Wednesday, June 6, 2012


                              MWALIMU AFARIKI  KWA KULIPUKIWA KIBATARI

                             Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufunzdi Dk Shukuru Kawambwa
Na Daniel Limbe,Chato
WALIMU watatu wa Shule za msingi wilayani Chato mkoani Geita wamefariki dunia katika matukio tofauti,likiwemo la mmoja wao kulipukiwa na moto wa kibatari wakati akiweka mafuta ambayo yanasadikiwa kuwa na mchanganyiko petroli.
 
Akizungumza na NIPASHE jana Ofisa elimu wa shule za msingi wilayani Chato Ishengoma Kyaruzi alisema katika tukio la kwanza lilimhusisha mwalimu wa shule ya msingi Chabulongo Asma Mudongwa (26) ambaye alifariki dunia jana katika hospitali ya wilaya hiyo baada ya kulipukiwa na moto uliosababishwa na mafuta yanayosadikiwa kuwa na mchanganyiko wa Petrol wakati akiweka kwenye taa ya kibatari.
 
Kyaruzi alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 3.30 usiku wakati marehemu akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Chabulongo kata ya katende wilayani chato,ambapo inadaiwa alichukua chupa ya mafuta na kuanza kumimina kwenye taa hiyo na kitambo kidogo kibatari hicho kililipuka hali iliyosababisha moto kutapakaa na kumuunguza kwenye paji la uso hadi kwenye utosi wa kichwa baada ya ngua zake kushika moto.
 
Hatua hiyo ilipelekea Mume wa marehemu huyo ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Chabulongo Khabibu Nuru kutoa taarifa kwenye uongozi wa halmashauri hiyo na kulazimika kukimbiza gari katika eneo la tukio lakini wakati akiendelea kupata matibabu katika hospitali ya wilaya ya chato mauti yalimkuta mnamo saa 7 mchana.
 
Kyaruzi aliongeza kuwa taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kwenda nyumbani kwao wilayani Mkuranga Mkoani Pwani zinafanyika ambapo kutokana na mazungumzo ya pande mbili kati ya mume na mke wamekualiana mazishi kufanyika mkoani humo na kwamba marehemu ameacha mtoto mmoja wa miezi 9.
 
Katika tukio la pili alisema lilimhusisha mwalimu wa shule ya msingi Nyamirembe Getruda Batenda (54) ambaye alifariki mei 24 katika kijiji cha Nyamirembe wilayani hapa kutokana na kinachosadikiwa kunywa pombe aina ya gongo hali iliyopelekea sukari kushuka na kusababisha mauti yake.
 
Alisema baada ya taratibu za mazishi kukamilika marehemu alizikwa kwenye mashamba yake yaliyopo kijijijini hapo,Huku tukio la tatu likimhusisha mwalimu wa shule ya msingi Kakanshe Kalilo Mukama (25) ambaye alifariki mei 26 mwaka huu baada ya kuugua ugonjwa wa Malaria na kupelekea kifo chake na kwamba mwili wa marehemu utasafirishwa kupelekwa nyumbani kwao katika kijiji cha Mwibara wilayani Bunda mkoani Mara.
 
Katibu wa Chama cha walimu (CWT) wilayani hapa Victoria Baseka amekiri kutokea kwa vifo hivyo na kudai kuwa hatua hiyo ni pigo kubwa kwa walimu na wananfunzi ambao walitegemea kuendelea kupata taaluma kutoka kwa walimu hao ambao wamepoteza maisha kwa kipindi cha mwezi mmoja.
 
Aidha Baseka aliwataka walimu na wanafunzi wote katika wilaya ya chato kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu na kuamini kuwa kifo ni mpango wa mwenyezi mungu na kwamba hakuna haja ya kukimbilia kwa waganga wa jadi kutafuta mchawi hali inayoweza kuleta uvunjifu wa amani katika jamii.
 
Jeshi la polisi wilayani hapa limekiri kuwepo kwa matukio hayo na kwamba hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na matukio hayo.

No comments:

Post a Comment