Friday, June 22, 2012

                                             AGIZO LA MKUU WA MKOA LAPUUZWA




                                            Mkuu wa mkoa wa Mwanza Mhandisi Evarist Ndikilo

Na Daniel Limbe,Geita
SIKU chache baada ya mkuu wa mkoa wa mwanza injinia Evarist Ndikilo kutoa siku saba kwa baadhi ya viongozi wa idara ya misitu wilayani geita mkoa wa mwanza kuchukuliwa sheria kali kutokana na tuhuma za ubadhilifu na utendaji kazi mbovu,agizo hilo limeonekana kugonga mwamba.

Katika agizo lake mkuu wa mkoa huo alimtaka mkurugenzi wa halmashauri ya geita Mpangalukera Tatala kuhakikisha watendaji waliochini ya ofisi yake (Misitu) ambao wamebainika na tuhuma za kuhujumu raslimali za nchi kutokana na maslahi yao binafsi wanachukuliwa sheria kali pasipo kujali nyadhifa walizonazo.

Agizo hilo alilitoa hivi karibuni kwenye kikao cha wakuu wa idara wa halmashauri hiyo huku akiomba kupewa taarifa za utekelezaji wa agizo hilo kabla ya februali 29 ambapo uchunguzi wa gazeti hili umebaini agizo halijatekelezwa.

Waliotuhumiwa kuhusika na utendaji kazi mbovu wenye lengo la kujinufaisha kinyume cha sheria ni Charles Tui na Emmanuel Marekano ambao walidaiwa kujihusisha na shughuli za ukamataji wa mazao ya misitu polini kisha kuyauza kwa watu binafsi pasipo kuzingatia kanuni na taratibu za kiutumishi.

Ndikilo alidai uchunguzi alioufanya katika ziara yake wilayani humo ulibaini watumishi hao kufanya kazi kwa mazoea kinyume na maadili ya utumishi wa umma kitendo alichodai hakiwezi kufumbiwa macho na serikali.

“Ninasema kwa utendaji kazi wa namna hii kamwe serikali haiwezi kuwafumbia macho watendaji wenye kufanya kazi kwa mazoea kwa lengo la wao kujinufaisha huku wakijua wazi kufanya hivyo ni kosa kisheria”alisema Ndikilo

Hata hivyo gazeti hili liliazimika kumtafuta mkurugenzi wa halmashauri ya geita kwa lengo la kupata ufafanuzi wa agizo la mkuu wa mkoa alililolitoa hivi karibuni,ambapo jitihada hizo ziligonga mwamba baada ya simu zake za mkononui kutopatikana

Wednesday, June 6, 2012


                       .SERIKALI YAWAONYA WAUZAJI WA DAWA ZA BINADAMU



                                        Waziri wa Afya na Maendeleo ya Jamii Dk Haji Mponda

Na Daniel Limbe,Chato
SERIKALI kupitia mamlaka ya chakula na dawa nchini imeonya vikali vitendo vya baadhi ya wauzaji wa maduka ya dawa baridi za binadamu kuendesha shughuli za kitabibu kwenye maduka yao kinyume cha sheria na kwamba huduma hizo zinapaswa kutolewa kwenye Hospitali,vituo vya afya na zahanati zilizosajiriwa kisheria.
Kwa mujibu wa uchunguzi  uliofanywa na wizara ya afya  kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Management Sciences for Health (MSH) mwezi aprili hadi mei 2001 walibaini ukiukwaji mkubwa wa utoaji huduma kwenye maduka ya madawa nchini,hali ambayo ilikuwa ikihatarisha maisha ya wananchi kutokana na tamaa za fedha kwa wamiliki wa maduka hayo.
Baadhi ya mambo waliobaini katika uchunguzi huo ni pamoja na wauzaji kutokuwa na elimu ya utoaji tiba,kuuza dawa moto na zisizosajiriwa kisheria badala ya dawa baridi za binadamu,kutoa mimba,kudunga sindano,kufunga vidonda na kulaza wagonjwa.
“Baada ya serikali kupitia mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la MSH tulibaini ikiukwaji mkubwa wa uendeshwaji wa maduka ya dawa baridi kutokana na kuuza dawa wasizoruhusiwa kisheria na kutoa huduma za kitabibu kinyume na maadili,hatua aliyopelekea seriakali kubuni mpango mkakati wa kuwaelimisha wamiliki na wauzaji wa maduka hayo”alisema
Katika taarifa ya mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya chakula na dawa TFDA iliyotolewa na Dk Bundara Maganga  katika mafunzo maalumu ya wauzaji wa maduka ya madawa baridi ya binadamu ambayo yanatarajiwa kupandishwa hadhi na kuwa maduka muhimu ya dawa alisema mpango huo umeonyesha mafanikio makubwa zaidi hasa katika mkoa wa Ruvuma ambako utekelezaji wake ulianza tangu februali 2002.
Aidha alisema mpango huo umetekelezwa katika mikoa 15 ya Tanzania na kuonyesha mafanikio makubwa baada ya wauzaji hao kutambua sheria na kanuni za utoaji wa sahihi wa dawa,kuelewa mbinu za magonjwa yatokeayo mara kwa mara katika jamii,huduma kwa magonjwa ya watoto,stadi za mawasiliano na elimu ya ukimwi na ushauri nasaha.
Alizitaja mikoa zilizoinufaika mafunzo hayo kuwa ni Ruvuma,kigoma,Manyara Lindi,Mbeya,Shinyanga,Pwani ,Dododma,Mara,Iringa,Singida,Tanga,Mtwara,Morogoro na rukwa huku mikoa mingine sita ikiwemo Kagera ikiendelea kupatiwa mafunzo hayo kwa kuzingatia uwezo wa seriakali.
Alisema kutokana na mpango huo wa seriakali itakuwa ni marufuku kwa mmiliki yoyote wa duka la dawa muhimu kuajiri mtumishi asiye na sifa zinazotakiwa kisheria na kwamba hatua hiyo itasaidia kuinua maendeleo ya jamii kutokana na wananchi kupata huduma yenye uhakika wa afya zao.
Mganga mkuu wa wilaya ya chato mkoa mpya wa geita ambaye pia alikuwa mgeni rasmi katika mafunzo hayo Dk Athanas Ngambakubi alisema mafunzo hayo ya siku 35 yatawasaidia kuongeza uelewa na mbinu sahihi za utoaji huduma kwa wagonjwa wao ukilinganisha na awali.
Dk Ngambakubi alisema kuwa iwapo dawa zikitumiwa kwa usahihi huleta matunda yaliyokusudiwa na dakatari  pamoja na  jamii,lakini kinyume chake zikitumika isivyofaa hugeuka na kuwa sumu hivyo husababisha madhara makubwa ambayo hayakukusudiwa.
Aidha alidai hatua hiyo itawasaidia kupewa vyeti vinavyotambuliwa na serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii,hatua itakayowasaidia kuongeza soko la ajira yao sanjari na kukua kwa mishahara yao ukilinganisha ha ilivyo hivi sasa.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo Ayubu Daniel na Dk Pius Ngambakubi  wameipongeza serikali kwa uanzisha mpango huo utakao saidia kuongeza ajira kwa wahitimu hao na kulejesha heshima ya taaluma ya ufamasia hasa katika maeneo ya vijijini ambako huduma za kiserikali zimekuwa ngumu kuwafikia wananchi.

                             .CHADEMA,CUF WAWAVAA VIONGOZI WA SERIKALI GEITA


 Mkuu Mkuu wa Mkoa wa Geita Magalula Said Magalula

Na Daniel Limbe,Geita
SIKU Chache baada ya kutokea mauaji ya mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi Kivukoni ambaye alipigwa risasi na mlinzi wa mgodi wa GGM uliopo wilayani hapa,Vyama vya Chadema na CUF vimetoa siku saba kwa mkurugenzi wa halmashauri,mkuu wa wilaya na mkuu wa mkoa wa geita Said Magalula kuhakikisha wanatatua tatizo la mauaji ya wananchi ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara.
 
Diwani wa kata ya Kalangalala wilayani Geita Peter Donard kupitia chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema),amesema chama hicho mkoani Geita,kimewapa siku saba kuanzia juni 1,mwaka huu kuhakikisha mauaji ya wananchi hayatokei.
 
Kwa mujibu wa walaka wa barua uliotumwa juni mosi na diwani huyo kwenda kwa mkurugenzi wa halmashauri ya geita Tatala Mpangalukela,Mkuu wa wilaya hiyo Magwenchie na mkuu wa mkoa wa geita Said Magalula ukiwataka kumaliza tatizo hilo ndani ya siku saba na kama matukio ya mauaji yatazidi kujitokeza chama hicho kitahamasisha maandamano ya amani ya kupinga mauaji hayo.
 
Alisema kamwe haiwezekani wananchi wafananishwe na chawa ambao huuawa kila wakati huku akiwatupia lawama viongozi husika kwa madai wanaonekana kuwakumbatia wauaji hao na kulinda maslahi ya wawekezaji.
 
Akiwahutubia wananchi wa kata ya Kasamwa juzi diwani huyo alisema kumeibuka wimbi la walinzi wa mgodi huo kujichukulia sheria mkononi ya kuwapiga na kuwauwa kwa risasi wananchi wanaoonekana katika mgodi huo na baadhi ya wananchi kupata ulemavu wa kudumu hatua ambayo imejenga mahusiano mabaya kati ya wananchi wa Geita na uongozi wa mgodi huo.
 
‘’Ndani ya siku saba kama kutatokea mauaji tena huko mgodini…walai nitahamasisha maandamano ya amani…viongozi hawa nimewapa hizo siku saba,kuhakikisha..wanalitolea ufafanuzi tatizo hilo,wananchi sio chawa wa kila wakati wanauawa’’alisema diwani huyo.
 
Mbali na kupinga mauaji hayo pia.diwani huyo alisema amepinga utaratibu uliotumika katika suala la uuzaji wa viwanja vya serikali ambavyo vinauzwa kinyume na taratibu kwa wananchi kwa gharama kubwa,ambapo kiwanja kidogo kinauzwa kwa sh.600,000 hadi 3,000,000 tofauti na bei ya iliyozoeleka ya kila kiwanja kuuzwa sh.560,000 kiwanja kidogo,cha kati sh.800,000 na kiwanja kikubwa ambacho huuzwa sh.1,000,000.
 
Alisema utaratibu huo umefanyika bila kuwashirikisha madiwani wa halmashauri hiyo ambao ndiyo wenye maamuzi ya mwisho ya utekelezaji na mipango ya maendeleo na kwamba kamati ya ugawaji wa viwanja ya mji huo haikutoa ushirikiano katika kupanga bei hiyo hatua ambayo amedai kama haitadhibiwa na viongozi hao wananchi watakosa imani na serikali yao.
 
Aidha kwa upande wake katibu wa chadema mkoa wa Mwanza,Wilison Mshumbusi alisema chama hicho hakiwezi kuvumilia wananchi kuendelea kunyanyasika katika nchi yao kwa kukumbatia wawekezaji na kuwageuza wazalendo kuwa wanyama wa kuuwa kila kukicha na hivyo kuwataka wananchi kukiunga mkono chama hicho katika kupigania haki zao.
 
Alisema serikali mkoani Geita inatakiwa kujipanga kutatua mvutano uliopo kati ya wananchi wanaoishi jirani na mgodi huo na uongozi wa mgodi ili kumaliza mauaji na maandamano ya kila wakati yanayogharimu maisha ya wananchi.
 
Kwa upande wake katibu wa chama cha CUF wilayani geita Seveline Malugu ameliambia gazeti hili kuwa chama chake kinaungana na Chadema katika kukemea mauaji hayo ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara lakini serikali ikionekana kuyafumbia macho matukio hayo.
 
"katika hili sisi kama CUF tuna laani kwa nguvu zote vitendo hivi kwa kuwa vinatokea na serikali ya wilaya na mkoa vikiwepo lakini hakuna hatua zozote za masingi ambazo zimechukuliwa ili kukomesha kuendelea kwa mauaji ya wananchi wetu...hii ni nchi yetu sote tunatakiwa tuishi kwa amani na utulivu...kitendo cha kuendekeza maslahi ya mwekezaji kuliko uzalendo wa nchi haina maana kabisa"alisema malugu.
 
Aidha alibainisha kuwa Chama hicho kinatarajia kufanya maandamano ya amani kuishin ikiza serikali kudhibiti vitendo vya mauaji ya wananchi ikiwemo kuiomba kuwatimua kazi baadhi ya viongozi wa serikali ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kuendekeza maslahi yao binafsi kutokana kwa mwekezaji huyo GGM na kushindwa kulinda maslahi ya jamii,
 
 
Kauli za viongozi hao zimekuja siku chache baada ya mwanafunzi wa darasa la sita Hoja Juma wa shule ya msingi Kivukoni kufa na mwingine kujeruhiwa vibaya kwa kile kilichosadikika kupigwa risasi na walinzi wa mgodi huo wakati akiokota vyuma chakavu kwenye mgodi huo kwa lengo la kwenda kuviuza kupata fedha ya kununulia sare za shule.
 
Tukio hilo lililotokea alhamisi iliyopita lilisababisha wananchi zaidi ya 600 wa Mwatulole anakoishi mwanafunzi huyo,siku iliyofuata kuandamana hadi kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya Geita kupinga mauaji hayo ambayo yametokea mwezi mmoja baada ya kutokea maandamano yaliyopelekea gari la mgodi huo kuteketezwa kwa moto na wananchi.

                                              .MAUAJI YA KINYAMA MGODINI GEITA
                                             .MWANAFUNZI WA DARASA LA SIT AUAWA KWA RISASI
                                             .ALIKUWA AKIOKOTA VYUMA CHAKAVU



                                                      Mgodi wa Dhabu wa Geita (GGM)

Na Daniel Limbe, Geita
KWA mara nyingine mgodi wa dhahabu wa Geita[GGM]umeingia katika kashifa kubwa baada ya walinzi wake kumpiga risasi na kumuuwa mtu mmoja ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya msingi kivukoni huku mwingine akijeruhiwa kwa risasi sehemu mbalimbali za mwili wake.
Tukio la mtoto huyo kupigwa risasi na kufa limepelekea zaidi ya wakazi 800 wa kitongoji cha Mwatulole katika Mji wa Geita Mkoani Geita kufanya maandamano makubwa hadi katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Geita,wakipinga kitendo cha Walinzi wa Mgodi wa Geita kumuua kijana huyo ambaye ni mwananchi mwenzao aliyetambuliwa kwa jina la Hoja Juma..
Maandamanao hayo yalianza jana majira ya saa 5 asubuhi katika kitongoji hicho kilichopo umbali wa kilkomita tatu kutoka katikati ya Mji wa Geita,na kupitia barabara kuu iendayo katika mikoa ya Kagera,Kigoma na Nje ya nchi,na kisha kupita katika eneo la mamlaka ya mji Mdogo hadi katika ofisi ya Mkuu wa wilaya.
Hata hivyo waandamanaji hao hawakufanya vurugu ya aina yoyote kama ambavyo ilitokea hivi karibuni,na baada ya kufika katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Geita waliketi chini na kutaka kuonana na Mkuu huyo wa wilaya.
Walidai kuwa walinzi wa Mgodi wa Geita wamemuua kwa kumpiga kwa risasi mwananchi mwenzao ambaye ni Mwanafunzi wa Darasa la sita katika shule ya Msingi Kivukoni,ambaye pamoja na wenzake waliingia katika eneo la mgodi huo kwa ajili ya kuiba vyuma chakavu na kuviuza ili kupata fedha za kununulia sare za shule.
Bw.Thomas Ngusa ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya shule alipokuwa akisomea marehemu akizungumza katika eneo la maandamano,alisema wamechoshwa na vitendo vya ndugu zao kuuawa ama kujeruhiwa na kusababishiwa vilema vya maisha na walinzi wa mgodi huo,hivyo ni vyema serikali ikachukua hatua za haraka za kudhibiti vitendo hivyo badala ya kuweka nta masikioni kama ilivyo sasa.
“Kwanza tuinataka kujua nini hatima kwa huyu marehemu ambaye tayari ameuawa na yuko kwenye chumba cha kluhifadhia maiti,wao tayari wamemuua na wamekaa kimya sisi ndiyo kwa sasa tunahangaika wamekaa kimya,kwanza hii ni dharau inaonekena hawa wawekezaji wamekwishatudharau sana sisi wanageita na watanzania kwa ujumla…….’’alisema Ngusa na Kuongeza.
“Hiyo ni mojan lakini pili tunataka kujua ni kwa nini sasa mauaji dhidi ya raia wenzetui ndani ya mgodi wa Geita yanaonekana kuzoeleka kwa kiasi kikubwa?!!,nanyi kama serikali mumeweka nta masikioni hivi inamaana hakuna serikali hapa,tunatambua kwamba Maiti siku zote hainja haki lakini mnadhanai inaleta picha gani kwa jamii na hasa ndugu,huu ndio tunaita uhasama na kwamba kama serikali haitachukua hatua za haraka katika kutatau tatizo hili ni wazi kwamba kuna siku nchi hii itakuja kutikisika…..’’.
Kwa mujibu wa habari zilkizothibitishwa na jeshi la polisi wilayani Geita Marehemu amefariki Dunia baada ya kupigwa risasi kwenye ubavu wa kulia huku mmwenzake mmoja aliyetambuliwa kwa jina la SwiraMussa (18),ambaye pamoja na majeraha ya risasi aliyo nayo mwilini anashikiliwa na jeshi la Polisi katika kituo kikuu cha polisi Mjini hapa.
Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Geita Ronard Makona alithibitishia Gazeti hili kutokea kwan tukio hilo pamoja na kuwepo kwa maandamano ya wananchi hao,huku akimtaja Mlinzi wa Mgodi wa Geita anayedaiwa kumuu kwa risais mwanafunzi huyo kuwa ni Exavery Revocatus ambaye anafanya kazi ya ulinzi katika kampuni ya G4S iliyoko katika Mgodi wa Geita ambaye anashikiliwa na polisi Mjini Geita.
Akizungumzia tukio hilo Baba Mzazi wa Marehemu Leonard Salala alisema amesikitishwa na mauaji ya mwanaye yaliyofanywa na walinzi hao wa mgodi wa Geita,na kwamba hakutegemea kama angepatwa na kifo kwa wakati huu kwani alikuwa amemuacha nyumbani na kwenda kutafuta fedha za kumnunulia sare za shule baada ya kufukuzwa shuleni.
“Alifukuzwa shule kwa sababu hakuwa na sare na ni kweli kwa sababu maisha tunayoishi ni magumu na hasa ikizingatiwa kwamba naishi naye peke yangu baada ya Mke wangu kukimbia kutokana na maisha yetu kuwa ya dhiki,na hiyo siku(Jana)..nilimuacha nyumbani na kumwambia nakwenda kutafuta fedha ili nikamnunulie sare……’’ alisema Baba wa Marehemu.
Aliongeza…”Niliporudi nikapata taarifa kwamba alifuatwa na vijana wenzake na kuwambia kwamba waende huko mgodi wakachukue vyuma chakavu ili wauze na kwa sababu wenzake wamekuwa wakifanya biashara hiyo alishawishika na kuamua kwenda na ndipo alipokutwa na kifo hicho…..’’.
Kwa mujibu wa taarifa ya Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu Dk.Venance Nyanda,kifo cha marehemu kimesababishwa na Kuvuja damu nyingi iliyotokana na kupigwea risasi kwenye ubavu wa kulia na hivyo kuharibu vibaya mapafu yake.
Hili ni tukio la tatu kutokea katika kipindi cha kisichozidi miezi miwili ambapo katika matukio mengine kama hilo wananchi wa mji wa Geita waliandamana na kufanya vurugu kubwa ikiwa ni pamoja na kuchoma moto magari ya Mgodi huo.
Akizungumza na wananchi hao waliondamana katika viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Wilaya kwa niaba ya Mkuu wa wilaya hiyo aliyeko Safarini Mjini Dodoma Katibu Tawala Wa Wilaya Moses Minga,aliwataka wananchi hao kuacha vitisho kwa wafanyakazi wa Mgodi huo,pamoja na kuwanyang’anya silahan walinzi wa mgodi huo.
Kauli hiyo ya Katibu Tawala ilikuja kutokana na wananchi hao kukataa kuuchukuwa mwili wa marehemu katika chumba cha kuhifadhia maiti,huku wakiwapiga marufuku wafanyakazi wa mgodi huo kuishi nao mitaani bali wakaishi ndani ya mgodi kwa vile wamegeuka wauaji wa kuwaua ndugu zao bila kujali utu wa Mwanadamu.
Aidha wananchi hao waliutupia lawama uongozi wa wilaya kwa kutojali na kushughulikia mauaji ya ndugu zao ambao wamedai wamekuwa wakiuawa mara kwa mara katika eneo la Mgodi huo na,huku wakisistiza kwamba unapopita pembezoni mwa mgodi huo unakutana na harufu wanazodaiwa ni za watu waliouawa na walinzi wa mgodi huo.
Hata hivyo kauli hiyo ilipingwa vikali na Katibu Tawala huyo wa wilaya na kueleza kwamba serikali imekuwa ikifanyia kazi malalamiko mbalimbali yanayotolewa juu ya mauaji yanayodaiwa kufanyika ndani ya mgodi huo dhidi ya raia,na kuwaonya wananchi hao kuacha vitisho dhidi ya wafanyakazi wa mgodi wa GGM pamoja na wawekezaji.

                              MWALIMU AFARIKI  KWA KULIPUKIWA KIBATARI

                             Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufunzdi Dk Shukuru Kawambwa
Na Daniel Limbe,Chato
WALIMU watatu wa Shule za msingi wilayani Chato mkoani Geita wamefariki dunia katika matukio tofauti,likiwemo la mmoja wao kulipukiwa na moto wa kibatari wakati akiweka mafuta ambayo yanasadikiwa kuwa na mchanganyiko petroli.
 
Akizungumza na NIPASHE jana Ofisa elimu wa shule za msingi wilayani Chato Ishengoma Kyaruzi alisema katika tukio la kwanza lilimhusisha mwalimu wa shule ya msingi Chabulongo Asma Mudongwa (26) ambaye alifariki dunia jana katika hospitali ya wilaya hiyo baada ya kulipukiwa na moto uliosababishwa na mafuta yanayosadikiwa kuwa na mchanganyiko wa Petrol wakati akiweka kwenye taa ya kibatari.
 
Kyaruzi alisema tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 3.30 usiku wakati marehemu akiwa nyumbani kwake katika kijiji cha Chabulongo kata ya katende wilayani chato,ambapo inadaiwa alichukua chupa ya mafuta na kuanza kumimina kwenye taa hiyo na kitambo kidogo kibatari hicho kililipuka hali iliyosababisha moto kutapakaa na kumuunguza kwenye paji la uso hadi kwenye utosi wa kichwa baada ya ngua zake kushika moto.
 
Hatua hiyo ilipelekea Mume wa marehemu huyo ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya msingi Chabulongo Khabibu Nuru kutoa taarifa kwenye uongozi wa halmashauri hiyo na kulazimika kukimbiza gari katika eneo la tukio lakini wakati akiendelea kupata matibabu katika hospitali ya wilaya ya chato mauti yalimkuta mnamo saa 7 mchana.
 
Kyaruzi aliongeza kuwa taratibu za kusafirisha mwili wa marehemu kwenda nyumbani kwao wilayani Mkuranga Mkoani Pwani zinafanyika ambapo kutokana na mazungumzo ya pande mbili kati ya mume na mke wamekualiana mazishi kufanyika mkoani humo na kwamba marehemu ameacha mtoto mmoja wa miezi 9.
 
Katika tukio la pili alisema lilimhusisha mwalimu wa shule ya msingi Nyamirembe Getruda Batenda (54) ambaye alifariki mei 24 katika kijiji cha Nyamirembe wilayani hapa kutokana na kinachosadikiwa kunywa pombe aina ya gongo hali iliyopelekea sukari kushuka na kusababisha mauti yake.
 
Alisema baada ya taratibu za mazishi kukamilika marehemu alizikwa kwenye mashamba yake yaliyopo kijijijini hapo,Huku tukio la tatu likimhusisha mwalimu wa shule ya msingi Kakanshe Kalilo Mukama (25) ambaye alifariki mei 26 mwaka huu baada ya kuugua ugonjwa wa Malaria na kupelekea kifo chake na kwamba mwili wa marehemu utasafirishwa kupelekwa nyumbani kwao katika kijiji cha Mwibara wilayani Bunda mkoani Mara.
 
Katibu wa Chama cha walimu (CWT) wilayani hapa Victoria Baseka amekiri kutokea kwa vifo hivyo na kudai kuwa hatua hiyo ni pigo kubwa kwa walimu na wananfunzi ambao walitegemea kuendelea kupata taaluma kutoka kwa walimu hao ambao wamepoteza maisha kwa kipindi cha mwezi mmoja.
 
Aidha Baseka aliwataka walimu na wanafunzi wote katika wilaya ya chato kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu na kuamini kuwa kifo ni mpango wa mwenyezi mungu na kwamba hakuna haja ya kukimbilia kwa waganga wa jadi kutafuta mchawi hali inayoweza kuleta uvunjifu wa amani katika jamii.
 
Jeshi la polisi wilayani hapa limekiri kuwepo kwa matukio hayo na kwamba hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na matukio hayo.



                                             LEMA ASAMBARATISHA KWA MAGUFULI

                                   Aliye kuwa Mbunge wa Arusha Mjini Bw, Godless Lema

Na Daniel Limbe,Chato
ALIYEKUWA mbunge Jimbo la Arusha Mjini Godbress Lema (CHADEMA) amezidi kuzisambaratisha ngome za waziri wa ujenzi Dk John Magufuli baada ya makada saba wa Chama cha Mapinduzi CCM jimbo la Chato kukihama chama hicho na kujinga na Chadema,huku akionekana kushangazwa na uwezo mkubwa wa waziri huyo katika kutambua wingi wa samaki walioko majini pamoja na mimba zao, lakini ameshindwa kutatua tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa jimbo lake.
 
Akizungumza na wananchi wa jimbo la chato juzi (jana) kwenye mkutano wa hadhara Lema alimtupia lawama Dk Magufuli kushindwa kuwatumikia wananchi wake katika kutatua matatizo yanayo wakabili ikiwemo ukosefu wa maji safi na salama ambapo wananchi hao wamekuwa wakitumia maji ya yasiyofaa kwa matumizi ya binadamu kutokana na kutumiwa na mifugo na wengine kuchota maji machafu ya ziwa ambayo yamekuwa yakiwasababishia magonjwa ya kuhara.
 
Lema aliwataka wananchi wa jimbo hilo kutambua kuwa saa ya ukombozi ni sasa, na kwamba hawana budi kujiunga na Chadema kwa kuwa ndiyo chama makini chenye kutetea maslahi ya wanyonge na kupambana na ufisadi wa viongozi wa nchi hii akiwemo magufuli ambaye amejilimbikizia mali kinyume cha sheria na kushindwa kuwathamini wananchi waliomchagua kuwa mbunge.
 
“Ndugu zangu inasikitisha sana kuona chato ndiyo hii…wakati nikipita njiani kuja huku nimeshuhudia ziwa likiwa karibu kabisa na makazi yenu kiasi kwamba mbunge wenu angekuwa na nia thabiti ya kuwatumikia ninaimani wananchi wa hapa msingelikuwa masikini wa kutupwa namna hii…mimi ni mara yangu ya kwanza kufika hapa lakini kutokana na mbwembwe za Magufuli bungeni kuonyesha anafahamu aina,idadi na mimba za samaki waliomo ndani ya maji niliamini Chato inafanana na Arusha kumbe la”alisema.
 
“Nimeshuhudia majumba mengi aliyojilimbikizia magufuli…sikutarajia kwa utajiri alionao kama mngelikuwa na tatizo la maji tangu uhuru wa Tanganyika …Magufuli ameshindwa kuongoza nahii inatokana na kumpa ubunge kwa takribani miaka 20 ndiyo maana amejisahau na kuona ninyi mliomchagua hamfai, kwa maana tayari ameshalewa madaraka”alisema Lema
 
Kauli hiyo ilipelekea baadhi ya wananchama 27 wa CCM wakiwemo makada saba kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema,hatua iliyotofasiliwa kuwa ni kuendelea kuvunjwa ngome za waziri Magufuli ambaye pia ni mbunge wa jimbo la chato kutokana na nafasi zingine za wenyeviti wa vijiji 8 kati ya 11 kutwaliwa na Chadema katika uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizokuwa zimeachwa wazi na viongozi waliokuwepo awali baada ya kujihudhuru na wangine kuhama makazi yao.
 
Makada wa CCM waliokihama chama hicho ni aliyekuwa mwenyekiti wa kijiji cha Mkuyuni Uhuru Selemani,aliyekuwa katibu wa vijana kata ya chato, mjumbe wa baraza kuu la vijana mkoa wa kagera,mjumbe wa kamati ya utekelezaji mkoa wa kagera na katibu wa hamasa chipukizi wilaya ya chato Masumbuko Kaitila, Lusia Kahindi,Fikiri Makoye,Samwel Mkome,Emmanuel Kayila na Vigoro Lucas ambao wote walikuwa ni wanachama wa CCM.
 
Huku akitumia kauli mbiu ya “Vua gamba vaa ngwanda, na vua ukada vaa Ukamanda”Lema aliwataka watumishi wa serikali hususani jeshi la polisi kuacha kutumia nafasi zao vibaya katika kuwanyanyasa wananchi wakiwemo viongozi wa Chadema na kwamba wanantakiwa kutenda haki pasipo kuegemea kukitumikia chama tawala kwa madai kitambo kidogo kimebaki Chadema kushika utawala wa nchi.
 
Alisema baadhi ya askari polisi wamekuwa wakitumiwa vibaya na viongozi wa chama tawala kutokana na kushinikizwa kuwapiga kwa malungu,Mabomu na kuwabambikiza kesi baadhi ya wananchi na wafuasi wa vyama vya upinzani wakiamini kuwa njia hiyo itasaidia kudidimiza kasi ya mageuzi kwa jamii hatua ambayo imekuwa ikiongeza chuki kwa wananchi dhidi ya polisi na serikali yao.
 
Aidha aliwataka wananchi kwa kushirikiana na viongozi wa Chadema kushirikiana kwa pamoja kufanya maandamano ya amani kuishinikiza serikali kuwafukuza kazi watendaji wabovu na wabadhilifu wa fedha za miradi ya maendeleo ya wilaya ya chato ambazo zimedaiwa kutafunwa bila huruma huku serikali ikishindwa kuwachukulia hatua stahiki ikiwa ni pamoja na kuwaburuza mahakamani.
 
“Niwaelezeni ukweli ndugu zangu,hata maandiko yanaeleza kuwa mtu mwoga hawezi kuingia kwenye utukufu wa mungu…mnatakiwa kuwa majasiri katika kudai haki yenu ambayo mnaona inaporwa na watu wachache…ikiwezekana hata watu wachache lazima wafe kwaajili ya kusaidia walio wengi”,alisema
 
Kwa upande wake Godifrey Gwakisa alimtuhumu Dk Magufuli kwa ufisadi wa kupindukia kutokana na kuiba raslimali za nchi na kuwekeza kwa maslahi yake binafsi hatua aliyodai kuwa kiongozi huyo hafai kuwa kiongozi na anapaswa kujihudhuru haraka ili kutoa mwanaya kwa wengine wenye uchungu wa kuwatumikia wananchi badala ya kuendela kumkubatia alihali wananchi wanazidi kutesema na ugumu wa maisha kila kukicha.
 
Alisema Dk Magufuli amejilimbikizia majumba zaidi ya 100 ikiwemo ghorofa alilojenga kuishi watumishi wa shamba lake lililopo nyabirezi wilayani chato mkoa mpya wa geita,farasi kwaajili ya watumishi hao kutembelea ikiwemo kanisa alilojenga nyumbani kwao na kuliita jina la marehemu mzazi wake ambalo hata hivyo lilikataliwa na wananchi baada ya kutaka madhehebu yote kuteua muda maalumu kwaajili ya kufanya ibada zao ndani ya jengo hilo ambalo linaonekana kutumia gjharama kubwa ya fedha za walipa kodi wa Tanzania.  
 
                              CHADEMA YAMKOMALIA NGEREJA NA WENZAKE


                                         Katibu Mkuu wa Chadema Dk Willbroad Slaa.
Na. Daniel Limbe,Sengerema
CHAMA cha demokrasia na maendeleo (Chadema) kimesema lazima kiwafikishe kwenye vyombo vya sheria aliyekuwa waziri wa nishati na madini Wiliam Ngeleja na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Sengerema Mathew Lubongeja kwa kosa la kushindwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusababisha ufisadi wa mamilioni ya fedha za serikali kwenye halmashauri hiyo.
 
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya waziri mkuu Mizengo Pinda kutoa agizo la kuhakikisha wakurugenzi wa halmashauri za wilaya ya Sengerema na Misungwi mkoani Mwanza wanachukuliwa hatua za kisheria kwa kuwafikisha mahakamani kwa kosa na ulaji wa fedha za umma kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali [CAG] ya mwaka 2009/10.
 
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya CAG ni kwamba watumishi 21 katika halmashauri ya Sengerema wa idara za fedha,manunuzi,elimu,maji,ujenzi,afya na kilimo na mifugo wametajwa kuhusika kutafuna sh.2.5 bill fedha za miradi ya maendeleo hatua ambayo mkuu wa mkoa wa Mwanza Evarist Ndikilo mei 8,mwaka huu alimlazimu kutoa siku 14 kwa watumishi hao kuandika barua za kujitetea juu ya tuhuma zinazowakabili.
 
Kufuatia hatua hiyo chadema kimedai hakiwezi kukaa kimiya kwa kulifumbia macho sakata hilo na kusema kuwa serikali inapaswa kuwafikisha makamani haraka kabla ya chama hicho hakijachukua uamuzi mgumu wa kuwapandisha mahakamani  kwa nguvu watuhumiwa hao akiwemo mwenyekiti Lubongeja aliyesaini mikata hewa na kujirimbikizia mali .
 
Katika kutekeleza hatua hiyo waliokuwa madiwani wa ccm kata za Nyampulukano Hamisi Tabasamu na Adrian Tizeba kata ya Lugata baada ya kuhamia chadema wamesema wako tayari kwenda kutoa ushahidi mahakamani kuhusu namna fedha hizo zilivyoliwa kutokana na mwenyekiti kushindwa kusimamia vyema majukumu yake.
 
Kauli ya kuwaburuza mahakamani Ngeleja na Lubongeja ilitolewa juzi kwa nyakati tofauti na mbunge wa jimbo la Nyamagana[chadema]Ezekiel Wenje wakati akiwahutubia wananchi wa Katunguru kwenye kata ya mwenyekiti huyo na Sengerema,huku akilaani kitendo cha Ngeleja kujisafisha kwa kutumia mabango ya magazeti yaliyochapisha taarifa ya kichwa cha habari Zitto Kabwe amsafisha Ngeleja.
 
‘’Zitto hata siku moja hawezi kumsafisha Ngeleja…amsafishe wakati yeye ndiyo alikuwa anakusanya sahihi za kutokuwa na imani na waziri mkuu kwa kushindwa kuwasimamia mawaziri wake,hili Gazeti[jina linahifadhiwa]ni ccm na haitatokea Zitto akafanya kitendo hicho’’alisema mbunge huyo.
 
Wenje alisema mwenyekiti wa halmashauri ya Sengerema  kati ya mikataba 73 aliyoisaini ,mikataba 13 ni mikataba hewa suala ambalo alisema sio la kulifumbia macho huku akikemea wananchi kujichukulia sheria mikononi za kuwapiga na kuwauwa wezi wa mifugo na mali zingine na badala yake wajikite kufuatilia waliokula fedha za serikali ndiyo wanaotakiwa kufanyiwa kitendo hicho.
 
‘’Lazima huyu[mwenyekiti]tumshitaki na kama itashindikana tutafanya maandamano ya amani kushinikiza serikali iwafikishe kortini,naye mbunge wenu[Ngeleja]kutokana na kashifa ya ufisadi wa sh.600 mill lazima tupande naye mahakamani..acheni ajisafishe’’alisema Wenje.
 
Kwa upande wake aliyekuwa mbunge wa jimbo la Arusha mjini Godbless Lema aliwataka wananchi kutambua uthamani wa maisha yao kupinga unyanyasaji na kutoa wito kushikamana katika kupinga hali hiyo ambayo baadhi ya watu wamekuwa wakiundiwa kesi na polisi kwa kuwabambikiziwa kesi za mauaji,ubakaji na kuwapeleka magerezaji kwa kupinga kauliza viongozi wa vyama vya siasa na serikali.
 
Katika hatua nyingine,Lema alisema kama serikali itashindwa kuwafikisha mahakamani mawaziri walioondolewa katika nafasi zao akiwemo mbunge wa jimbo la Sengerema Ngeleja kwa ufisadi inapaswa wafungwa walioko magerezani kwa makosa ya wizi wa simu,ng’ombe,kuku na baiskeli wafunguliwe wawe huru.
 
Aidha chama hicho kilivuna wanachama wa ccm 20,waliorudisha kadi zao na kujiunga na chadema kutoka Katunguru na Sengerema mjini,muda mfupi baada ya Lema kutangaza oporesheni ya nchi nzima ya”Vua Ngamba Vaa Gwanda’’

                           TAKUKURU YAISHUKIA MAHAKAMA YA ARDHI CHATO


                                       Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru Dk Edward Hossea
Na Daniel Limbe,Chato
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) wilayani chato mkoani kagera imeishukia mahakama ya ardhi na nyumba wilayani humo kwa madai ya kugeuza ofisi hiyo duka la kuuza haki kwa wananchi kinyume cha sheria,hatua ambayo imepelekea baadhi ya wananchi kupoteza imani na huduma zinazotolewa na mahakama hiyo.
 
Hatua hiyo imekuja siku chache baada ya taasisi hiyo kupitia dawati la utafiti,udhibiti na takwimu kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na utendaji kazi wa mahakama ya ardhi na nyumba wilayani humo,ambapo ilibaini ukiukwaji mkubwa wa uwajibikaji wa watendaji wa sekta hiyo muhimu kwa wananchi.
 
Akizungumza na NIPASHE Kamanda wa Takukuru wilayani chato Ellimius Millanzi alisema kuwa taasisi yake ililazimika kufanya utafiti huo kutokana na malalamiko ya wananchi wengi waliofika katika mahakama hiyo kwa lengo la kupata ufumbuzi wa migogoro ya ardhi zao,na baadaye kutoridhishwa na utendaji kazi wa baadhi ya viongozi wa mahakama hiyo kutokana na kuendekeza vitendo vya kuomba rushwa.
 
Millanzi alisema utafiti huo ulifanyika mwezi machi hadi mei 2012 kwa njia ya mahojiano na wananchi,viongozi na watendaji mbalimbali waliopo kwenye maeneo ya wilaya hiyo ambapo Takukuru ilibaini kesi nyingi zinazofunguliwa dhidi ya serikali zimekuwa zikiisha kwa serikali kushindwa, kutokana na kutotoa rushwa hali ambayo imekuwa ikiisababishia hasara kubwa.
 
Akitoa mfano wa soko la Iparamasa alisema “Kuna mwananchi mmoja aliishtaki serikali ya kijiji cha Iparamasa baada ya kujenga soko kwenye eneo alilodai lilikuwa la kwake na mahakama ya ardhi na nyumba wilayani hapa iliamuru soko hilo kuvunjwa,licha ya kuwa tayari ilikuwa imeshawekeza gharama kubwa kutokana na kodi mbalimbali za wananchi”alisema
 
“ Kama haitoshi mahakama hiyo imekuwa ikilalamikiwa kwa kitendo chake cha kupokea upya kesi ambazo tayari zimekwisha tolewa hukumu na mahakama zingine za juu…kuendesha mashauri na kutoa hukumu bila kwenda kwenye eneo la migogoro…na baadhi ya kesi zimekuwa zikisikilizwa kwa kipindi kirefu baada ya kuahirishwa mara kwa mara pasipo kuwa na sababu za msingi”alisema Millanzi.
 
Mambo mengine ni pamoja na kuishi jijini mwanza badala ya chato ambapo ndiyo kituo chake cha kazi,hivyo kupelekea kushindwa kupata muda wa kutosha kusikiliza kesi za wananchi,kuzitoa mahakamani baadhi ya kesi ambazo walalamikaji wanatoa taarifa za kutofika mahakamani kwa sababu mbalimbali ikiwemo ugonjwa,licha ya kuwepo kwa kesi zingine ambazo walalamikaji walitoa udhuru kwa zaidi ya mara tatu na zinaendelea kuwepo mahakamani hapo kutokana na mazingira ya rushwa.
 
Millanzi aliongeza kuwa baadhi ya wananchi wamekuwa wakiilalamikia mahakama hiyo kuwa imekuwa duka la kuuzia haki kwa sababu ya kukithiri kwa vitendo vya rushwa katika utoaji haki na kwamba mtu anayetoa pesa ndiye amekuwa akishinda kesi,hali  ambayo imepelekea wananchi wengi kutolidhishwa na utendaji kazi wa mahakama hiyo.
 
Kufuatia hali hiyo TAKUKURU imelazimika kupeleka utafiti huo kwenye ofisi ya mkuu wa wilaya ya chato Hadija Nyembo kwa lengo la kutaka wadau wa maendeleo ikiwemo Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya,mashirika yasiyo ya kiserikali,Ofisa ardhi maliasili na mazingira,diwani na ofisa tarafa ya chato kujadili na kutoa mapendekezo namna ya kutatua kero zilizopo kwenye mahakama hiyo.
 
Akijibu tuhuma hizo Hakimu wa baraza la ardhi na nyumba wilayani hapa Elias Mogasa alikiri kupokea malalamiko hayo, huku akikanusha vikali ofisi yake kujihusisha na vitendo vya kuomba na kupokea rushwa kwa madai uwajibikaji wa mahakama hiyo imeboreka ukilinganisha na idadi ya kesi zilizokuwepo awali na hivi sasa.
 
Alisema tangu kuanzishwa kwa mahakama hiyo mwaka 2007 kwa lengo la kuhudumia wakazi wa wilaya tatu za Chato,Biharamulo na Ngara zaidi ya kesi 580 zilifunguliwa na kati ya hizo kesi 425 zimeshatolewa maamuzi huku kesi 157 zikiendelea kusikilizwa mahakamani hapo,nakwamba takwimu zinaonyesha kuwa wilaya ya ngara inaongoza kwa kesi nyingi ikifuatiwa na Biharamulo na mwisho ni Chato.
 
Aidha Mogasa alisema kuwa anachokiamini yeye ni kuwa wananchi wana imani na utendaji kazi wa mahakama hiyo kutokana na kulidhishwa na maamuzi yanayotolewa pindi pande mbili zinapo kuwa na mvutano wa migogoro ya ardhi ambayo baadhi yake imekuwa ikitishia uvunjifu wa amani kwa wananchi.
 
Hata hivyo alidai taarifa iliyotolewa na TAKUKURU ni changamoto katika kuongeza uwajibikaji wa mahakama hiyo katika kutenda haki dhidi ya kesi zinazofikishwa hapo.
 
Kwa upande wao baadhi ya wananchi na viongozi wa vyama vya siasa wilayani hapa wameupongeza uamuzi wa taasisi hiyo kufanya utafiti kwenye mahakama hiyo ambayo wamedai kumekuwa na urasimu mkubwa katika upatikanaji wa haki kwa kesi zinazopelekwa hapo kutokana na viongozi wake kupenda rushwa kuliko kutenda haki.
 
Salum Selemani mkazi wa kijiji cha Kalema na Frola Mashauri mkazi wa mkuyuni wamesema TAKUKURU wamefungua ukurasa mpya katika kuhakikisha haki kwa jamii inatendeka kwa kuzuia mianya yote ya rushwa huku wakiishauri kwenda mbele zaidi hasa katika idara ya afya kutokana na baadhi ya wauguzi wilayani humo kuendekeza vitendo vya kuomba rushwa kwa wagonjwa na mama wajawazito ambao hufika kwenye hospital,vituo vya afya na zahanati ili kupata huduma za kiafya.
 
Wamedai kuwa baadhi ya wanawake wajawazito wamekuwa wakiombwa fedha na wauguzi pindi wananpo kwenda kujifungua kwenye hospitali ya wilaya hiyo kinyume cha sheria na kwamba wanapo kaidi hupata matibabu yaliyochini ya kiwango kwa lengo la kuwakomoa.
 
                                                                                                Mwisho.