.WALIMU GEITA WAKESHA OFISI YA MKURUGENZI WAKISHINIKIZA KULIPWA MADAI YAO
. WADAI WAPO TAYARI KUFA KWA KUDAI HAKI YAO
. DED ASUSIA KIKAO BAADA YA HOJA ZAKE KUPINGWA VIKALI
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa.
Na Daniel Limbe,Geita
Na Daniel Limbe,Geita
KATIKA hali inayoonekana kuiumiza kichwa serikali kutokana na migomo na maandamano ya watumishi kila kukicha, hali hiyo imezua tafrani wilayani Geita mkoani hapa baada ya walimu wapya zaidi ya 60 wa shule za sekondari kuandamana hadi ofisi za mkurugenzi wa halmashauri hiyo Mpangalukera Tatala wakidai kulipwa stahiki zao ambazo wamedai kupigwa danadana kila uchwao.
Hatua hiyo iliwalazimu siku ya jana kukesha usiku na mchana mbele ya ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri hiyo huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kuiusia serikali kuacha kuwanyanyasa kutokana na madai yao huku shughuli mbalimbali za kiofisi zikiwa zimesimama kwa muda usiojulikana kutokana na kuhofia usalama wa watumishi.
Baadhi ya nyimbo walizokuwa wakiimnba ni pamoja na ule wa “kama siyo juhudi zako nyerere uongozi wangepata wapi!!...na ule wa tunataka haki zetu..”
Kufuatia hali hiyo Mkurugenzi wa halmashauri hiyo na ofisa elimu sekondari wa Wilayani hiyo walilazimika kukutana na walimu hao kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo ili kuzungumza nao na juhudi hizo kugonga mwamba baada ya walimu hao kupinga kila alichokuwa akizungumza mkurugenzi huyo ambaye alichukia na kuwaacha ukumbini.
Ofisa elimu ya sekondari wilayani Geita, George Opiyo, alilieleza gazeti hili kuwa walimu hao walivamia eneo hilo tangu machi 4 mwaka huu majira ya asubuhi, wakiimba nyimbo mbalimbali za mapambio ambapo mbali na uongozi wa halmashauri hiyo kukutana nao kuwaeleza hali halisi bado walimu hao wamegoma kurudi kwenye vituo vyao vya kazi hadi hapo watakapolipwa madai yao .
Opiyo alisema walimu hao wanadai mishahara yao ya mwezi mmoja tangu waanze kazi Februari mwaka huu, fedha za kujikimu za siku 7,walimu wa shahada siku 3 na stashahada 4 na nauli ya kusafirisha mizigo yao kwenda vituo vya kazi,na kwamba wanadai jumla ya Tsh. Mil 40,037,100 za awamu ya pili baada ya pesa za awamu ya kwanza Tsh. 30,150,000 kati ya Tsh. Mil 70,187,100 walizokuwa wanadai walikwishawalipa.
Kwa upande wake katibu wa Chama cha Walimu Wilayani Geita Samwel Hewa mbali na kukutana na walimu hao leo,amelaani vikali unyanyasaji huo na kuiomba serikali iwarudishe nyumbani walimu hao hadi hapo itakapopata fedha za kuwalipa na siyo kuwatesa kama inavyofanya sasa hali iliyopelekea walimu hao kulala bila kula nje ya ofisi za halmashauri hiyo kama wanyama.
No comments:
Post a Comment