. WAUNGA MKONO KAULI YA LOWASA TATIZO LA AJIRA NCHINI
WAZIRI WA KAZI AJIRA NA VIJANA MH,GAUDENSIA KABAKA
Na Daniel Limbe,Geita
SIKU chache baada ya serikali kupinga vikali kauli ya
aliyekuwa waziri mkuu aliyejihudhuru Edward Lowassa kuhusiana na tatizo la
ajira kwa vijana nchini,baadhi ya vijana wilayani hapa mkoa mpya wa geita
wamemshukia waziri wa Ajira kazi na vijana Gaudensia Kabaka huku wakiunga mkono
kauli ya Lowasa.
Lowasa amewahi kukaliliwa zaidi ya mara tatu akitoa angalizo
hilo kwa
serikali na kulifananisha na bomu linalotarajiwa kulipuka siku za usoni iwapo
hatua za haraka hazitachukuliwa kuhakikisha vijana wanapata ajira.
Kufuatia hali hiyo serikali kupitia waziri wake wa kazi
ajira na vijana alivunja ukimya na kupinga vikali kauli hiyo kwa madai kauli
hizo ni kutoitendea haki serikali kwa kuwa inaendelea kukabiliana na tatizo
hilo na kwamba imefanikiwa kupunguza tatizo la ajira kwa aslimia 1.2 kutoka
mwaka 2000/1 hadi kufikia mwaka 2006.
Wakizungumza katika kongamano la vijana kuhusiana na tatizo
la ajira hapa nchini lililofanyika kata ya kamena wilayani geita na kuhudhuliwa
na vijana zaidi ya 1200 wakiwemo wanafunzi wa shule ya sekondari Kamena na
Nyamalimbe,ambalo limefadhiliwa na shirika NELICO kupitia programu ya sauti ya
vijana wamesema tatizo la ajira kwa vijana ni kubwa na kwamba serikali
imeshindwa kutengeneza mazingira rafiki ya kuwasaidia kujiajiri.
Wamesema serikali inaowajibu mkubwa wa kuwasaidia vijna
kupata ajira rasmi na zisizo rasmi ili kupunguza ongezeko la umaskini hapa
nchini ikiwa ni pamoja na kufufua na kujenga viwanda vingi nchini,kutoa elimu
inayoweza kumfanya kijana kuwa na ujuzi na maarifa,kutoa mikopo kwa masharti
nafuu na kuwapatia pembejeo zenye ruzuku ya serikali badala ya kuendelea
kuwahimiza kusoma kwa lengo la kukusanya vyeti visivyo na tija.
“Tulisikitika sana kuona serikali ikipinga kauli ya lowasa
kuhusiana na tatizo la ajira kwa vijna lilivyo kubwa hapa nchini,ukweli hakuna
nchi inayoweza kuendelea pasipo kuwa na viwanda nchini kwake…ili kuondoa tatizo
hili kunahaja kubwa kwa serikali kuimalisha na kujenga viwanda,kutoa mikopo kwa
masharti nafuu,na kutupa vijana hasa tulioko vijijini pembejeo za kilimo tena
kwa wakati ili tusaidie kukuza uchumi wan chi badala ya kundelea kukusanya
vyeti”alisema Richard Poleni.
Na kwamba njia nyingine ya kusadidia kuondoa tatizo hilo ni
serikali kupunguza mishahara na posho za viongozi wa ngazi za juu ili kuiwezesha
kuwa na pesa za kuajili vijana wengi ambao humaliza elimu zao na kukosa kazi
hali inayosababisha baadhi yao kujiingiza kwenye vitendo vya ujambazi na
uporaji.
Kadhalika katiba ya nchi ibadilishwe na kutambua uwepo wa
ajira kwa vijana badala ya kuendelea na utaratibu ulivyo hivi sasa ambapo
vijana wamekuwa wakinyimwa kazi huku baadhi ya wazee wakiwa wameng’anga’nia
madarakani na wengine kutoa ajira kwa “undugu nazesheni” hali inayowanyima
vijana wengi haki ya kuajiriwa.
Kwa upande wake Alphonce Emmanuel ameitaka serikali kubadili
mfumo wa utoaji elimu kwa wananfunzi huku akisisitiza masomo ya stadi za kazi
na maisha vipewe kipaumbele ili kumwandaa kijana anapo hitimu elimu yake awe na
uwezo wa kujiajiri mwenyewe badala ya kuendelea kusubili kuajiliwa na serikali.
Amedai kuwa serikali haiwezi kukwepa tatizo la ajira kwa
vijana,ni vema ikatafuta mbinu sahihi ya kuondoa tatizo hilo badala ya kuendela kupinga uwepo wa
changamoto hiyo ilihali vijana wengi wakiwa mitaani hawana ajira.
Mratibu wa kitengo cha sauti ya vijana ambaye pia ni mwana
sheria wa asasi ya NELICO Benard Otieno amesema lengo la kongamano hilo limelenga kutoa wigo
wa kuhakikisha sauti za vijana zinasikika kwa viongozi na watunga sera
kuhusiana na mabo mbalimbali yanayowahusu kila kukicha.
Sababu nyingine ni kuwafanya vijana kutambua na kutoa ufumbuzi
wa matatizo yao
wenyewe kwa lengo la kutumia fulsa walizonazo kujiletea maendeleo na kupunguza
tatizo la ajira nchini ambalo limekuwa likiwatesa vijna wengi na kulazimika
kuitupia lawama serikali iliyopo madarakani.
Naye Mkuu wa idara ya saikolojia wa NELICO,Diana Renatus
ameliambia gazeti hili kuwa kutokana na tatizo la ajira kwa vijana hapa nchini
kuwa mwamba usiovunjika, shirika hilo limelazimika kuendela kutoa msaada wa
kuwawezesha vijana kupata elimu ya ujasiliamali ili kuboresha maisha yao na
kuinua uchumi wa taifa.
Awali akitoa
ufafanuzi wa tatizo hilo kwa vijana
waliohudhulia kongamano hilo
mmoja wa maofisa maendeleo ya jamii wilayani geita Emma Busanji aliwataka
vijana kuacha kubweteka na kungoja ajira za serikali,huku akiwahimiza kutumia
raslimali walizonazo kujiajiri wenyewe.
Amesema hali ilivyo hivi sasa ni tofauti na zamani kwa kuwa
awali kulikuwa na wasomi wachache na ajira zilikuwa nyingi ukilinganisha na
hali ilivyo hivi sasa ambapo teknolojia za kisayansi zimechangia kupunguza kwa
ajira kwa wananchi na kurahisisha kazi.