Sunday, October 28, 2012


                      WANANCHI  GEITA WAKIFUATILIA HABARI KATIKA MAGAZETI

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya geita mkoani geita wakifuatilia habari mbalimbali katika magazeti kama walivyokutwa na mmiliki wa blog hii.Picha Daniel Limbe.

Saturday, October 27, 2012

                           WALIMU SENGEREMA WATWANGANA MAKONDE OFISINI.

Na Daniel Limbe,Sengerema
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida,walimu wawili wa shule ya msingi Igaka wilayani Sengerema mkoani mwanza wametwangana makonde ndani ya ofisi ya shule baada ya kurushiana maneno makali kutokana na mwalimu mkuu msaidizi kumtuhumu mwenzake kwa uwajibikaji mbovu.

Akizungumza na NIPASHE mwalimu mkuu wa shule hiyo Boniphace Shilunga amesema tukio hilo limetokea juzi oktoba 19 mwaka huu majira ya saa 8 mchana baada ya mwalimu Lazimani Manyabele kusukumiana makonde na mwalimu mkuu msaidizi Edson Kagusa.

Hatua hiyo ilitokana na majibizano ya maneno kati ya walimu hao wawili baada ya mwalimu mkuu msaidizi kumtuhumu mwenzake kuwa ni amekuwa akivunja sheria za kwa makusudi kutokana na kuchelewa kufika shuleni na kushindwa kuhudhuria kwenye vipindi kama alivyopangiwa.

Amesema baada ya kurushiana maneno ndani ya ofisi hiyo mwalimu Manyabele alinyanyuka mahari alipokuwa ameketi na kumkwida mwalimu mwenzake baada ya kumwita kuwa msaliti hatua iliyosababisha kumrushia konde lililopelekea majibizano ya ngumi hizo kabla ya walimu wengine kuingilia na kuwaachanisha.

Amedai kuwa mbali na sheria za nchi zinazowataka watumishi kuwahi kazini na kutimiza wajibu wao,shule hiyo tayari ilikuwa imejiwekea utaratibu wa walimu wote kufika shuleni kabla ya saa 2 asubuhi sanjari na kuhudhuria kwenye vipindi vyote vya masomo ikilinganishwa na ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wakifika shuleni saa 4 asubuhi na kuondoka pasipo utaratibu unaotakiwa.

Mratibu elimu kata ya Buzilasoga Robert Cheyo amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kudai kuwa tayari amekwisha andaa taarifa ya maandishi kwenda kwa ofisa elimu wa wilaya hiyo ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya walimu hao kwa madai kupigana maeneo ya shule ni kuidhalilisha shule na taaluma ya ualimu.
Amesema kamwe serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo kwa kuwa ni utovu wa nidhamu kazini na uzalilishaji wa taaluma ya ualimu kwa kuwa wao wanatakiwa kuwa kioo kwa jamii wanayoiongoza.

Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya sengerema Juma Mwanjombe aliupoulizwa na mwandishi wa habari hizi kuhusiana na tukio hilo alidai kuwa tayari ofisi yake imekwisha pokea taarifa ya sakata hilo huku akiahidi kuwachukulia hatua kali za kisheria walimu hao ili iwe fundisho kwa wengine wenye nia ya kama hiyo.

Mwanjombe alifafanua kuwa walimu hao wamevunja sheria namba 56 ya mwaka 2003 ambayo inawataka walimu kuwa na mahusiano bora kazini na kwamba inabainisha wazi kuwa atakaye vunja sheria hiyo adhabu yake ni kupewa onyo kali,kutelemshwa daraja la kazi,au kufukuzwa kazi.

Aidha ametoa wito kwa walimu wote wilayani humo kutii sheria na kuheshimiana kwa kuwa ndiyo silaha ya mahusiano kazini na kwamba serikali haitamwonea aibu mwalimu yoyote atakaye endelea kuvunja sheria zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba.
    DIWANI WA NGEREJA AGEUKA OMBAOMBA,APORWA GEST NGUO,SIMU NA FEDHA

Na Daniel Limbe,Sengerema
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida diwani wa kata ya Kasenyi wilayani sengerema mkoani mwanza Sindano Sanyiwa amegeuka omba omba baada ya watu wanaosadikiwa vibaka kumpora nguo,simu ya mkononi na fedha zote alizokuwa nazo.
Sakata hilo limemkumba jana majira ya saa 8 usiku akiwa amelala kwenye chumba namba 105 kwenye nyumba ya kulala wageni ya Nyakaduha Motel iliyopo nje kidogo ya mji wa sengerema wakati akihudhulia vikao vya baraza lahalmashauri hiyo.
Hatua ya diwani huyo kugeuka ombaomba imekuja baada ya mwenyekiti wa halmashauri hiyo Methew Lubongeja kumpa nafasi ya kuuliza swali kwenye kikao cha baraza la madiwani,ambapo diwani huyo kabla ya kuuliza swali aliomba kulijulisha baraza hilo kuwa ameibiwa nguo zake,simu ya mkononi na fedha zilizokuwa kwenye mfuko wa suluali yake.
Kutokana na hali hiyo aliwaomba madiwani wenzake kufanya harambee ili kumsaidia kupata kiasi cha fedha zitakazomwezesha kuendelea kumudu gharama za maisha wakati akiendelea na vikao vya baraza hilo hatua iliyopelekea madiwani hao kubwaga vicheko vingi kabla ya mwenyekiti wao kuwatuliza.
“Mheshimiwa mwenyekiti kwanza kabisa napenda kulijulisha baraza lako tukufu kuwa usiku wa kuamkia leo nikiwa nimelala kwenye chumba changu kuna watu wanaohisiwa kuwa ni vibaka walikata nyavu za dirisha la chumba hicho kisha kuniibia nguo zangu,simu ya mkononi na pesa taslimu nilizokuwa nazo,hivyo ninaomba madiwani wenzangu mnichangie changie kiasi chochote ili nami niendelee kushiriki na ninyi kwenye vikao vyetu”alisema Diwani huyo.
Hata hivyo mwenyekiti wa baraza hilo alifanikiwa kutuliza vicheko vilivyoambatana na makofi ndani ya ukumbi huo na kuwataka madiwani kumpa pole mwenzao kwa tukio hilo kwa kuwa linaweza kumtokea mtu yeyote pasipo kujali ni kiongozi.
Baada ya hatua hiyo diwani huyo aliendeliendelea na swali lake la msingi juu ya ujenzi wa barabara ya Kafundile kwenda kasenyi Rugongo yenye urefu wa kilomita 17 na daraja la Shitwego linaloungaisha vijiji vya Kasenyi na Rugongo ambalo limekatika na kuwafanya wakulima wa maeneo hayo kushindwa kusafirisha mazao yao kwenda kwenye soko kuu la mjini sengerema.
Vilevile alidai kuwa kutokana na hali hiyo baadhi ya wakulima,mama wajawazito na wazee wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kwaajili ya kufika kwenye soko kuu,hospitali ya wilaya na huduma zingine mhimu za kibinadamu zinazopatikana mjini sengerema.
Alidai kuwa licha ya barabara na daraja hilo kutangazwa na halmashauri hiyo kwaajili ya kumpata mkandarasi hakuna hatua zozote zilizoonekana kuchukuliwa ili kunusuru maisha ya wananchi wa kata ya Kasenyi ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia hali hiyo.
Kufuatia madai ya diwani huyo kuporwa mali zake NIPASHE limelazimika kufika kwenye Motel hiyo ili kupata ufafanuzi wa tukio hilo ambapo mbali na kukiri kuwepo kwa tukio hilo Meneja wa Motel hiyo Tindos Pangani amesema hatua hiyo imetokana na uzembe wa diwani huyo kwa kile alichodai alifungua dirisha na kuliacha wazi wakati akitaka kulala usiku.
“Tukio hilo lipo limetokea majira ya saa 8 usiku,lakini ninachoweza kusema ni kuwa diwani mwenyewe ndiye mzembe kwa maana wakati amelala alifungua dirisha na kuliacha wazi baadaya kuona kuna joto kali ndani huku akiwa kafungulia feni, hali iliyosababisha vibaka kupata njia rahisi ya kujipatia fedha”alisema Pangani.
Pangani amesema tukio hilo limetokea kwa mara ya pili tangu kufunguliwa kwa Motel hiyo takribani miaka 3 iliyopita na kwamba mazungumzo ya upotevu huo dhidi ya mteja wao yamefanyika na kupata suruhu.
                   WALIMU TISA WAISHI KWENYE NYUMBA MOJA SENGEREMA. 

                    Mkuu wa wilaya ya sengerema Bi Karen Yunus.(Picha   kwa hisani ya Blog)

Na Daniel Limbe,Sengerema.
KATIKA hali inayochochea misongo ya mawazo, walimu tisa wamejikuta wakiishi katika vyumba vitatu vya nyumba moja kutokana na uhaba wa nyumba.

Kufuatia hali hiyo, Baraza la Madiwani la Sengerema mkoani Mwanza limemuagiza Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwatafutia nyumba mara moja walimu walimu hao.

Walimu wanaodaiwa kuishi kwenye nyumba moja yenye vyumba vitatu ni wa Shule ya Msingi Soswa wilayani hapa mkoani Mwanza baada ya kuripoti eneo la kazi na kukuta uhaba mkubwa wa nyumba za walimu.

Hatua hiyo imekuja baada ya Diwani wa Kata ya Bulyaheke, Bageti Ngele kuwasilisha taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye kata yake ambapo alisema licha ya kuwepo mafanikio makubwa ya miradi, kata hiyo inakabiliwa na ukosefu wa nyumba za walimu kwenye baadhi ya shule za msingi na sekondari, akitoa mfano wa walimu tisa wa shule ya msingi Soswa kuishi kwenye nyumba moja.

Ngele alidai hatua hiyo imekuwa ikiwaathiri walimu hao kisaikolojia na kuwa vigumu kupunguza tamaa ya mwili itokanayo na tendo la ndoa licha ya mwalimu mkuu wa shule hiyo kuishi yeye na familia yake ndani ya nyumba hiyo ambayo hata hivyo haina dari.

Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,  Mathew Lubongeja alimwagiza Kaimu mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Juma Mwajombe kuhakikisha walimu hao wanaondolewa kwenye nyumba hiyo haraka wakati serikali ikijipanga kuondoa tatizo hilo.

“Kutokana na unyeti wa suala hili…mkurugenzi ninakuagiza uhakikishe walimu hao wanaondoka haraka kwenye nyumba hiyo ili ibaki idadi inayokubalika kwa kuwa hali hiyo inaweza kusababisha walimu hao kuathirika kisaikolojia…hii ni hatari sana,”alisema Lubongeja.

Aidha alisema jitihada za makusudi zinatakiwa kuchukuliwa ili kuhakikisha shule hiyo inaongezewa majengo ya nyumba za walimu haraka kwa kutumia fedha za serikali badala ya kuendelea kusubiri michango ya wananchi katika kutekeleza miradi hiyo.

Kaimu mkurugenzi huyo aliahidi kulishughulikia haraka suala hilo kwa kuzingatia taratibu na kanuni za utumishi wa Umma ili kuondoa adha inayowakabili walimu hao.

Alisema hatua hiyo inaweza kuathiri kiwango cha utoaji elimu kwa wanafunzi kutokana na walimu hao kuishi kwa misongo ya mawazo.