Wednesday, June 6, 2012


                             .CHADEMA,CUF WAWAVAA VIONGOZI WA SERIKALI GEITA


 Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Geita Magalula Said Magalula

Na Daniel Limbe,Geita
SIKU Chache baada ya kutokea mauaji ya mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Kivukoni ambaye alipigwa risasi na mlinzi wa mgodi wa GGM uliopo wilayani hapa,Vyama vya Chadema na CUF vimetoa siku saba kwa mkurugenzi wa halmashauri,mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa wa geita Said Magalula kuhakikisha wanatatua tatizo la mauaji ya wananchi ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara.
 
Diwani wa kata ya Kalangalala wilayani Geita Peter Donard kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema),amesema chama hicho mkoani Geita,kimewapa siku saba kuanzia juni 1,mwaka huu kuhakikisha mauaji ya wananchi hayatokei.
 
Kwa mujibu wa walaka wa barua uliotumwa juni mosi na diwani huyo kwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri ya geita Tatala Mpangalukela,Mkuu wa wilaya hiyo Magwenchie na mkuu wa mkoa wa geita Said Magalula ukiwataka kumaliza tatizo hilo ndani ya siku saba na kama matukio ya mauaji yatazidi kujitokeza chama hicho kitahamasisha maandamano ya amani ya kupinga mauaji hayo.
 
Alisema kamwe haiwezekani wananchi wafananishwe na chawa ambao huuawa kila wakati huku akiwatupia lawama viongozi husika kwa madai wanaonekana kuwakumbatia wauaji hao na kulinda maslahi ya wawekezaji.
 
Akiwahutubia wananchi wa kata ya Kasamwa juzi diwani huyo alisema kumeibuka wimbi la walinzi wa mgodi huo kujichukulia sheria mkononi ya kuwapiga na kuwauwa kwa risasi wananchi wanaoonekana katika mgodi huo na baadhi ya wananchi kupata ulemavu wa kudumu hatua ambayo imejenga mahusiano mabaya kati ya wananchi wa Geita na uongozi wa mgodi huo.
 
‘’Ndani ya siku saba kama kutatokea mauaji tena huko mgodini…walai nitahamasisha maandamano ya amani…viongozi hawa nimewapa hizo siku saba,kuhakikisha..wanalitolea ufafanuzi tatizo hilo,wananchi sio chawa wa kila wakati wanauawa’’alisema diwani huyo.
 
Mbali na kupinga mauaji hayo pia.diwani huyo alisema amepinga utaratibu uliotumika katika suala la uuzaji wa viwanja vya serikali ambavyo vinauzwa kinyume na taratibu kwa wananchi kwa gharama kubwa,ambapo kiwanja kidogo kinauzwa kwa sh.600,000 hadi 3,000,000 tofauti na bei ya iliyozoeleka ya kila kiwanja kuuzwa sh.560,000 kiwanja kidogo,cha kati sh.800,000 na kiwanja kikubwa ambacho huuzwa sh.1,000,000.
 
Alisema utaratibu huo umefanyika bila kuwashirikisha madiwani wa halmashauri hiyo ambao ndiyo wenye maamuzi ya mwisho ya utekelezaji na mipango ya maendeleo na kwamba kamati ya ugawaji wa viwanja ya mji huo haikutoa ushirikiano katika kupanga bei hiyo hatua ambayo amedai kama haitadhibiwa na viongozi hao wananchi watakosa imani na serikali yao.
 
Aidha kwa upande wake katibu wa chadema mkoa wa Mwanza,Wilison Mshumbusi alisema chama hicho hakiwezi kuvumilia wananchi kuendelea kunyanyasika katika nchi yao kwa kukumbatia wawekezaji na kuwageuza wazalendo kuwa wanyama wa kuuwa kila kukicha na hivyo kuwataka wananchi kukiunga mkono chama hicho katika kupigania haki zao.
 
Alisema serikali mkoani Geita inatakiwa kujipanga kutatua mvutano uliopo kati ya wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo na uongozi wa mgodi ili kumaliza mauaji na maandamano ya kila wakati yanayogharimu maisha ya wananchi.
 
Kwa upande wake katibu wa chama cha CUF wilayani geita Seveline Malugu ameliambia gazeti hili kuwa chama chake kinaungana na Chadema katika kukemea mauaji hayo ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara lakini serikali ikionekana kuyafumbia macho matukio hayo.
 
"katika hili sisi kama CUF tuna laani kwa nguvu zote vitendo hivi kwa kuwa vinatokea na serikali ya wilaya na mkoa vikiwepo lakini hakuna hatua zozote za masingi ambazo zimechukuliwa ili kukomesha kuendelea kwa mauaji ya wananchi wetu...hii ni nchi yetu sote tunatakiwa tuishi kwa amani na utulivu...kitendo cha kuendekeza maslahi ya mwekezaji kuliko uzalendo wa nchi haina maana kabisa"alisema malugu.
 
Aidha alibainisha kuwa Chama hicho kinatarajia kufanya maandamano ya amani kuishin ikiza serikali kudhibiti vitendo vya mauaji ya wananchi ikiwemo kuiomba kuwatimua kazi baadhi ya viongozi wa serikali ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kuendekeza maslahi yao binafsi kutokana kwa mwekezaji huyo GGM na kushindwa kulinda maslahi ya jamii,
 
 
Kauli za viongozi hao zimekuja siku chache baada ya mwanafunzi wa darasa la sita Hoja Juma wa shule ya msingi Kivukoni kufa na mwingine kujeruhiwa vibaya kwa kile kilichosadikika kupigwa risasi na walinzi wa mgodi huo wakati akiokota vyuma chakavu kwenye mgodi huo kwa lengo la kwenda kuviuza kupata fedha ya kununulia sare za shule.
 
Tukio hilo lililotokea alhamisi iliyopita lilisababisha wananchi zaidi ya 600 wa Mwatulole anakoishi mwanafunzi huyo,siku iliyofuata kuandamana hadi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Geita kupinga mauaji hayo ambayo yametokea mwezi mmoja baada ya kutokea maandamano yaliyopelekea gari la mgodi huo kuteketezwa kwa moto na wananchi.

No comments:

Post a Comment