Na Daniel
Limbe,Sengerema
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida diwani wa kata ya Kasenyi wilayani
sengerema mkoani mwanza Sindano Sanyiwa amegeuka omba omba baada ya watu
wanaosadikiwa vibaka kumpora nguo,simu ya mkononi na fedha zote alizokuwa
nazo.
Sakata hilo limemkumba jana
majira ya saa 8 usiku akiwa amelala kwenye chumba namba 105 kwenye nyumba ya
kulala wageni ya Nyakaduha Motel iliyopo nje kidogo ya mji wa sengerema wakati
akihudhulia vikao vya baraza lahalmashauri hiyo.
Hatua ya diwani huyo kugeuka ombaomba imekuja baada ya mwenyekiti
wa halmashauri hiyo Methew Lubongeja kumpa nafasi ya kuuliza swali kwenye kikao
cha baraza la madiwani,ambapo diwani huyo kabla ya kuuliza swali aliomba
kulijulisha baraza hilo kuwa ameibiwa nguo zake,simu ya mkononi na fedha
zilizokuwa kwenye mfuko wa suluali yake.
Kutokana na hali hiyo aliwaomba madiwani wenzake kufanya harambee
ili kumsaidia kupata kiasi cha fedha zitakazomwezesha kuendelea kumudu gharama
za maisha wakati akiendelea na vikao vya baraza hilo hatua iliyopelekea madiwani
hao kubwaga vicheko vingi kabla ya mwenyekiti wao kuwatuliza.
“Mheshimiwa mwenyekiti kwanza kabisa napenda kulijulisha baraza
lako tukufu kuwa usiku wa kuamkia leo nikiwa nimelala kwenye chumba changu kuna
watu wanaohisiwa kuwa ni vibaka walikata nyavu za dirisha la chumba hicho kisha
kuniibia nguo zangu,simu ya mkononi na pesa taslimu nilizokuwa nazo,hivyo
ninaomba madiwani wenzangu mnichangie changie kiasi chochote ili nami niendelee
kushiriki na ninyi kwenye vikao vyetu”alisema Diwani huyo.
Hata hivyo mwenyekiti wa baraza hilo alifanikiwa kutuliza vicheko
vilivyoambatana na makofi ndani ya ukumbi huo na kuwataka madiwani
kumpa pole mwenzao kwa tukio hilo kwa kuwa linaweza kumtokea mtu yeyote pasipo
kujali ni kiongozi.
Baada ya hatua hiyo diwani huyo aliendeliendelea na swali lake la
msingi juu ya ujenzi wa barabara ya Kafundile kwenda kasenyi Rugongo yenye urefu
wa kilomita 17 na daraja la Shitwego linaloungaisha vijiji vya Kasenyi na
Rugongo ambalo limekatika na kuwafanya wakulima wa maeneo hayo kushindwa
kusafirisha mazao yao kwenda kwenye soko kuu la mjini sengerema.
Vilevile alidai kuwa kutokana na hali hiyo baadhi ya wakulima,mama
wajawazito na wazee wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kwaajili ya
kufika kwenye soko kuu,hospitali ya wilaya na huduma zingine mhimu za kibinadamu
zinazopatikana mjini sengerema.
Alidai kuwa licha ya barabara na daraja hilo kutangazwa na
halmashauri hiyo kwaajili ya kumpata mkandarasi hakuna hatua zozote
zilizoonekana kuchukuliwa ili kunusuru maisha ya wananchi wa kata ya Kasenyi
ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia hali hiyo.
Kufuatia madai ya diwani huyo
kuporwa mali zake NIPASHE limelazimika kufika kwenye Motel hiyo ili kupata
ufafanuzi wa tukio hilo ambapo mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo Meneja wa
Motel hiyo Tindos Pangani amesema hatua hiyo imetokana na uzembe wa diwani huyo
kwa kile alichodai alifungua dirisha na kuliacha wazi wakati akitaka kulala
usiku.
“Tukio hilo lipo limetokea majira ya saa 8 usiku,lakini
ninachoweza kusema ni kuwa diwani mwenyewe ndiye mzembe kwa maana wakati amelala
alifungua dirisha na kuliacha wazi baadaya kuona kuna joto kali ndani huku akiwa
kafungulia feni, hali iliyosababisha vibaka kupata njia rahisi ya kujipatia
fedha”alisema Pangani.
Pangani amesema tukio hilo limetokea kwa mara ya pili tangu kufunguliwa kwa Motel hiyo takribani miaka 3 iliyopita na kwamba mazungumzo ya upotevu huo dhidi
ya mteja wao yamefanyika na kupata suruhu.
No comments:
Post a Comment