Saturday, July 21, 2012

                     MAJAMBAZI YATEKA KIJIJI,YAPORA FEDHA NA SIMU



                                        Kamanda wa Polisi mkoa wa Gita Leonard Paul

Na Daniel Limbe,Chato
WATU wanaosadikiwa majambazi waliokuwa na silaha za kivita,mapanga na malungu wameteka kijiji cha Kibehe kata ya kigongo wilayani chato mkoani geita na kufanikiwa kupora fedha,simu za mkononi na kujeruhi baadhi ya wananchi. 


Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa 6;30 usiku baada ya majambazi hao kuteka kaya zaidi ya tano kabla ya kurusha risasi kadhaa hewani hatua iliyosababisha wananchi kushindwa kutoka ndani ya nyumba zao.

Wakizungumza na NIPASHE baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo Mussa Limbe na Inocent Moshi wamesema majambazi hao baada ya kuanza uvamizi huo uliodumu kwa zaidi ya saa 2 walimteka na kumweka chini ya ulinzi mwalimu wa shule ya msingi Kibehe Nyalusule Kungula na kumuamuru kuwatembeza kwenye kaya za watu wenye fedha.

Baada ya uvamizi huo,majambazi hao walitumia silaha za jadi(Mapanga na Malungu) kuwajeruhi baadhi ya wananchi kwa lengo la kuwashinikiza kutoa fedha na simu za mkononi hatua iliyopelekea kujeruhiwa vibaya katika maeneo mbalimbali ya miili yao.

"Baada ya kuvamia majambazi hayo yalianza kuwapiga kwa kutumia malungu na mapanga huku yakiwashinikiza kutoa fedha zote walizo nazo na baada ya kuchukua fedha na simu yalianza kufyatua risasi hewani ili kuwatishia wananchi"alisema Moshi.

Aidha wamedai kuwa majambazi hao wanaokadiliwa kufikia idadi ya 11 walianza kupiga yowe wakati wakiondoka na wananchi walipojitokeza kwa lengo la kusaidia kunakotokea yowe walikutana na majambazi hao na kuwashambulia kwa mapanga hatua iliyopelekea baadhi ya wananchi kujeruhiwa vibaya.

Wamewataja baadhi ya waliojeruhiwa vibaya kuwa ni pamoja na Paschal Magoma,Mwalimu wa shule ya msingi Bukamila Edwin Mponela na Mtu mmoja ambaye hajafahamika jina lake lakini anadaiwa kuwa fundi wa pikipiki katika kijiji hicho ambao wote wamelazwa kwenye hospitali ya wilaya ya chato kwaajili ya matibabu.

Kamanda wa polisi mkoani geita Leonard Paul amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi la polisi linaendelea kuwasaka watu wote wanaodaiwa kuhusika na kwamba watakapo bainika watafikishwa mahakamani.

Aidha Paul amewataka wananchi kujenga tabia ya kutoa taarifa mapema kwa jeshi la polisi pindi wanapowahisi baadhi ya watu wasiowafahamu ili iwe rahisi kwa jeshi hilo kukabiliana na matukio kama hayo kabla ya kutokea uvunjifu wa amani.

Kamanda huyo amedai kuwa mbali na polisi kuwahi kwenye eneo la tukio hakuna mtu aliyekamwatwa kuhusika na uvamizi huo.

No comments:

Post a Comment