Saturday, July 28, 2012

KUKU WA AJABU AIBUKA SENGEREMA AKIWA NA HIRIZI,SHANGA NA CHALE.



WAKAZI wa mtaa wa barabara ya Nyanchenche mjini Sengerema juzi walifurika kushuhudia tukio la ajabu lisilokuwa la kawaida baada ya kuonekana kuku dume wa ajabu akiwa hana manyoya na akitembea huku akiwa amefungwa shanga na hilizi mbili shingoni na mabawa yake yakiwa yamechanjwa chale na kupakwa dawa nyeusi za kienyeji.

Tukio hilo lililovuta umati mkubwa wa watu lilitokea juzi majira ya saa 7:00 mchana kwenye moja ya familia ya mtaa huo[jina limehifadhiwa]ambaye alidai kwamba kuku huyo alijitokeza nyumbani kwake bila kufahamu alikotokea.

Kuku huyo wa ajabu alikutwa na wananchi katika mji huo ambao uko kando kando ya barabara,jambo ambalo limeshituwa mamia ya wananchi wa mji wa Sengerema ambao walifika katika eneo hilo ili kushuhudia tukio hilo ambalo wamelihusisha na imani za kishirikina.

Katika tukio hilo la kuonekana kuku wa ajabu hakuna hata mwananchi aliyejitokeza kumshika kuku huyo huku wenyeji wa mji husika wakiendelea na shughuli zao licha ya kuonyesha mshituko wa tukio hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa kitongoji hicho Leah James alionyesha kushangazwa na tukio hilo na kusema kuwa ni la ajabu haijawahi kutokea jambo kama hilo katika kitongoji hicho ambalo limeibuwa hisia tofauti miongoni mwa wanajamii.

“Nimepata taarifa za tukio hili ilikuwa mchana muda wa saa saba na tumefika mpaka eneo la tukio ….kwa kweli inashangaza na kusikitisha huyo kuku wa ajabu hana nyoya hata moja wala alama ya kidonda na amechanjwa chale kwenye mbawa zake,kavishwa hilizi mbili shingoni na amefungwa shanga kwenye mbawa zake”alisema mwenyekiti.

Baada ya tukio hilo uongozi wa eneo hilo na jeshi la jadi sungusungu uliamuwa kuitisha mkutano siku iliyofuata leo(jana) ambapo walifuatilia na kumbaini mmiliki wa kuku huyo kuwa ni  Leticia Makoye ambaye alidai kuku huyo ni wake na  humtumia katika shughuli za uganga wa kienyeji .

Kikao hicho kiliamua kumrudishia kuku huyo ingawa alikuwa amekufa kutokana na kupigwa baridi usiku kucha,maamuzi yaliyopingwa na wananchi na hivyo kulazimika kumshambulia kwa mawe hadi nyumbani kwake huku viongozi wa mtaa huo wakimpatia ulinzi hadi alipoingia ndani ya nyumba.

Nao baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili eneo la tukio wamekuwa na hisia tofauti huku baadhi yao wakilihusisha na imani za kishirikina kutokana na vitu alivyokutwa navyo kuku huyo ikiwa ni pamoja na shanga,hilizi,na chale alizochanjwa kwenye mbawa zake.

Baadhi ya wananchi hao Grece Michael (32) Fadhili Alfani (45) na Daniel Marco walisema kuanza kutokea kwa matukio ya ajabu kama hilo ni dalili za mwisho wa dunia kutokana na vitendo vya kishirikina kuongezeka na kwamba njia pekee ya kuepukana navyo ni kudumu katika sara na imani ndiyo njia pekee.
                                 Mwisho.

Saturday, July 21, 2012

                     MAJAMBAZI YATEKA KIJIJI,YAPORA FEDHA NA SIMU



                                        Kamanda wa Polisi mkoa wa Gita Leonard Paul

Na Daniel Limbe,Chato
WATU wanaosadikiwa majambazi waliokuwa na silaha za kivita,mapanga na malungu wameteka kijiji cha Kibehe kata ya kigongo wilayani chato mkoani geita na kufanikiwa kupora fedha,simu za mkononi na kujeruhi baadhi ya wananchi. 


Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo majira ya saa 6;30 usiku baada ya majambazi hao kuteka kaya zaidi ya tano kabla ya kurusha risasi kadhaa hewani hatua iliyosababisha wananchi kushindwa kutoka ndani ya nyumba zao.

Wakizungumza na NIPASHE baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo Mussa Limbe na Inocent Moshi wamesema majambazi hao baada ya kuanza uvamizi huo uliodumu kwa zaidi ya saa 2 walimteka na kumweka chini ya ulinzi mwalimu wa shule ya msingi Kibehe Nyalusule Kungula na kumuamuru kuwatembeza kwenye kaya za watu wenye fedha.

Baada ya uvamizi huo,majambazi hao walitumia silaha za jadi(Mapanga na Malungu) kuwajeruhi baadhi ya wananchi kwa lengo la kuwashinikiza kutoa fedha na simu za mkononi hatua iliyopelekea kujeruhiwa vibaya katika maeneo mbalimbali ya miili yao.

"Baada ya kuvamia majambazi hayo yalianza kuwapiga kwa kutumia malungu na mapanga huku yakiwashinikiza kutoa fedha zote walizo nazo na baada ya kuchukua fedha na simu yalianza kufyatua risasi hewani ili kuwatishia wananchi"alisema Moshi.

Aidha wamedai kuwa majambazi hao wanaokadiliwa kufikia idadi ya 11 walianza kupiga yowe wakati wakiondoka na wananchi walipojitokeza kwa lengo la kusaidia kunakotokea yowe walikutana na majambazi hao na kuwashambulia kwa mapanga hatua iliyopelekea baadhi ya wananchi kujeruhiwa vibaya.

Wamewataja baadhi ya waliojeruhiwa vibaya kuwa ni pamoja na Paschal Magoma,Mwalimu wa shule ya msingi Bukamila Edwin Mponela na Mtu mmoja ambaye hajafahamika jina lake lakini anadaiwa kuwa fundi wa pikipiki katika kijiji hicho ambao wote wamelazwa kwenye hospitali ya wilaya ya chato kwaajili ya matibabu.

Kamanda wa polisi mkoani geita Leonard Paul amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba jeshi la polisi linaendelea kuwasaka watu wote wanaodaiwa kuhusika na kwamba watakapo bainika watafikishwa mahakamani.

Aidha Paul amewataka wananchi kujenga tabia ya kutoa taarifa mapema kwa jeshi la polisi pindi wanapowahisi baadhi ya watu wasiowafahamu ili iwe rahisi kwa jeshi hilo kukabiliana na matukio kama hayo kabla ya kutokea uvunjifu wa amani.

Kamanda huyo amedai kuwa mbali na polisi kuwahi kwenye eneo la tukio hakuna mtu aliyekamwatwa kuhusika na uvamizi huo.

Monday, July 16, 2012

                                              AJALI YAUA 11 NA KUJERUHI 12 GEITA

                   
                                                                                                                                               
                                                                                                                                                                       
Baadhi ya marehemu waliopata ajali leo katika kijiji cha Chibingo wilayani geita mkoani hapa wakiwa wamehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti kwenye hospitali ya wilaya ya geita
Na Daniel Limbe,Geita
WATU 11 wamekufa papo hapo na wengine 12 wamejeruhiwa vibaya baada ya magari waliokuwa wakisafiria kugongana uso kwa uso katika kijiji cha Chibingo wilayani geita mkoani geita wakati gari moja aina ya Colola likiwa katika harakati za kulivuka gari lililokuwa mbele hali iliyosababisha kutokea kwa mauti hayo.

Ajali hiyo imetokea leo majira ya saa 6:30 mchana ikihusisha magari matatu  huku mawili yakiwa na abiria ambapo gari namba T 813 AZE iligongana na gari lenye namba za usajiri T 344 BPL wakati likitakka kuivuka gari yenye namba T 813  AZE aiana ya Land cluser lililo kuwa likitoka Katoro kuelekea mwanza.

Mbali na magari hayo madogo pamoja na kuwa na uwezo wa kubeba abiria watano,yamekuwa yakibeba zaidi ya watu 10 kwenye gari moja ambapo wengine hupakiwa kwenye buti kama mizigo amabpo baada ya ajari hiyo baadhi ya abiria walipoteza maisha yao papo hapo.


Mashuhuda wa ajari hiyo ambao hawakutaka majina yao yaandikwe gazetini wamedai kuwa chanzo cha ajari hiyo ni mwendo kasi wa madereva wa magari hayo almaarufu "MICHOMOKO".

Akithibitisha kuwepo kwa ajari hiyo Mkuu wa Polisi Usalama Barabarani Mkoa wa Geita John Mfinanga amesema kuwa waliokufa kwenye eneo la tukio ni watu 9 na wengine wawili walikufa wakati wakipatiwa matibabu kwenye hospitali ya Wilaya ya Geita.

Na kwamba kati ya waliokufa wanaume ni watano,wanawake watatu na watoto watatu akiwemo dereva wa moja ya magari hayo.

Aidha baadhi ya marehemu wa ajali hiyo ni pamoja na Baba na watoto wake watatu amabao ni Eliud Ngovongo (Baba) Amini aliud(mtoto),Emison Eliud(mtoto)na Sala Eliud(Mtoto) huku wengine wakiwa ni Ummy Charles,Masasila Benjamini na dereva wa moja ya magari yaliyopata ajari aliyetambulika kwa jina moja la James.

Wengine ni pamoja na Daniel Osca, na James waliofahamika kwa jina moja kila mmoja.

Mkuu wa Wilaya ya Geita Omari Manzie ameika katika chumba cha kuhifadhia maiti ilipo miili ya marehemu hao na kuonmyesha kusikitishwa na ajali hiyo huku akiahidi kuwashughulikia madereva wote watakaobainika kuvunja sheria za usalama barabarani kwa kushirikiana na jeshi la polisi.

Baadhi ya wananchi aakiwemo Waziri Joseph wamedai kushangazwa na wingi wa majeruhi hao hasa ikizingatiwa kuwa idadi ya maiti na majeruhi ikikusanywa inafikia abiria wa gari kubwa na kuiomba serikali kuingilia kati suala la madereva kujaza abiria kupita kiasi.

Saturday, July 14, 2012

                                        JIMBO LA MAGUFULI VIPANDE VIPANDE
                                        MHADHIRI WA CHUO KIKUU MZUMBE ATIMKIA CHADEMA
                                        MAKADA WENGINE SABA WASALIMISHA KADI ZAO

 Kushoto Mkurugenzi wa ulinzi na usalama Chadema taifa Bw, Wilfred Lwakatare akipokea kadi ya CCM na Kumkabidhi Kadi ya Chadema Dk Benedicto Lukanima (jana) muda mchache baada ya kujiunga na Chama hicho.

Na.Daniel Limbe,Chato.
MKURUGENZI wa ulinzi na usalama wa Chadema taifa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho mkoani Kagera Wilfred Lwakatare amezidi kuzibomoa ngome za Waziri wa Ujenzi Dk John Magufuli,baada ya wanachama 72 wa Chama cha Mapinduzi wakiwemo makada 8 wa chama hicho katika jimbo la Chato mkoa mpya wa geita kukihama na kujiunga na Chadema.
 
Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Chato kwenye mkutano wa hadhara jana Lwakatare alidai kushangazwa na uwezo wa Dk Magufuli kutunza takwimu za mambo mbalimbali ikiwemo wingi wa samaki ndani ya maziwa,mito,bahari sanjari na barabara zilizopo nchini lakini takwimu hizo zimeshindwa kuwasaidia wananchi wa jimbo lake katika kutatua tatizo kubwa la upatikanaji wa maji safi na salama licha kuwepo ziwa victoria katika umbali wa nusu kilometa.
 
Alisema kuwa Dk Magufuli hana uwezo wa kuwatumikia wananchi wake kutokana na kuwa kwenye chama cha watu mafisadi wasio na aibu ya mwenyezi mungu kutokana na baadhi ya viongozi wa serikali ya chama hicho kuhujumu raslimali za taifa na kuzificha nje ya nchi kwa lengo la kuongopa kufahamika kwa wananchi.
 
“Kama mnafuatilia vizuri vyombo vya habari,juzi bungeni kuna mbunge aliyeeleza wazi kuwa kunakiasi cha zaidi ya shilingi 300 bilioni zimeibwa na baadhi ya viongozi wa serikali na kuzificha kwenye benk ya uswis ili wananchi tusijue…kiasi hiki cha fedha ni kikubwa sana kiasi kwamba kwa bajeti nzima ya halmashauri ya chato ya mwaka 2012/13 kiasi cha bilioni 12…fedha hizi zilizoibwa iwapo zingetolewa kwenye halmashuri yenu zingetumika kwa miaka 24 pasipo serikali kutoa fedha.
 
Kauli hizo zilipelekea baadhi ya wanachama 72 wakiwemo makada wanane wa Chama cha Mapinduzi kukihama na kujiunga na Chadema hatua iliyotofasiriwa kuwa ni kuvunjwa kwa ngome za mbunge wa Chato,baada ya wanachama wengine 27 wakiwemo makada 7 wa chama hicho kukihama na kujiunga na Chadema mwezi mei 2012.
     
Baadhi ya makada wa CCM waliokihama chama hicho ni pamoja na aliyewahi kupambana na Dk Magufuli katika kinyang’anyiro cha kusaka nafasi ya kuwania ubunge wa jimbo hilo kupitia chama cha mapinduzi kwenye kura za maoni za mwaka 2010 Dk.Benedicto Lukanima ambaye pia ni mhadhiri wa chuo kikuu cha Mzumbe Morogoro ambaye alishika nafasi ya pili kati ya wagombea wanne wa chama hicho.
 
Wengine waliokihama cha hicho ni Cosmas Kabitelanya mwenyekiti wa kitongoji cha Nyisanzi,Mashaka Sululu kitongoji cha Dodoma,Charles Ngoloma kitongoji cha Nyasenga,kada aliyewahi kuwa mwenyekiti wa ccm tawi la Busaka mwaka 2006/08 Josephat Manyenye na aliyekuwa mjumbe wa mkutano mkuu  Uvccm mkoa Makonzere Phinias.
 
Wanachama hao walikihama cha hicho jana kwenye mkutano wa hadhara wa chadema uliofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Chato na kuhudhuria na mamia ya wakazi wa wilaya hiyo,ambapo walisema wamelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kuona CCM kinpoteza mwelekeo wa kisiasa kutokana na kukumbatia mafisadi waliohujumu rasilimali za Taifa huku wananchi wakibaki kuwa masikini wa kutupwa.
 
Mara baada ya kukabidhi kadi ya CCM kwa mgeni rasmi Dk.Lukanima alisema kuendelea kuwa kwenye chama cha mapinduzi ni sawa na kukubali kuendelea kuwa mtumwa hivyo hayupo tayari kuendelea kukaa kwenye chama ambacho tayari kimewakatisha tamaa wananchi kwa kuwasababishia umaskini wa kutupwa.
 
“Kukubali kuendelea kuwa ndani ya CCM ni sawa na kuwa mtumwa kwa kuwa wengi wao hujinufaisha matumbo yao kinyume na dhamira ya mwasisi wa chama hicho hayati Mwalimu Julias Nyerere ambaye alihitaji kuwa Chama cha wakulima na wafanyakazi..cha kutetea maslahi ya wanyonge…lakini kimekuwa cha kuwanyonya wananchi’’alisema Dk.Lukanima na kuongeza.
 
“Mimi na elimu yangu siwezi kuendelea kuwa ndani CCM kana kwamba nimelogwa..dunia imeniamini kuwa daktari elimu ambayo inategemewa na jamii kuisaidia katika kutenda mema..hivyo siwezi kukubali kula sahani moja na mafisadi huku wananchi wakiendelea kutaabika kwa kukosa huduma mbalimbali za elimu,afya na maji’’
 
Alisema moja ya malengo yake baada ya kukihama CCM na kujiunga na Chadema ni kuhakikisha anashiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kweli katika kuwakomboa wananchi wa Tanzania wakiwemo wa jimbo la Chato ambao wameshindwa kutengenezewa vichocheo vya kiuchumi ili kukabiliana na lindi la Umasikini unao wakabili.
 
Hatua hiyo imekuja huku kukiwa na taarifa ambazo hazijathibitishwa kuwa tayari kuna diwani mmoja maalufu katika halmashauri ya chato ambaye jina leke limehifadhiwa na kata anayotoka kuwa anajiandaa kulejesha kadi ya CCM na kujiunga na Chadema wakati wowote.
 

Sunday, July 8, 2012

                   SERIKALI YAWATAKA WAUZAJI MADAWA KUZINGATIA SHERIA


Baadhi ya wauzaji wa madawa muhimu ya binadamu wakiwa katika maandamano wakati wa   kuhitimu mafunzo ya siku 35 wilayani Chato.
Na Daniel Limbe,Chato
SERIKALI ya wilaya ya Chato mkoani geita imewataka wauzaji wa maduka ya dawa muhimu za binadamu kuzingatia sheria na taratibu za uendeshaji wa maduka hayo ili kunusuru vifo ambavyo vimekuwa vikitokea kutokana na wauzaji wengi kutokuwa na taaluma hiyo na kwamba serikali ya wilaya hiyo haitawavumilia watu wote watakaoendela kutoa dawa pasipo kuzingatia misingi ya sheria.
Akizungumza na wahitimu wa mafunzo ya utoaji wa dawa muhimu za binadamu jana (leo) Katibu tawala wa wilaya ya chato Cosmas Lugora alisema kwa muda mrefu wamiliki wa maduka ya dawa baridi ya binadamu wamekuwa wakiendesha shughuli zao pasipo kuzingatia baadhi ya taratibu na kanuni za utoaji wa dawa hali ambayo imekuwa ikihatarisha maisha ya wananchi kutokana na kupewa dawa pasipo maelekezo sahihi.
Alisema dawa ni tiba iwapo ikitolewa kwa kuzingatia taratibu lakini pia ni sumu iwapo itatumiwa kinyume hali ambayo inaweza kuhatarisha maisha ya wananchi na kusababisha kupoteza nguvu kazi ya taifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya mkurugenzi mkuu wa Mamalaka ya Chakula na dawa nchini,iliyotolewa na Meneja wa TFDA kanda ya ziwa Seth Kisenge uchunguzi uliofanywa na wizara ya afya  kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la Management Sciences for Health (MSH) mwezi aprili hadi mei 2001 walibaini ukiukwaji mkubwa wa utoaji huduma kwenye maduka ya madawa nchini,hali ambayo ilikuwa ikihatarisha maisha ya wananchi kutokana na tamaa za fedha kwa wamiliki wa maduka hayo.
Baadhi ya mambo waliobaini katika uchunguzi huo ni pamoja na wauzaji kutokuwa na elimu ya utoaji tiba,kuuza dawa moto na zisizosajiriwa kisheria badala ya dawa baridi za binadamu,kutoa mimba,kudunga sindano,kufunga vidonda na kulaza wagonjwa.
“Baada ya serikali kupitia mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) kwa kushirikiana na shirika lisilo la kiserikali la MSH tulibaini ikiukwaji mkubwa wa uendeshwaji wa maduka ya dawa baridi kutokana na kuuza dawa wasizoruhusiwa kisheria na kutoa huduma za kitabibu kinyume na maadili,hatua aliyopelekea seriakali kubuni mpango mkakati wa kuwaelimisha wamiliki na wauzaji wa maduka hayo”alisema
Kisenge alisema lengo la Mamlaka ya Chakula na dawa ni kuhakikisha wananchi wanapatiwa huduma sahihi kupitia kwa wauzaji dawa wenye ujuzi uliothibitishwa na serikali ikilinganishwa hali ilivyokuwa awali ambapo wauzaji wengi walikuwa wakitoa huduma hiyo kutokana na mazoea hali ambayo haitakiwi kisheria.
Alisema katika mafunzo maalumu ya wauzaji wa maduka ya madawa baridi ya binadamu ambayo yanatarajiwa kupandishwa hadhi na kuwa maduka muhimu ya dawa yameonyesha mafanikio makubwa zaidi hasa katika mkoa wa Ruvuma ambako utekelezaji wake ulianza tangu februali 2002.
Aidha alisema mpango huo umetekelezwa katika mikoa 15 ya Tanzania na kuonyesha mafanikio makubwa baada ya wauzaji hao kutambua sheria na kanuni za utoaji wa sahihi wa dawa,kuelewa mbinu za magonjwa yatokeayo mara kwa mara katika jamii,huduma kwa magonjwa ya watoto,stadi za mawasiliano na elimu ya ukimwi na ushauri nasaha.
Alizitaja mikoa zilizoinufaika mafunzo hayo kuwa ni Ruvuma,kigoma,Manyara Lindi,Mbeya,Shinyanga,Pwani ,Dododma,Mara,Iringa,Singida,Tanga,Mtwara,Morogoro na rukwa huku mikoa mingine sita ikiwemo Kagera ikiendelea kupatiwa mafunzo hayo kwa kuzingatia uwezo wa seriakali.
Mganga mkuu wa wilaya ya chato Dk Athanas Ngambakubi alisema mafunzo hayo ya siku 35 yatakuwa yamewasaidia kuongeza uelewa na mbinu sahihi za utoaji huduma kwa wagonjwa wao ukilinganisha na awali.
Vilevile Ngambakubi alisema iwapo dawa zikitumiwa kwa usahihi huleta matunda yaliyokusudiwa na dakatari  pamoja na  jamii,lakini kinyume chake zikitumika isivyofaa hugeuka na kuwa sumu hivyo husababisha madhara makubwa ambayo hayakukusudiwa.
Aidha katika risala ya wahitimu wa mafunzo hayo iliyosomwa kwa niaba yao na Rachel Kassawa walidai kabla ya mafunzo hayo walikuwa wakiuza dawa kiholela pasipo kuzingatia sheria namba moja ya mwaka 2003 na kanuni ya sheria hiyo namba 122 (H) na kwa,mba mafunzo hayo yamewafanya kutambua Sheria,Kanuni na Miongozo ya uendeshaji wa maduka ya dawa muhimu.
Hata hivyo katika mahafari hayo wahitimu 81 walioshiriki kwenye mafunzo hayo walitunukiwa vyeti vinavyotambuliwa na serikali kupitia wizara ya afya na ustawi wa jamii,hatua itakayowasaidia kuongeza soko la ajira yao sanjari na kukua kwa mishahara yao ukilinganisha ha ilivyo hivi sasa.

                                                                                                     Mwisho.