Na Daniel Limbe,Sengerema
KATIKA hali
isiyokuwa ya kawaida,walimu wawili wa shule ya msingi Igaka wilayani Sengerema
mkoani mwanza wametwangana makonde ndani ya ofisi ya shule baada ya kurushiana
maneno makali kutokana na mwalimu mkuu msaidizi kumtuhumu mwenzake kwa uwajibikaji
mbovu.
Akizungumza na
NIPASHE mwalimu mkuu wa shule hiyo Boniphace Shilunga amesema tukio hilo
limetokea juzi oktoba 19 mwaka huu majira ya saa 8 mchana baada ya mwalimu
Lazimani Manyabele kusukumiana makonde na mwalimu mkuu msaidizi Edson
Kagusa.
Hatua hiyo ilitokana
na majibizano ya maneno kati ya walimu hao wawili baada ya mwalimu mkuu msaidizi
kumtuhumu mwenzake kuwa ni amekuwa akivunja sheria za kwa makusudi kutokana na
kuchelewa kufika shuleni na kushindwa kuhudhuria kwenye vipindi kama
alivyopangiwa.
Amesema baada ya
kurushiana maneno ndani ya ofisi hiyo mwalimu Manyabele alinyanyuka mahari
alipokuwa ameketi na kumkwida mwalimu mwenzake baada ya kumwita kuwa msaliti
hatua iliyosababisha kumrushia konde lililopelekea majibizano ya ngumi hizo
kabla ya walimu wengine kuingilia na kuwaachanisha.
Amedai kuwa mbali na sheria za nchi
zinazowataka watumishi kuwahi kazini na kutimiza wajibu wao,shule hiyo tayari
ilikuwa imejiwekea utaratibu wa walimu wote kufika shuleni kabla ya saa 2
asubuhi sanjari na kuhudhuria kwenye vipindi vyote vya masomo ikilinganishwa na
ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wakifika shuleni saa 4 asubuhi na kuondoka
pasipo utaratibu unaotakiwa.
Mratibu elimu kata
ya Buzilasoga Robert Cheyo amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa tayari
amekwisha andaa taarifa ya maandishi kwenda kwa ofisa elimu wa wilaya hiyo ili
hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya walimu hao kwa madai kupigana maeneo ya
shule ni kuidhalilisha shule na taaluma ya ualimu.
Amesema kamwe
serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo kwa kuwa ni utovu wa nidhamu kazini
na uzalilishaji wa taaluma ya ualimu kwa kuwa wao wanatakiwa kuwa kioo kwa jamii
wanayoiongoza.
Kaimu mkurugenzi wa
halmashauri ya wilaya ya sengerema Juma Mwanjombe aliupoulizwa na mwandishi wa
habari hizi kuhusiana na tukio hilo alidai kuwa tayari ofisi yake imekwisha
pokea taarifa ya sakata hilo huku akiahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria
walimu hao ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kama hiyo.
Mwanjombe alifafanua
kuwa walimu hao wamevunja sheria namba 56 ya mwaka 2003 ambayo inawataka walimu
kuwa na mahusiano bora kazini na kwamba inabainisha wazi kuwa atakaye vunja
sheria hiyo adhabu yake ni kupewa onyo kali,kutelemshwa daraja la kazi,au
kufukuzwa kazi.
Aidha ametoa wito
kwa walimu wote wilayani humo kutii sheria na kuheshimiana kwa kuwa ndiyo silaha
ya mahusiano kazini na kwamba serikali haitamwonea aibu mwalimu yoyote atakaye
endelea kuvunja sheria zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba.
No comments:
Post a Comment