CUF CHAMLIPUA DC GEITA
ADAIWA KUONGOZA KIBABE
AWATIMUA WANANCHI OFISINI KWAKE
Mkuu wa mkoa wa Geita Said Magalula
Na Daniel
Limbe,Geita
CHAMA cha wananchi CUF
wilayani geita mkoani hapa kimemshitaki mkuu wa wilaya hiyo Omary Manzie kwa
mkuu wa mkoa wa huo Said Magalula kwa madai ya kutawala kibabe,kushindwa kutatua
kero za wananchi na kuwabagua wananchi wake kwa itkadi za vyama vyao kinyume cha
sheria.
Hatua hiyo imetokana na
malalamiko mbalimbali ya wananchi ambayo yamekuwa yakiwasilishwa kwake kwa ajili
ya kuyapatia ufumbuzi lakini baadhi yao huwatimua ofisini mwake kwa madai hana
nafasi ya kusikiliza majungu.
Katibu wa Chama cha
wananchi CUF wilayani geita Sevelin Malugu ameliambia NIPASHE kuwa Mkuu wa
wilaya hiyo aliteuliwa na rais Jakaya Kikwete hivi karibuni kwaajili ya
kuwatumika wananchi wa wilaya ya geita lakini hali hiyo imekuwa kinyume na
matarajio ya wengi kwa kuwa amekuwa limbukeni wa madaraka,hali inayosababisha
watu kuhoji sifa za kuteuliwa kwake.
“Mimi namuona DC wangu huyo
ni limbukeni wa madaraka… kama nafasi aliyonayo anakuwa hivyo,je angepewa ukuu
wa mkoa ingelikuwaje..ama angelikuwa kwenye cheo cha mheshimiwa Kikwete si
angeliweza kutemea mate watu”alihoji Malugu.
Kutokana na hali hiyo
Katibu huyo amemwandikia walaka wa maandishi mkuu wa mkoa huo (Magalula )
kuingilia kati mgogoro wa ardhi dhidi ya wananchi wa kijiji cha Nyantorontoro
“A” na baadhi ya viongozi Idara ya madini wilayani humo ambao wanadaiwa
kumilikisha ardhi ya wananchi kinyume cha sheria.
Katika taarifa ya Chama
hicho mwekezaji aliyemilikishwa ardhi hiyo kinyume cha sheria ni Majaliwa
Maziku, ambaye anadaiwa kufanya mazungumzo na viongozi wa idara hiyo kisha
kumpatia eneo hilo licha ya wananchi wa maeneo hayo kudai hawajaripwa fidia ya
ardhi yao .
Awali eneo hilo lilikuwa
likimilikiwa na wananchi na baadaye mwaka 2004 ardhi hiyo ilichukuliwa na
kampuni ya kichina ya Sino Hidro Company Limited, iliyokuwa
ikitengeneza barabara kwa kiwango cha lami kutoka wilayani Geita hadi
Buzirayombo wilayani Chato kwa makubaliano ya kuitumia ardhi hiyo kwa kipindi
cha miaka mitatu ya mradi huo kisha ingelejea mikononi mwa wananchi
hao.
Katika mradi huo wananchi
hao walitakiwa kuhama maeneo hayo ili kuepuka kupata madhara yatokanayo na
shughuli za ulipuaji baruti na vumbi kubwa linalotokana na usagaji wa kokoto
kwenye “Crasher” ambapo wananchi hao walilipwa fedha kidogo kwa makubaliano ya
miaka mitatu huku wengine wakikosa hata kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo baada ya mradi
huo kuanza kutekelezwa baadhi ya wananchi walijitokeza na kupeleka malalamiko
yao kwa mtendaji wa kjiji cha Nyankumbu kudai kulipwa fidia ya mazao na nyumba
zao zilizoharibiwa baada ya milipuko iliyotokea septemba 8 mwaka 2006 kutokana
na maeneo yao kutokuwa kwenye orodha ya watu waliolipwa awali.
Hatua hiyo ilipelekea
mtendaji wa kijiji hicho kumwandikia barua mkuu wa wilaya hiyo Septemba 11 mwaka
2006 ikimuarifu Malalamiko ya kuharibiwa mazao kutokana na milipuko inayotokana
na wachina wanaotengeneza barabara ya Geita hadi Buzirayombo,na baadaye Ofisi ya
mkuu wa wilaya kuandika barua yenye Kumb. Namba.R. 40/1/VOL.V/147 ya novemba 8
mwaka 2006 kwenda kwa Meneja wa Tanroads Mkoa wa mwanza juu ya uwepo wa
malalamiko hayo.
Aidha baada ya mradi huo kukamilika mwaka
2007 wananchi walilejea kwenye maeneo yao ya awali na kuendesha maisha yao ya
kila siku lakini katika hali ya kushangaza hivi karibuni walipewa taarifa
kupitia ofisi ya madini wilayani humo kuwa maeneo hayo yamemilikishwa kwa
mwekezaji na kutakiwa kuondoka kwa kuwa tayari walishalipwa fidia ya ardhi zao
na kampuni ya Kichina iliyokuwa ikitengeneza barabara.
Alipotakiwa kuzungumzia
malalamiko hayo Ofisa madini wa kanda ya ziwa Juma Kharuna alikiri eneo hilo
kugawiwa kwa mwekezaji na kudai kuwa taratibu zote za kisheria zimezingatiwa kwa
kuwa eneo hilo lilikaa wazi kwa muda mrefu mpaka hapo alipojitokeza mwekezaji
huyo.
Kadhalika Kharuna alimtaka
mwandishi wa habari hizi kufanya mawasiliano na Mtendaji wa kata ya Kalangalala
Hamad Juma ili kuzungumzia suala hilo kwa kina kutokana na kuufahamu vizuri
mgogoro huo wa wananchi dhidi ya serikali.
Hata hivyo baada ya
mwandishi wa habari hizi kumtafuta kwa njia ya simu mtendaji huyo alikanusha
kuwa taarifa sahihi na badala yake kumuomba mwandishi wa habari kumtafuta mkuu
wa wilaya kwa kuwa mgogoro huo ulishafika ofisini kwake.
No comments:
Post a Comment