Tuesday, November 27, 2012



WATOTO SABA WANUSURIKA KUFA CHATO.



                       Waziri wa ujenzi Dk John Mafufuli akitoa maagizo ya kukamatwa mhudumu wa afya.

Na Daniel Limbe,Chato
WATOTO Saba wamenusurika kuawa kwenye hospitali ya wilaya ya Chato mkoani geita baada ya mhudumu wa afya Maliagoreth Kyaruzi kuwanyofolea maji yenye dawa (drip) wagonjwa waliolazwa kwenye wodi ya watoto kwa madai ya ndugu zao kukataa kufanya usafi wa vyoo vya hospitali hiyo.
 
Watoto walionusurika na vifo hivyo ni Edward Robert(4)mkazi wa kijiji cha Nyamirembe,Kashinje Lukanya(12) mkazi wa Busaka,Iren Nasib(3)mkazi wa Bwanga,Naomi Tumain(5) mkazi wa Kachwamba,Yunis William(3)mkazi wa Kasala,Astelia Siajali(2)mkazi wa Kahumo na Alphonce Makolobelo.
 
Tukio hilo la kusikitisha limetokea leo majira ya saa 2:30 asubuhi baada ya mhudumu huyo wa afya kuwataka ndugu za wagonjwa wote walilazwa kwenye wodi ya wanawake na watoto kwenda kufanya usafi wa vyoo kutokana na kuwepo kwa uchufu unaodaiwa kusababishwa na wagonjwa wenyewe.
 
Wakizungumza na Blog hii baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo William Masai na Ester Misungwi wamesema hatua hiyo ilikuja baada ya ndugu za wagonjwa kukaidi amri iliyotolewa na mhudumu huyo aliyewataka kuondoka ndani ya wodi hizo na kwenda kufanya usafi kwenye vyoo vya hospitali hiyo.
 
Baada ya wananchi hao kukaidi amri hiyo mhudumu huyo anadaiwa alilaejea na kuanza kunyofoa maji yenye dawa yaliyokuwa yamening’iniziwa kwa wagonjwa kwaajili ya matibabu kisha kuondoka ndani ya wodi hiyo huku akiwataka watu walioumizwa na kitendo hicho kushitaki popote watakapo ona panafaa.
 
Hatua hiyo iliwalazimu baadhi ya ndugu za wagonjwa waliolazwa hospitalini hapo kuutafuta uongozi wa haospitali hiyo kabla ya kuwasiliana na katibu wa mbunge wa jimbo la Chato Gelvas Stephano ambaye naye alizungumza na waziri wa ujenzi ambaye pia ni mbunge wa jimbo hilo ambaye alifika eneo la tukio akiwa ameongozana na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.
 
Kufuatia hali hiyo Waziri Magufuli alilazimika kuzungumza na wagonjwa,na watumishi wa afya kwa lengo la kusikiliza kero zao muda mchache baada ya kumaliza kujionea hali halisi ya watoto waliokuwa wamenyofolewa drip za dawa kisha kulejeshwa baada ya ndugu za wagonjwa kulalamika.
 
Kutokana na malalamiko mengi yaliyotolewa na wagonjwa kuhusu vitendo vinavyofanywa na mhudumu huyo Waziri Magufuli amelazimika kumwagiza mkuu wa wilaya ya Chato Rodrick Mpogolo kwa kushirikiana na Jeshi la polisi kuhakikisha wanamtafuta na kumkamata mtuhumiwa huyo kisha afikishwe mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.
 
“Bahati nzuri mkuu wa wilaya upo hapa,na Ocd na wewe upo hapa…ninaagiza huyo Maliagoreth akamatwe mara moja na kesho afikishwe mahakamani kujibu tuhuma za kutaka kuuwa wagonjwa saba kwa makusudi”alisema Magufuli
 
“Nasema huyo siyo mhudumu anayetakiwa kufanya kazi ya afya…maana kuwanyofolea drip wagonjwa kwa kosa la ndugu zao kukataa kufanya usafi wa vyoo haliwezi kufumbiwa macho….huyo maliagoreth hafai na ninaomba kuanzia leo asikanyage hapa kwenye hospitali kuja kuhudumia wagonjwa…maana ipo siku hata mimi ataninyofolea drip,naamini mmenielewa”alisema Magufuli na kushangiliwa na wagonjwa.
 
Kadhalika magufuli aliwataka waganga na wauguzi wengine kutoa huduma nzuri kadri ya inavyopaswa na kuwatahadhalisha iwapo watawahudumia wagonjwa vibaya kwa lengo la kulipiza kisasi kwa madai wagonjwa wamewashitaki kwake ambapo amedai kufanya hivyo itakuwa ni kutowatendea haki wagonjwa.
 
Vilevile amemwagiza mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Shaban Ntarambe kuhakikisha anamsimamisha kazi mara moja nesi huyo kwa madai hana sifa za kuendelea kuwa mtumishi kwenye wilaya ya chato.
 
Mkuu wa wilaya ya chato Rodrick Mpogolo mbali na kudai kusikitishwa na tukio hilo ameahidi kuunda tume maalumu itakayochunguza utolewaji wa huduma za afya kwa wananchi wanaofika kutibiwa hapo kutokana na kuwepo kwa malalamiko mengi.
 
Aidha amesema msingi wa serikali ni kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora na kwamba dosari zinazojitokeza atahakikisha zinapatiwa ufumbuzi wa kudumu ili kusijitokeza vitendo kama vilivyojitokeza.
 
Kwa upande wake Mganga mkuu wa hospitali ya wilaya hiyo Dk Pius Buchukundi amekiri  kutokea tukio hilo na kudai kuwa kitendo kilichofanywa na mhudumu wake siyo msimamo wa hospitali bali ni matakwa yake mwenyewe na kwamba atahukumiwa kwa matendo aliyoyatenda yeye mwenyewe.
 
Dk Buchukundi amewataka wagonjwa kutoa ushirikiano kwa uongozi wa hospitali hiyo ili kila kunapojitokeza mapungufu kama hayo yaweze kushughulikiwa haraka badala ya kukaa kimya na kuondoka wakinung’unika.
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment