Saturday, September 1, 2012




                                MBIO ZA MWENGE WA UHURU ZAENDELA KUINGIA DOSARI GEITA
                                BENDERA YA TAIFA YAZUA TAFRANI CHATO.
Na Daniel Limbe,Geita
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida mbio za Mwenge wa uhuru juzi ziliendelea kuingia dosari katika Mkoa mpya wa geita baada ya Waandishi wa habari pamoja na Madereva waliokuwa kwenye msafara wa mbio za Mwenge katika Wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita, kujikuta katika wakati Mgumu baada ya kuzuiwa kula chakula na Ofisa usalama wa Taifa wa Wilaya hiyo Sunday Steven.
Tukio hilo liliwakera madereva waliokuwa wakiendesha magari kwenye msafara huo na kulazimika kuingia kwenye mgomo,kabla ya mgomo huo kunusuriwa na kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa mwaka huu Kapteni Honest Mwanossa.
Baada ya kumaliza kula chakula katika chumba maalum katika shule ya msingi Lugunga kiongozi wa mbio za mwenge alitoka nje na kuwafuata madereva hao waliokuwa wamejikusanya katika kundi moja wakijadili kugoma kuendesha magari hayo na kuwaomba kwenda kula chakula katika chumba hicho.
Haikufahamika mara moja mtu aliyempa taarifa kiongozi huyo wa mbio za mwenge kwamba madereva hao walikuwa wamenyimwa chakula na kwamba walikuwa katika harakati za kugomea safari,ambapo katika hali isiyokuwa ya kawaida alipomaliza kunawa alikwenda moja kwa moja na kuwafuata madereva hao mahali walipokuwa na kuwaelekeza mahali pa kula chakula.
Vilevile Mwanossa aliendelea na zoezi la kuwasaka madereva wengine ambao walionekana hawako katika mazingira hayo ambapo alikuwa akimsaka mmoja baada ya mwingine na kumpeleka kwenye chumba cha chakula,na baada ya hapo safari ikaanza,hata hivyo alionekana kukerwa na hali hiyo.
Madereva hao zaidi ya 11 walikumbana na mkasa huo kwa kile kilichoelezwa  na ofisa ulasama huyo wa wilaya kwamba chakula hicho kilikuwa kimeandaliwa kwa ajili ya viongozi wa mbio za mwenge wa uhuru kitaifa,Mkoa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 8:26 mchana katika kijiji na kata ya Lugunga  wakati madereva hao  wakiwa kwenye foleni ili kupata chakula na baadaye kuendelea na msafara hadi katika shule ya sekondari Masumbwe kuzindua klabu ya kupambana na rushwa.
Walipokumbana na mkasa huo kutoka kwa ofisa usalama wa taifa walienda kujadili kuhusu suala hilo umbali wa mita 100 kutoka kwenye moja vyumba vya madarasa lililokuwa likitumika kama chumba cha kupatia chakula cha mchana katika shule ya msingi Lugunga.
Katika majadiliano hayo madereva walikubaliana kususia kuendelea na msafara wa mbio za mwenge wa uhuru kwa kuwa hawakuwa katika orodha ya wageni waliotakiwa kupata chakula hicho,kitendo ambacho kiliwafanya baadhi yao kukaa mbali na magari yao.
Pia mkasa kama huo uliwakumba waandishi wa habari sita waliokuwa wameambatana na msafara huo kutoka mkoani na wilayani humo baada ya ofisa usalama huyo kuwazuia kupata chakula cha asubuhi kilichokuwa kimeandaliwa katika ya sekondari Isangijo kata ya ushirika ambapo kiongozi wa mbio hizo aliweka jiwe la msingi kwenye chumba cha maabara.
Ofisa huyo alitumia kauli ya kwamba wanaotakiwa kupata chakula walikuwa wageni wa kitaifa na kimkoa licha ya miongoni mwa wanahabari hao kutoka mkoani ambao walikuwa wameambata na mbio za mwenge tangu ulipoingia katika mkoa wa Geita agosti 26,mwaka huu.
Mkuu wa wilaya hiyo Husna Mwilima ambaye naye alionekana kukerwa na kitendo cha Ofisa usalama huyo,alizungumza baadaye na waandishi wa habari na kuwaomba radhi kwa yote yaliyojitokeza,na kuwataka kuendela na zeozi hilo la kukimbiza mwenge katika wilaya hiyo.
"Jamani Ndugu kila binadamu ana mapungufu yake,naomba mumsamehe alikua hajui alitendalo,namuombea msamaha wa dhati kabisa,jamani wilaya yangu ni Mpya,na naweza kuwathibitishia kwamba wilaya mama (Bukombe) imenitenga sana katika zoezi hili nimhangaika sana na huyu ofisa usalama yanwekena amechanganyikiwa....'' alisisitiza mkuu huyo wa wilaya.
Hatua hiyo ilikuja siku moja baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuripoti habari za mkuu wa wilaya ya Geita Omary Mangochie  kupoteza mbio za mwenge wa uhuru baada ya kupitiliza mradi  mmoja uliotarajiwa kukaguliwa na kiongozi wa mbio hizo Kapten Mwanosa katika kijiji cha Nyamalimbe.
Tukio hili lilitokea baada ya kiongozi huyo kupitiliza umati mkubwa wa watu waliokuwa wamepanga foleni barabarani kusubiri kuupokea mwenge huo ili kukagua na kutoa mkopo  kwenye kikundi cha mikopo na akiba cha kijiji hicho.
Baada ya mbio hizo kukimbia umabli wa kilomita 3,kiongozi huyo alipoipitia ratiba ya mkoa aligundua kupitilizwa mradi huo huku mkuu wa wilaya akiwa amekaa kimya kitendo kilichoonekana kumkera na la kulazimika kuusimamisha msafara na kuhoji kabla ya kuamua kuendelea na msafara huo.
Mbali na hilo Mwanossa alionekana kukerwa na mapokezi ya mwenge huo katika wilaya ya chato baada ya kuufikisha mwenge wa uhuru kwenye uwanja wa mkesha na kukuta hakuna maandalizi ya kutosha ikiwa ni pamoja na kutokuwepo Bendera ya taifa.
“Huu ni mwenge wa uhuru ambao tunaukimbiza kitaifa…nasikitika kufika hapa kwenye mkesha wa mwenge huu lakini sijaona bendera ya taifa ikipepea mahari hapa”alisema
Kutokana na kauli hiyo baadhi ya viongozi wa wilaya hiyo ambao hawakujulikana majina yao haraka walilazimika kuwaagiza baadhi ya vijana ambao wapo kwenye mafunzo mgambo wilayani humo kwenda kung’oa bendera iliyokuwa imesimikwa kwenye ofisi za kata ya chato na kuikimbiza haraka kwenye uwanja wa mkesha wa mwenge huo.
Awali akikagua baadhi ya miradi ya maendeleo kwenye wilaya hiyo Mwanossa alidai miradi mingi aliyojionea aslimia kubwa imejengwa chini ya kiwango licha ya kuwa pesa nyingi za serikali zikionekana kutumika katika miradi hiyo.
                                                                                 Mwisho.

No comments:

Post a Comment