Monday, March 12, 2012


                                   MADIWANI CHADEMA WAMLIPUA MAGUFULI



                                         Waziri wa Ujenzi John Magufuli

Na Daniel Limbe,Chato
MADIWANI wa halmashauri ya chato mkoani kagera kupitia tiketi ya Chadema wamemlipua mbunge wa jimbo la Chato ambaye pia ni Waziri wa Ujenzi John Magufuli kwa madai amekuwa akitoa lugha za uchochezi na kejeli kwenye mikutano yake ya hadhara pindi anapokuwa akizungumza na wananchi kwenye kata za madiwani wa upinzani.

Akitoa kauli hiyo leo (jana) kwenye kikao cha baraza hilo,diwani wa kata ya Muganza Marko Maduka amedai mbunge wa jimbo hilo amekuwa akitumia lugha chafu kwa wananchi, huku akitamka hadharani kuwa serikali haitopeleka maendeleo kwa wananchi hao kwa madai ya kuwachagua viongozi wa upinzani ndani ya jimbo lake.

Hatua hiyo imefuatia swali la papo kwa papo lililoulizwa na diwani wa kata ya Nyamirembe John Ibawa kwa mwenyekiti wa halmashauri ya Chato Charles Maisha ambaye alitaka kujua kanuni zinazowaruhusu madiwani wa upinzani kufanya mikutano ya hadhara kwenye kata za madiwani wa CCM na kuwachonganisha kwa wapiga kura wao.

Swali hilo lilionekana kuchafua hali ya hewa kwenye baraza hilo,baada ya kumtuhumu vikali diwani wa kata ya Buseresere Crespen Kagoma kwa madai amekuwa akilenga kuchochea vulugu kwa wananchi dhidi ya madiwani wa chama tawala.

Hatua hiyo ililazimu madiwani wa Chadema kumhusisha mbunge wa jimbo hilo kutokana na kauli zake chafu na kejeli kubwa kwa wananchi wanaoongozwa na madiwani wa upinzani, na kuwataka madiwani na viongozi wa CCM kumshauri mbunge huyo kuacha kutoa kauli za uchochezi kwenye kata zao ili kudumisha demokrasia katika wilaya hiyo.

“Mheshimiwa mwenyekiti mimi nachelea kuunga mkono kauli ya diwani mwenzangu wa CCM kwa madai madiwani wa chadema wamekuwa wakilenga kuchochea vurugu kwa wananchi wa kata za madiwani wa chama tawala...kauli za uchochezi mbona zimekuwa zikitolewa na mbunge wetu John Magufuli pindi anapokuwa kwenye kata zetu za upinzani?”alihoji diwani wa kata ya Ilyamchele Josephat Mayunga.

“Inasikitisha sana kuona madiwani wa CCM mmeshindwa kumshauri mbunge wa chama chenu…leo kauli za madiwani wa upinzani ndiyo mmeziona mbaya kuliko za Magufuli?..inashangaza kuona hajapata watu wa kumshauri”.

Akitoa mfano wa kauli za Magufuli alizozungumza na wananchi wa kata ya Muganza diwani wa kata hiyo alisema “akiwa kwangu Magufuli alisema kwa sababu ninyi mlijifanya kumchagua Chadema, Maduka kuwa diwani wenu basi kaeni namaduka wenu ili awafungulie maduka mengi..lakini ninawaahidi suala la umeme kufika Kasenda msitegemee hata kidogo”alisema

Kufuatia hali hiyo diwani viti maalumu kata ya Chato Brandina Mwarabu (CCM) aliwasihi madiwani wenzake kuacha kuogopa kusemwa na wapinzani badala yake amewataka pale wanaona wamezungumzwa hawana budi nao kuitisha mikutano na kuzungumza na wanachi ikiwezekana kukanusha kauli hizo badala ya hoja hizo kuzipeleka kwenye baraza la madiwani.

Jitihada za kumpata Mbunge wa jimbo la Chato Magufuli hazikuzaa matunda baada ya simu yake ya mkoni kutopatikana.

                                                        

No comments:

Post a Comment