingia ndani ya hifadhi pasipo kibari cha serikali,kukutwa na nyavu haramu na kutuhumiwa kutoa rushwa ili askari hao wasifanye kazi.
 
Kufuatia hali hiyo Chama hicho kimemwandikia walaka Mkuu wa wilaya ya Geita Omary Manzie kuelezea Ukatili wa kinyama unaofanywa na askari wa kisiwa cha Rubondo na kumtaka kutoa ufafanuzi juu ya mauaji hayo badala ya serikali kukaa kimya na kuyafumbia macho huku wahusiano ya wananchi na askari hao yakizidi kutoweka kila kunapo kucha.
 
Aidha mbali na chama hicho kumwandikia barua mkuu wa wilaya pia,kimemtaka kuunda tume huru kuchunguza vitendo hivyo badala ya kusubiri kupewa taarifa na viongozi wa hifadhi hiyo ambao wanadaiwa wamekuwa wakipotosha maelezo kwa kuhofia kuwajibishwa iwapo itafahamika wazi unyama wanaoutenda.
 
Alipotafutwa kwa njia ya simu ili kuzungumzia tuhuma dhidi yake Ofisa doria wa kisiwa hicho Chuwa alidai yupo safarini na kwamba hawezi kulitolea maelezo swala hilo na kumtaka mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na mhifadhi mkuu wa kisiwa cha Rubondo kwa namba 0782643402 ambaye hata hivyo baada ya kutafutwa kwa simu hakuweza kupatikana.
 
Kadhalika baada ya jitihada za mwandishi wa habari hizi kugonga mwamba alilazimika kumtafuta kwa njia ya simu mkuu wa wilaya ya geita Omary Manzie ambaye pia simu yake ya mkononi haikupatikana mbali na kumtafuta mara kwa mara.
 

No comments:

Post a Comment