WALIMU TISA WAISHI KWENYE NYUMBA MOJA SENGEREMA.
Mkuu wa wilaya ya sengerema Bi Karen Yunus.(Picha kwa hisani ya Blog)
Na Daniel Limbe,Sengerema.
KATIKA hali inayochochea misongo ya
mawazo, walimu tisa wamejikuta wakiishi katika vyumba vitatu vya nyumba
moja kutokana na uhaba wa nyumba.
Kufuatia hali hiyo, Baraza la Madiwani la Sengerema mkoani Mwanza
limemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwatafutia nyumba mara
moja walimu walimu hao.
Walimu wanaodaiwa kuishi kwenye nyumba moja yenye vyumba vitatu ni wa
Shule ya Msingi Soswa wilayani hapa mkoani Mwanza baada ya kuripoti eneo
la kazi na kukuta uhaba mkubwa wa nyumba za walimu.
Hatua hiyo imekuja baada ya Diwani wa Kata ya Bulyaheke, Bageti Ngele
kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye kata
yake ambapo alisema licha ya kuwepo mafanikio makubwa ya miradi, kata
hiyo inakabiliwa na ukosefu wa nyumba za walimu kwenye baadhi ya shule
za msingi na sekondari, akitoa mfano wa walimu tisa wa shule ya msingi
Soswa kuishi kwenye nyumba moja.
Ngele alidai hatua hiyo imekuwa ikiwaathiri walimu hao kisaikolojia na
kuwa vigumu kupunguza tamaa ya mwili itokanayo na tendo la ndoa licha ya
mwalimu mkuu wa shule hiyo kuishi yeye na familia yake ndani ya nyumba
hiyo ambayo hata hivyo haina dari.
Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Mathew Lubongeja
alimwagiza Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Juma Mwajombe
kuhakikisha walimu hao wanaondolewa kwenye nyumba hiyo haraka wakati
serikali ikijipanga kuondoa tatizo hilo.
“Kutokana na unyeti wa suala hili…mkurugenzi ninakuagiza uhakikishe
walimu hao wanaondoka haraka kwenye nyumba hiyo ili ibaki idadi
inayokubalika kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha walimu hao
kuathirika kisaikolojia…hii ni hatari sana,”alisema Lubongeja.
Aidha alisema jitihada za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa ili
kuhakikisha shule hiyo inaongezewa majengo ya nyumba za walimu haraka
kwa kutumia fedha za serikali badala ya kuendelea kusubiri michango ya
wananchi katika kutekeleza miradi hiyo.
Kaimu mkurugenzi huyo aliahidi kulishughulikia haraka suala hilo kwa
kuzingatia taratibu na kanuni za utumishi wa Umma ili kuondoa adha
inayowakabili walimu hao.
Alisema hatua hiyo inaweza kuathiri kiwango cha utoaji elimu kwa wanafunzi kutokana na walimu hao kuishi kwa misongo ya mawazo.
No comments:
Post a Comment