WAZIRI AONYA UKARIMU KWA WAHAMIAJI HARAMU
Na Daniel Limbe,Bukoba
WAZIRI wa maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Mathayo David Mathayo ameonya vikali ukarimu wa watanzania wakiwemo viongozi wa serikali kuwakaribisha wahamiaji haramu wenye makundi makubwa ya mifugo kutoka nje ya nchi kinyume cha sheria,huku akitishia kuwafukuza kazi baadhi ya viongozi wa idara yake ambao watabainika kuwakumbatia wahamiaji hao kutokana na maslahi binafsi.
Wahamiaji hao wanadaiwa kutoka nchi za Uganda , Rwanda na Burundi ambao huingia nchini kinyume cha sheria kupitia njia za panya huku wakiwa na makundi makubwa ya mifugo nakwamba hupewa maeneo ya kuishi na baadhi ya viongozi wa serikali walioko katika mipaka ya nchi kutokana na makubaliano haramu.
Waziri amebainisha hayo jana mjini Bukoba muda mchache baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Wizara yake mkoani kagera kwenye Ofisi ya mkuu wa mkoa huo Fabian Masawe ambapo alisema serikali kamwe haitakubali kuona wananchi wake wanaendelea kuteseka ndani ya nchi yao kutokana na ukatili wanaotendewa na wahamiaji haramu kutoka nchi za Rwanda,Uganda na Burundi kwa kuwa kitendo hicho ni aibu kwa taifa.
Aidha alishangazwa na taarifa ya mkoa huo iliyoeleza wazi kuwepo kwa baadhi ya viongozi wa serikali za vijiji vilivyoko mipakani kutokuwa raia wa Tanzania na kwamba walichaguliwa kwa nguvu ya fedha kutoka kwa wahamiaji haramu wa nje yanchi kwa lengo la kuwahifadhi wahamiaji hao pamoja na mifugo yao.
“Kamwe serikali haitakubali kuendelea kusikia unyanyasaji mkubwa wa wananchi wake wanaofanyiwa na wahamiaji haramu wenye mifugo iliyoingia nchini kwetu kinyume cha sheria kutokana na maslahi ya viongozi wachache wasio raia waliochaguliwa kwa nguvu ya fedha ili kulinda maslahi ya wahamiaji haramu” alisema Waziri Mathayo.
Viongozi hao wamedaiwa kuwa mawakala wa kuwakaribisha wenzao kutoka nje ya nchi pindi wanapokuwa wamepata madaraka kisha kuwapa maeneo ya kufanyia kazi zao nchini, hali inayopelekea uvunjifu wa amani nchini.
“Nchi hii inaongozwa kwa sheria taratibu na kanuni..ninasema kiongozi yeyote katika idara yangu atakayebainika kushirikiana na wahamiaji hao haramu kuingiza,kuhifadhi au kutoa msaada wowote kwa nia ya kuingia nchini tutamtimua kazi mara moja”.
Awali katika taarifa ya mkoa wa kagera,iliyosomwa kwa niaba ya mkuu wa mkoa huo Fabian Masawe,Dk Paulin Msafili alisema mkoa huo unawahamiaji haramu 35,000 ambao wameweka makazi ndani ya misitu wakijihusisha na ufugaji mifugo,Upasuaji mbao na kuchoma mkaa kinyume cha sheria.
Na kwamba zaidi ya ng’ombe 200,000 zimo ndani ya misitu ya hifadhi kinyume cha sheria huku baadhi ya viongozi wa serikali wakiendelea kuwakumbatia kutokana na maslahi binafsi.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment